25 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

MBUNGE CCM KIZIMBANI KWA RUSHWA

 

Mwandishi Wetu


MBUNGE wa Kishapu, Suleiman Nchambi (CCM) na wenzake wawili, wamefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Biharamulo wakikabiliwa na mashtaka ya kutoa na kupokea rushwa.

Nchambi na wenzake Clara Mwaikambo, aliyekuwa Meneja wa Fedha wa Kampuni ya Stamigold na Yasin Abdala, Msimamizi wa Kampuni ya Junior Construction, walifikishwa katika mahakama hiyo jana na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).

Washtakiwa hao walifikishwa mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Biharamulo, Flora Ndale, na kusomewa mashtaka dhidi yao na mwendesha mashtaka wa Takukuru, Dismas Muganyizi.

Abdala na Nchambi ambaye pia ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Junior Construction, wameshitakiwa kwa kosa la kutoa rushwa ya Sh milioni tano kwa aliyekuwa Meneja wa Fedha wa Stamigold, Clara Mwaikambo, Oktoba 21, 2016.

Ilidaiwa Abdala na Nchambi walimpa Clara fedha hizo kutokana na yeye kuwawezesha kupata malipo ya Dola za Marekani 170, 945.18  sawa na Sh milioni 390 kwa kazi hewa ya kuchimba udongo wenye madini ya dhahabu  mwaka 2015 ikiwa ni kinyume na makubaliano yaliyopo kwenye zabuni waliyopewa na Stamigold.

Stamigold ni kampuni ya uchimbaji dhahabu wilayani Biharamulo iliyoanzishwa mwaka 2013 na inamilikiwa na  Serikali kupitia Shirika la Madini la STAMICO lenye hisa asilimia 99  na Msajili wa Hazina mwenye hisa asilimia moja.

Wakati Nchambi na Abdala wakitetewa na mawakili wa kujitegemea Nassoro Mbilikilya na Frank Mwalongo, Clara anatetewa na wakili Francis Jesse.

Washtakiwa hao wako nje kwa dhamana ya Sh milioni tano na watumishi wa Serikali wawili na kesi hiyo itakuwa  mahakamani Septemba 3 kwa ajili ya kutajwa.

Washatakiwa hao walikamatwa Agosti nne na kuwekwa rumande katika Gereza la Wilaya ya Biharamulo mpaka jana walipopandishwa kizimbani.

Nchambi anakuwa mbunge wa tano katika awamu hii kupandishwa kizimbani kwa tuhuma za rushwa.

Mapema mwaka 2016, Kangi Lugola (Mwibara), Sadiq Murad (Mvomero) na Victor Mwambalaswa (Lupa), walifikishwa mahakamani  na kusomewa shitaka la kuomba rushwa ya Sh milioni 30 kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Gairo mkoani Morogoro, Mbwana Magote.

Wabunge hao ambao walikuwa wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), walidaiwa Machi 15, mwaka 2016  kati ya saa 2:00 na 4:00 usiku katika Hoteli ya Golden Tulip iliyopo Masaki, jijini Dar es Salaam, wakiwa wajumbe wa kamati hiyo, walimshawishi Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Gairo, Mbwana Magote, kutoa rushwa ya Sh. milioni 30.

Washtakiwa hao walidaiwa kushawishi kupewa rushwa ili wapitishe mapendekezo ya hesabu za halmashauri hiyo ya mwaka 2015/2016.

Hata hivyo, washtakiwa walikana mashtaka hayo na upande wa Jamhuri ulisema upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika.

Siku mbili baadaye,  Mbunge wa Sumve (CCM), Richard Ndassa (56) naye alifikishwa mahakamani hapo kujibu mashtaka mawili; kuomba rushwa ya Sh milioni 30 kutoka kwa aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Felchesmi Mramba na kumshinikiza kiongozi huyo kuwafungia umeme ndugu na rafiki zake.

Ndassa alipandishwa kizimbani ikiwa ni siku chache tangu ang’olewe uenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Uwekezaji na Mitaji (PIC) na Spika, Job Ndugai katika mabadiliko aliyosema ni ya kawaida.

Katika shtaka la kwanza, Ndassa alidaiwa kuwa siku ya tukio kwa nafasi yake ndani ya PIC, aliomba rushwa ya Sh milioni 30 kutoka kwa Mramba ili kamati yake iweze kutoa hati safi ya ukaguzi wa ripoti ya hesabu za mwaka 2015/2016 kwa shirika hilo.

Katika shtaka la pili, ilidaiwa kuwa siku hiyohiyo, mshtakiwa huyo alimshinikiza Mramba kumpatia umeme ndugu yake Ndassa, aliyetajwa kwa jina la Matanga Mbushi na rafiki yake Lameck Mahewa ili kamati yake iweze kutoa hati safi ya ukaguzi wa ripoti ya hesabu ya mwaka 2015/2016 kwa shirika hilo.

Mshtakiwa alikana mashtaka na Wakili Lekayo aliieleza mahakama kuwa upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika hivyo akaiomba mahakama ipange tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa kwa kesi hiyo.

Hata hivyo baadaye Jamuhuri ilisema haina nia ya kuendelea na kesi hizo hivyo kesi hizo zikafutwa.

 

 

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles