23.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Mchungaji adaiwa kuuza viwanja, waumini watwangana

Ramadhan Hassan -Dododma

WAUMINI wa Kanisa la Assembles of God (TAG), Swaswa mkoani hapa, wamezitwanga kavukavu mara baada ya Mchungaji wa Kanisa hilo, Msafiri Malendaa kukamatwa na Jeshi la Polisi akidaiwa kuuza viwanja 13 vya kanisa hilo na fedha kutafunwa.

Mwandishi wa habari hizi ambaye alikuwapo katika eneo la tukio wakati wa vurugu hizo zilizotokea juzi katika kanisa hilo lililopo Mtaa wa Swaswa Mnarani, Kata ya Ipagala mkoani hapa, alishuhudia Mchungaji Malendaa akikamatwa na polisi wakati akiendesha ibada ya Jumapili.

Mara baada ya polisi kufika katika kanisa hilo saa 10.30 asubuhi wakiwa katika gari namba PT 4300, waliingia kanisani humo na kumchukua Mchungaji Malendaa na kumpakia katika gari hiyo na kuondoka naye.

Mara baada ya mchungaji huyo kuchukuliwa, ibada iliishia hapo hapo, waumini wakatoka nje ya kanisa na kuanza kuhoji ni kwanini amekamatwa huku baadhi yao wakianza kutwangana.

 Lidya Mgowela ambaye ni muumini wa kanisa hilo, alidai wakati vurugu hizo zikitokea alishangaa kuona katibu wa kanisa akikunjana na muumini.

“Nimetoa sadaka yangu, nilivyomaliza nikaona watu wanaanza kupigana, nikaogopa sana, nimekuja kutubu halafu kuna mambo haya, nipo hapa nje naangalia kinachoendelea ila ni mbaya sana, mimi sijui chochote, nimeumia,” alisema.

Wakizungumza na waandishi wa habari, baadhi ya waumini walisema Jiji la Dodoma lilibomoa kanisa hilo katika eneo la Swaswa Mnarani kupisha ujenzi wa barabara na kulilipa kifuta jasho viwanja 13 katika eneo la Ilazo Extension ili viuzwe na lijengwe kanisa jipya.

 “Tuliona ni sawa kwani alisema vikiandikwa jina la taasisi vitakuwa vigumu kuuzwa na kanisa lilipewa kiwanja kingine cha kujenga kanisa, hivyo kama tungeviuza vile tungepata fedha za kuendelea na ujenzi.

“Lakini alipoviuza fedha hakuna na hatujui kinachoendelea, ukimuuliza unafukuzwa kanisani,” alidai.

Naye Yona Mkopi alidai fidia waliyopewa na Jiji ni viwanja, lakini mchungaji kaviuza na fedha kuzitafuta.

“Hatuna imani naye, suala hili lipo kwa Mkuu wa Mkoa na Wilaya na hata Waziri Jafo (Selemani) alikuja hapa kanisani kwetu, ndiyo maana kachukuliwa na polisi, sisi tunataka viwanja vyetu,” alisema.

Akilitolea ufafanuzi suala hilo, Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Patrobas Katambi, alisema mgogoro huo anaufahamu na mara baada ya barabara kupita katika kanisa hilo, Jiji walitoa viwanja vya hisani ili waweze kuviuza na kuendelea na ujenzi wa kanisa mahali pengine.

“Maelezo ya mchungaji ni kwamba viwanja vile viandikwe kwa majina binafsi ili viweze kuuzika na fedha ziendelee na ujenzi, inawezekana hapa ndipo walipokosea, kama kuna mgogoro wameutengeneza wao sisi kama Serikali tuliishamaliza kuwapa viwanja,” alisema Katambi.

Naye Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Gilles Muroto alisema jambo hilo bado wanaendelea kufuatilia.

MTANZANIA ilimtafuta Mchungaji Malendaa ili alitolee ufafanuzi jambo hilo, lakini simu yake iliita bila kupokewa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles