24.1 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Mbunge Bobi Wine aisimamisha Uganda

Kampala

MBUNGE wa Kyadondo, Robert Kyagulanyi, maarufu kama Bobi Wine, jana alilisimamisha kwa muda jiji la Kampala baada ya polisi kuonekana kuranda randa mitaani kuhofia kuzuka kwa gasia wakati akiwasili nchini humo akitokea Marekani kwenye matibabu.

Mara tu baada ya kushuka Uganda na ndege ya Kenya Airways, Bobi Wine, alipakizwa kwenye gari ya jeshi na kupelekwa kijijini kwake Magere.

Awali mwanamuziki huyo aliyegeuka mwanasiasa aliapa kukaidi amri hiyo iliyotangazwa mapema akieleza kuwa yeye ni raia huru wa Uganda mwenye haki zote za kutembea kokote hivyo asipangiwe nani ampokee na aende wapi.

Bobi Wine aliyekwenda Marekani kwa ajili ya matibabu baada ya kudai kupigwa na kuteswa wakati akiwa mikononi mwa polisi, alisema kurejea kwake Uganda hakuwahusu polisi, hawapaswi kuhoji nani atampokea.

“Nimekuwa najiuliza kwa nini hawa maofisa wa polisi wanakubali kujidhalilisha kiasi hicho. Wanataka kuamua nani aje kunipokea na wapi nielekee baada ya kuwasili?” Alihoji.

Vyombo vya habari nchini Uganda vimemnukuu msemaji wa polisi, Emilian Kayima aliyewaambia waandishi wa habari kuwa atakapowasili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa Entebbe, mbunge huyo atapokelewa na familia yake na atapatiwa ulinzi kutoka uwanja wa ndege mpaka nyumbani.

Awali Wine alisema kuwa alihofia kurudi Uganda “kutoka na namna serikali ivyolikuwa ikiendesha shughuli zake”.

Aliyasema hayo kwenye uwanja wa ndege wa kimataifa wa Jomo Kenyatta mjini Nairobi kabla ya kuendelea na safari yake kwenda Uganda

Bobi Wine, anakabiliwa na mashtaka ya uhaini akidaiwa kuhusika katika tukio la kupigwa mawe msafara wa Rais Yoweri Meseveni wakati wa kampeni ya uchaguzi mdogo.

Mapema nduguye Wine Eddy Yawe na naibu msemaji wa chama cha Democratic party, Waiswa Alex Mufumbiro, walikamatwa na vikosi vya usalama na kuzuiwa kwenye kituo cha polisi uwanja wa Entebbe.

Ripoti pia zinasema kuwa kila mtu wa familia aliyewasili uwanja wa Entebbe alikamatwa, licha ya polisi kusema awali kuwa watawaruhusu watu wa familia kumkaribisha Bobi Wine.

Tangu atangaze kurudi Uganda, makamanda wa polisi mjini Kampala wamekuwa wakifanya mikutano tangu Jumatatu kujiandaa kurudi kwa mbunge huyo.

Mapema jana taarifa za polisi zilisema kuwa vikosi vya kupambana na ghasia vimepelekwa kwenye barabara ya Entebe, katikati mwa mji wa Kampala, Kamwokya (alikokulia Bobi Wine na Kasangati.

Kiwango kikubwa cha polisi kilipelekwa kwenye barabara ya kutoka Kampala kwenda Entebbe ambapo watu wanaweza kukusanyika kumuona Bobi Wine.

Polisi walisema Bobi Wine hajapewa kibali cha kufanya mkutano au shughuli yoyote.

Msemaji wa polisi mjini Kamapala Luke Owoyesigyire, alionya kuwa yeyote ambaye atashiriki kwenye shughuli yoyote inayomhusu Bobi Wine atakamatwa

Kwenye video aliyoiweka  kwenye mtandao wa Facebook, Bobi Wine alisema serikali inapanga kuzua ghasia ili kuwalaumu wafuasi wa chama cha People Power.

Kulinganga na Bobi, baadhi ya watu wanachapisha shati nyekundu za wafuasi wa People Power na kuwapa majangili wa serikali ili wapate kuzua ghasia ndio waonekane kuwa wao ni wafuasi wake.

Bobi Wine amekuwa nchini Marekani kwa muda wa siku 18, baada ya kuruhusiwa kwenda kupata matibabu tarehe 31 Agosti.

Alidai aliteswa vibaya baada ya kukamatwa kutoka Hoteli ya Pacific mjini Arua alikokuwa akifanya kampeni ya uchaguzi.

Alifikishwa mbele ya Mahakama ya Kijeshi huko Gulu kwa kumiliki silaha kinyume na sheria mshataka ambayo yalifutwa baadaye.

Akiwa nchini Marekani Bobi Wine alifanya mikutano kadhaa na waandishi wa habari, akihojiwa na vituo vingi vya televisheni za kimtaifa na kuhudhuria misa na raia wa Uganda wanaoishi huko Boston.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles