24.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

MBUNGE CUF AMWANGUKIA RAIS MAGUFULI

Na Hadija Omary – LINDI           |           


MBUNGE wa Mchinga, Hamidu Bobali (CUF), amemwomba Rais Dk. John Magufuli, kuingilia kati na kuona jinsi agizo la Rais mstaafu Jakaya Kikwete alilolitoa mwaka 2010 lilivyopuuzwa kuhusu ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Lindi.

Amesema mwaka 2010 Rais mstaafu Kikwete, alitoa agizo la kupandishwa hadhi kwa Kituo cha Afya Kitomanga na kuwa Hospitali ya Wilaya, lakini hadi sasa hakuna utekelezaji wake.

Akizungumza na waandishi wa habari jana mjini hapa, alisema kikao cha Baraza la Madiwani cha robo ya nne ya mwaka 2017/18, liliamua hospitali hiyo kujengwa Kata ya Kiwalala bila kujali kuwa ujenzi wa hospitali hiyo ulikuwa ni utekekezaji wa agizo la Rais.

Kutokana na hali hiyo, alisema wananchi wa Mchinga wanamwomba Rais Dk. John Magufuli, kuingilia kati suala hilo ili Serikali iweze kulitekeleza.

“Kwa mujibu wa kanuni, Rais akitoa maagizo ya jambo fulani litekelezwe, hakuna mtu au kundi la watu ambao wanaweza kutengua maamuzi hayo isipokuwa Rais mwenyewe. Hivyo basi huwezi kubadilisha jambo hilo kama Rais hajatengua, sasa tunashangaa huu ujasiri wa kubadilisha ujenzi wa kituo cha afya wanaupata wapi?” alisema na kuhoji Bobali.

Alisema upanuzi wa kituo cha afya kuwa hospitali ya wilaya ungesaidia kwa kiasi kikubwa kuongeza huduma katika jimbo hilo na maeneo ya jirani ambayo kwa kiasi kikubwa wanataabika kutafuta huduma za afya kwa kutembea umbali mrefu.

Bobali alisema ikiwa agizo hilo la Rais litashindwa kutekelezwa, wananchi wa Mchinga watajaza fomu maalumu na kuisaini, ya kuomba kujitoa Halmashauri ya Lindi na badala yake wahamie Manispaa ya Lindi ambako wanahisi wanaweza kutendewa haki.

Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Kitomanga, Hamisi Msagula (CUF), alisema kituo hicho cha afya ambacho kilitarajiwa kuwa hospitali ya wilaya, kingekuwa mkombozi kwa wananchi wa maeneo yake, vijiji na vitongoji mbalimbali vya Halmashauri ya Lindi.

Alisema hatua ya kukosekana kwa hospitali huwalazimu wananchi kufuata huduma za afya Wilaya ya Kilwa au Manispaa ya Lindi, huku wenzao wa Mtama wakipata huduma za afya kwa urahisi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles