23.7 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Mbunge ataka wabakaji kuhasiwa

RAMADHAN HASSAN

MBUNGE wa Viti Maalumu, Zainab Katimba (CCM) amependekeza mbakaji apewe adhabu ya kuhasiwa ili asije akarudia tena kosa kama hilo ambalo linaleta ukatili mkubwa kwa wanawake na watoto kutokana na kuwaathiri.

Lakini Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Profesa Adelardus Kilangi, amesema kuruhusu adhabu ya kuhasiwa kwa watuhumiwa wa makosa ya ubakaji na ulawiti ni kuvunja katiba ya nchi na kwamba adhabu zilizopo zinajitosheleza.

Alisema ibara ya 13 ibara ndogo ya 6 ya katiba inasema ni marufuku kwa mtu kuteswa, kuadhibiwa kwa kinyama au kupewa adhabu zinazomdhalilisha hivyo pendekezo hilo likichukuliwa ni kuvunjwa kwa katiba.

Kauli hiyo aliitoa bungeni jana wakati akijibu swali la nyongeza la Katimba (CCM), ambaye alisema kuna changamoto kubwa sana ya ukatili wa wanawake na watoto kwenye masuala ya ubakaji wakati Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inataka kuwahakikishia usalama Watanzania wote.

Katimba alisema kwenye makosa ya ubakaji kama ilivyoainishwa kwenye kifungu cha tano cha Sheria ya Sexual offences ya mwaka 1998 ambayo imeenda kufanya marekebisho ya kifungu cha 130 cha sheria ya adhabu ya ubakaji.

”Kigezo au masharti ya kuthibitisha kosa la ubakaji ni mpaka yule aliyebakwa athibitishe kwamba kulikuwa na kuingiliwa, na mazingira hayo ni magumu sana katika utaratibu wa kawaida kuthibitisha kwamba mtu amekuingilia, hasa kwa watoto.

“Je, Serikali haioni katika mazingira haya kwamba kufanyike marekebisho ya sheria ili vigezo vya kuthibitsiha au kuthibitisha kosa la ubakaji ipunguzwe kiwango chake ili kusiwe na haja ya kufanya hivyo sababu watoto sio rahisi kwao kuweza kuthibitisha jambo kama hilo na mazingira yaangaliwe ili kuweza kutoa haki?

“Serikali haioni kwamba kuna haja ya kuongeza adhabu kwa wale watakaothibitika kwamba wamefanya kosa la ubakaji ili adhabu yao iwe kali ili kuhakikisha kwamba makosa haya ya ubakaji yanakwisha ili watu waogope?” aliuliza Katimba.

Alitolea mfano kuwa Serikali haioni kwenye kosa la ubakaji, mbakaji apewe adhabu ya kuhasiwa ili asije akarudia tena kosa kama hilo ambalo linaleta ukatili mkubwa kwa wanawake na watoto kutokana na kuwaathiri.

Akijibu maswali hayo, Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Augustine Mahiga alisema kuwa wameondoa baadhi ya vigezo vilivyokuwepo hasa watoto kutoa ushahidi wenyewe na kuachia mahakama uamuzi wa busara na wa kitaalamu kuweza kutoa ushuhuda huo kama kitendo hicho kimetokea.

Alisema kuwa kwa sasa kuna mfumo wa kutazama na kuboresha mfumo mzima wa kesi za jinai likiwamo suala la ubakaji na kama itatoa mapendekezo yatafuatana na adhabu.

”Lakini niwaambie kweli kwamba kwenye makosa haya adhabu ambazo zipo mpaka sasa ni kali na inafika mpaka miaka 30 na limejadiliwa bungeni, hivyo kama itabidi kuongeza adhabu hizo baada ya marekebisho na mapitio ya sheria hizi ninashauri kwamba Bunge hili likae na tushauriane kwakuwa linahitaji uamuzi wa kisheria,” alisema Dk. Mahiga.

Akitoa majibu ya nyongeza, Profesa Kilangi alisema sheria inayohusu mambo ya jinai ilipopitishwa mojawapo ya masuala iliyoyaondoa kwenye sheria ya ushahidi ilikuwa ni kifungu kinachoeleza ni lazima kuonyesha ishara fulani zilizosalia baada ya tendo la ubakaji jambo ambalo lilikuwa linadhalilisha.

Alisema mwisho ni lazima hayo yote yafuate misingi ya sheria za jinai, kwamba lazima kuomba kuthibitisha pasipo kuacha shaka na kwamba anayetuhumiwa asituhumiwe au kupewa adhabu isivyo sahihi.

”Na kwenye hili suala la kuongeza adhabu tayari sheria ile imeiongeza adhabu imekuwa kali sana ambayo ni miaka 30, sasa hili pendekezo la kuhasiwa lina tatizo moja, litatupelekea kuvunja katiba.

“Kwa sababu ibara ya 13 ibara ndogo ya 6 inaeleza kwamba ni marufuku kwa mtu kuteswa kuadhibiwa kwa kinyama au kupewa adhabu zinazomdhalilisha, kwahiyo tukichukua pendekezo la kuhasiwa linatupeleka tena kwenye upande mwingine ambapo tutavunja katiba kwakuwa adhabu zilizopo zinajitosheleza,” alisema Profesa Kilangi.

Naye, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu alisema hata ziwepo sheria kali kiasi gani, matatizo ya ubakaji nchini hayataisha kutokana na kuwa ni suala la malezi.

Aliwataka wazazi, walezi na jamii kutimiza wajibu wa malezi na ulinzi wa watoto huku akitolea mfano kuwa kuna watoto wanabakwa miezi mitatu bila mzazi kujua, hivyo kuwataka wawakague, wawaulize na kuwafuatilia ili waeleze matatizo wanayopata.

Awali katika swali la msingi, Katimba alihoji kuwa Serikali haioni ni wakati mwafaka wa kuleta bungeni marekebisho ya sheria ili kupunguza kiwango cha ushahidi kwenye kesi za ubakaji na hasa wa watoto.

Akijibu swali hilo, Dk. Mahiga alisema suala la ushahidi katika kesi za jinai husimamiwa na Sheria ya Ushahidi, Sura ya 6.

“Makosa ya ubakaji hususan kwa watoto wenye umri chini ya miaka 18 yaadhibiwa kwa mujibu wa kifungu cha 130(1) na 131(2)(e) cha kanuni ya adhabu, sura ya 20,” alisema Dk. Mahiga.

Alisema kuwa makosa haya kwa mujibu wa Sheria ya Ushahidi yanahitaji kuthibitishwa pasipo kuacha shaka yoyote ili mtuhumiwa atiwe hatiani.

Dk. Mahiga alisema kwa kuwa kiwango cha kuthibitisha mashauri ya jinai ni pasipo kuacha shaka yoyote, kiwango cha ushahidi kitategemea mazingira ya kosa husika, namna lilivyotendeka na mashahidi walioshuhudia kutokea kwa tukio hilo. Sheria haijatoa masharti ya idadi ya mashahidi wanaotakiwa kutoa ushahidi.

“Hivyo, kila kesi uangaliwa kwa kuzingatia mazingira yake na kwamba pamoja na hayo, na kwa lengo la kumlinda mtoto aliyeathirika na tukio la ubakaji, mwaka 2016 Bunge lako tukufu lilifanya marekebisho katika kifungu cha 127 cha Sheria ya Ushahidi, kwa kuondoa masharti ya kumhoji mtoto ili kupima ufahamu wake na badala yake kuweka masharti ya mahakama kujiridhisha kuwa mtoto ana uwezo wa kusema ukweli pekee.

”Hivi sasa Serikali inaendelea na itaendelea kufanya maboresho ya mfumo wa haki jinai ili kuondoa vikwazo vyote vinavyokwamisha usikilizwaji, si tu wa mashauri ya namna hii, bali mashauri yote yanayohusu makundi ya watu katika jamii yetu ili kulinda utu wao, ikiwemo watoto, wanawake, wazee na watu wenye ulemavu wanaoathirika na vitendo vya ukatili ikiwa ni pamoja na ubakaji,” alisema Dk. Mahiga.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles