31.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Mdhamini wa Lissu ataka kujitoa mahakamani

KULWA MZEE-DAR ES SALAAM

MDHAMINI wa Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, Robert Katula, amedai mshtakiwa aliyemdhamini hana ushirikiano naye, hivyo anataka kujitoa kumdhamini.

Katula alidai hayo jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba baada ya kutakiwa kueleza hali ya mshtakiwa.

“Mheshimiwa sina la kusema zaidi, hatuna taarifa na mshtakiwa na hana ushirikiano kwa kweli, ikiwezekana nijitoe,”alidai.

Hakimu Simba alisema mdhamini huyo hawezi kujitoa wakati mshtakiwa hayupo mahakamani na kumruhusu Wakili wa Serikali Patrick Mwita kuwsilisha hoja zake.

Mwita alidai kama mdhamini hajui alipo mshtakiwa, mahakama iamuru mdhamini amlete mahakamani tarehe ijayo kama atataka kujitoa ndio ajitoe au itajulikana hapo hapo mahakamani.

“Mdhamini anasema haelewi huyo mshtakiwa yuko wapi, hiyo mheshimiwa inatupa shaka,” alisema.

Akizungumza mdhamini wa pili, Ibrahim Ahmed, alisema alifanya jitihada za kupata mawasiliano ya mshtakiwa ili ajue hali yake jambo ambalo limeshindikana, lakini kwa kuwa wajibu wake ni kutoa taarifa za mshtakiwa, atatoa na anaendelea kumfatilia.

Hakimu Simba baada ya kusikiliza hoja zote alisema ni kweli anachosema Wakili wa Serikali, kumbukumbu za mahakama ziko kimya, kesi imekwama.

“Jukumu la wadhamini ni kuijulisha mahakama, tunatarajia taarifa kutoka kwa wadhamini, kesi yetu imekwama,”alisema na kuahirisha kesi hadi Aprili 25.

Mbali na Lissu, washtakiwa wengine wanaokabiliwa na kesi hiyo ni Mhariri wa gazeti la Mawio, Simon Mkina, Jabir Idrisa na Mchapishaji wa Kampuni ya Jamana, Ismail Mehboob.

Lissu na wenzake wanakabiliwa na mashtaka matano ikiwamo la kuandika habari za uchochezi kinyume na Sheria ya Magazeti ya Mwaka 2002.

Inadaiwa kuwa Januari 12 hadi 14, 2016 katika jiji la Dar es Salaam, washtakiwa watatu, Jabir, Mkina na Lissu, kwa pamoja waliandika na kuchapisha taarifa za uchochezi zenye kichwa cha habari kisemacho, ‘Machafuko yaja Zanzibar’.

Katika shtaka la pili wanadaiwa kuwa Januari 14, 2016 katika jiji la Dar es Salaam, walichapisha habari hizo ili kuleta chuki kwa wananchi wa Zanzibar.

Mshtakiwa Mehboob anadaiwa kuwa Januari 13,2016 katika jengo la Jamana lililopo Manispaa ya Ilala, Dar es Salaam, alichapisha gazeti la Mawio lililokua na taarifa za uchochezi.

Alidai mshtakiwa huyo pia alichapisha gazeti hilo bila ya kuwasilisha hati ya sheria ya kiapo kwa Msajili wa Magazeti.

Mbali na mashtaka hayo washtakiwa hao kwa pamoja wanadaiwa kuwa Januari 14, 2016, Dar es Salaam, bila ya kuwa na mamlaka yoyote, waliwatisha na kuwatia hofu wananchi wa Zanzibar wasiweze kuingia kwenye marudio ya Uchaguzi Mkuu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles