30.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

MCB YADAI SERIKALI IPITISHE MISHAHARA, MADAI YA WALIMU KWENYE BENKI YAO

Na FERDNANDA MBAMILA-DAR ES SALAAM


UANZISHAJI wa Mwalimu  Commercial Bank mwaka mmoja  na nusu uliopita, ni uamuzi uliokuwa unasubiriwa na tasnia ya ualimu kwa muda mrefu ili  kuondokana na matatizo mbalimbali ya kiuchumi yanayowakabili walimu wengi mijini na vijijini.

Hali hiyo ni kutokana na kilio cha walimu kufanya kazi kwenye mazingira magumu kwa muda mrefu, huku mishahara na masilahi mengine kuwa madogo, jambo ambalo  limekuwa likiwafanya  kuishi maisha  duni kuliko wafanyakazi wengine wa Serikali na taasisi nyinginezo za umma.

Ni ukweli usiopingika kwamba, licha ya walimu kutoa mchango mkubwa katika maendeleo ya nchi  hasa  wafanyao kazi vijijini, bado wameshindwa kupata muda na mtaji ili kupata mapato ya ziada na waweze kujikimu au kufanya maendeleo ya taaluma yao.

Wazo la kuanzishwa Benki hii  ni walimu wenyewe walioona  umuhimu wa kuanzisha chombo hicho, baada ya baadhi yao kuzidiwa na mzigo wa madeni yaliyotokana na mikopo kutoka benki mengine  ili kujiendeleza kimaisha, hivyo pamoja na huduma hizo lakini zimewaongezea mzigo wa madeni.

Kuanza kwa MCB kumeleta matumaini mapya kwa vile itawasaidia waalimu kuwa na maisha bora, kwani licha ya kuwa wateja wa benki pia ni wanahisa wa benki hiyo. Hivyo uongozi wa  benki kuhakikisha wanatengeneza faida na pia ina bidhaa zinazowanufaisha wateja wao mahsusi, walimu ambao wengi wao wapo vijijini.

Itakumbukwa kuwa walimu wengi hapo zamani hasa wa vijijini walilazimika kusafiri hadi mijini kufuata huduma za fedha ikiwemo mishahara. Lakini hivi sasa huduma jumuishi za fedha zimeweza kusogeza huduma hadi ngazi za chini na hivyo kupata huduma hiyo.

MCB imeanza wakati huduma hii imezagaa nchini nzima na pia ina wateja wake kila pembe ya nchi  hadi mipakani. Huu ni mtaji mkubwa na mhimili wa benki kujenga mazingira bora ya kutengeneza faida ya benki hiyo na kuinua hali ya uchumi ya wanahisa wake.

Kwa mujibu wa Ofisa Mtendaji Mkuu,  Ronald Manongi, anasema mtaji uliotumika kuanzisha Benki hiyo ni Sh bilioni 31.

Anasema mtaji huu ni mkubwa, ni karibu mara mbili ya kiwango cha chini kinachotakiwa ili Benki Kuu ya Tanzania (BoT) iweze kutoa leseni.

“Uhitaji wa uanzishwaji benki ulionekana tangu awali hasa baada ya  Uongozi wa Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) kuisajili kwenye Soko la Hisa na kwa muda mfupi kukusanya  mtaji haraka,” anasema Manongi.

Anasema wanahisa wengi wa benki  hiyo ni mwalimu mmoja mmoja na kwamba ni dhahiri MCB ilianza shughuli zake sambamba  na mfumo wa kisasa wa kimataifa wa kutoa huduma za kifedha  jumuishi.

Mwalimu mmoja mmoja anamiliki hisa za benki asilimia 35.28; wakifuatiwa na wananchi kwa ujumla, 16.19, mifuko ya Hifadhi ya Jamii ya PSPF na NHIF, asilimia 16.17 kila mmoja; Chama cha Walimu (CWT)  asilimia (12.94 na Kampuni ya Maendeleo ya Walimu (Teachers’ Development Company Ltd) ina asilimia 3.23.

Huduma  jumuishi ni ile inayowaunganisha watu wa kipato cha chini  katika mfumo wa kibenki na kunufaika na matumizi rafiki ya mtandao wa kidigitali kwa gharama nafuu na usalama wa miamala hiyo.

Mkurugenzi Mkuu huyo anasema wakati   menejementi   ya   MCB  inajitahidi   kuwa  na  mikakati ya kuikuza   benki   hiyo ili   kuwafikia   walimu   wengi   waliotapakaa   kila kona ya Tanzania, bado inakabiliwa na ushindani wa vyombo vya fedha vilivyowakopesha   walimu   hao   kuendelea   kuwashikilia   ili waendelee kuwa wateja wao kwa hofu ya kupunguza wateja wao.

“Ni wajibu wa Serikali kuwa karibu na Benki hii ili kuunga mkono juhudi za uwekezaji wa ndani uliofanywa na waajiriwa wao. Kwa kufanya   hivyo   itaweza   kuwasaidia wananchi   wake   kuboresha maisha ya   wananchi   wake   na   faida   itokanayo na benki   hiyo  itaweza kusaidia jamii kwa kuelekea uchumi wa kati,” anasema Manongi.

Anasema  maamuzi  mengi yanayoweza kufanywa na  Serikali kuisaidia benki hiyo kukua haraka likiwemo lile la kupitishia mishahara ya walimu kwenye benki yao.

Manongi anasema mbali na njia hiyo, pia malipo mengine yakiwemo madeni wanayoidai Serikali   yangeweza   kuwapa   morali   walimu   ili

kuendelea kuitumikia nchi yao kwa moyo  mmoja.

Anatoa pongezi kwa manejimenti ya MCB kwa kufikia makubaliano ya kufanya kazi pamoja na Benki ya Posta (TPB) kwa kile anachodai hizi ni benki za kizalendo, hivyo lazima tukubali kuwa  benki zinazoanzishwa na  Watanzania kwa manufaa ya Watanzania lazima zikidhi haja ya Watanzania.

“Ushuhuda kutoka kwa wateja, wanasema  wanapotaka  kuongeza amana kwenye akaunti zao, huenda  tawi la Benki ya Posta lililoko jirani na kujaza fomu. Mara karani wa benki anapomaliza kuingiza   taarifa   za   mteja   kwenye   kompyuta, hapo   kwa   hapo muamala umekuwa umekamilika kupitia kwenye mtandao,” anasema mkurugenzi huyo.

Anazitaja huduma  zinazotolewa na MCB   kuwa   mikopo   kwa   mtu   mmoja   mmoja   na makundi madogo madogo, jambo  ambalo anasema linawavutia  wateja wengi ni masharti  rahisi  ya   upatikanaji   wa   mikopo   ili   kukidhi   mahitaji   ya mwombaji.

“Mikopo   inaambatana   na   masharti   rahisi na inaweza kulipwa kwa kipindi cha miezi 72,” anasema Manongi.

Akizungumzia mipango   ya   baadaye   ya   benki   hiyo, Manongi anasema wamedhamiria kuwafikia wananchi wenye kipato cha chini ambao ndio tegemeo la ukuaji wa benki hiyo.

Anasema kwa sasa maombi ni mengi na kinachosubiriwa ni kibali cha Benki Kuu ya Tanzania kutekeleza mikakati hiyo kutokana na kuwa   benki ipo imara.

“MCB si benki pekee ya walimu duniani, kuna mabenki mengine kama   hayo   nchi   nyinginezo     zikiwemo   zile  zilizoendelea. Ni vyema   menejementi   ya   Benki   ikaangalia   namna   ya   kujifunza  kutoka   huko   ili   kuboresha   benki   hii   na   ikiwezekana   kuhamisha teknolojia  na mifumo ili ziweze kuijenga MCB kuwa ya kisasa zaidi,” anasema mkurugenzi huyo.

Anasema jukumu jingine la Menejimenti ya MCB ni kutayarisha mkakati wa   mawasiliano   na   kujitangaza   hasa   kwa   wananchi   wa   vijijini, ambapo kuna mahitaji makubwa ya huduma za benki ili kwenda  sambamba na mfumo uliozinduliwa na Benki Kuu hivi karibuni wa mpango wa huduma jumuishi za fedha kufika vijijini.

Anatoa wito   kwa   wanahisa   ambao ni walimu   kwani wamekuwa   wakitumika   katika kampeni   mbalimbali   za   kitaifa, hivyo   ni   vyema   kama   wanahisa wakaunga   mkono   na   kuwasiliana   na   menejimenti   ya   benki kuhamasisha   wananchi   kujiunga   na   benki   yao   ili   kuinua   hali   za maisha yao.

Manongi anasema ni vyema MCB ikaangalia huduma za kifedha ambazo zinalenga kuwekeza kwenye elimu ili kuinua viwango vya elimu ya wanahisa  na   familia   zao   ambapo   mara   nyingi   tunashuhudia   baadhi   yao wakihangaika   kutafuta   mikopo   kwa   ajili   ya   kugharamia   ada   za mafunzo ya familia za wanahisa katika ngazi mabalimbali za elimu.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles