27.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 16, 2024

Contact us: [email protected]

Mbowe amshangaa DC Sabaya

ANDREW MSECHU

MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe amesema anamshangaa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya kuzuia na kubadili matumizi ya Sh milioni 42 za Mfuko wa Jimbo la Hai.

Amesema kutokana na hali hiyo, hataki kulizungumzia kwa kina.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Mbowe alisema hawezi kuzungumzia suala hilo kwa kuwa Sabaya hana mamlaka ya kufanya hivyo.

“Sina comment katika suala hilo kwa sababu DC (mkuu wa wilaya) Sabaya hana mamlaka kama hayo,nikianza kuzungumzia mambo yasiyofaa kama hayo na mimi nitakuwa kama yeye, nadhani nimemaliza,” alisema kisha kukata simu.

OLE SABAYA 

Akizungumza na MTANZANIA jana, Ole Sabaya alisema amechukua hatua hiyo kwa kuwa mbunge alipaswa kuitisha kikao ili kuidhinisha fedha hizo zipangiwe matumizi yake tangu Desemba 2018, lakini kipindi chote hicho hajafika.

Alisema taarifa aliyanayo, ni kwamba mbunge Mbowe alipiga simu kama ambavyo amezoea kufanya na kuagiza fedha hizo zigawanywe kila kijiji Sh 500,000, yeye aliona suala hilo haliwezi kufanyika bila muhtasari kwa kuwa watahitajika kuandika ripoti ya matumizi ya fedha hizo.

“Sheria inasema katika mazingira ya kawaida mbunge aje ajadiliane na wajumbe na wakubaliane kipaumbele fedha zitakwenda wapi. Kwa maagizo yake kuwa ziende kila kijiji, mimi nasema tunataka uthibitisho wanapogawanya itakuwa inachochea maendeleo yapi kwa sababu ile ni catalyst fund (fedha ya uwezeshaji) kwa h maelekezo yapo, lazima na mimi nijiridhishe. 

“Tunapofanya return (kuwasilisha taarifa ya mapato na matumizi), maana yake ule ukaguzi utaonyesha utaratibu upi? muhtasari upi watu walikaa wakaridhia kwa hiyo kwa utaratibu huo,nikazuia fedha hizo,” alisema.

Sabaya, alisema hata maelekezo aliyotoa Mbowe hayana muhtasari kwa sababu katibu wa kikao na mtekelezaji ni ofisa mipango wa wilaya na ndiye aliyepigiwa simu.

 “Kwa hiyo huwezi kumpigia ofisa mipango simu na kumwambia pelekeni kijijini kwa sababu muhtasari ndiyo ushahidi,fedha hizo zilitumika vipi, hatuwezi kuoperate (kuendesha) kwa simu bwana,” alisisitiza.

Alisema tangu alipohitajika kuitisha kikao kwa ajili ya kupitisha matumizi ya fedha hizo Desemba 2018, hadi jana hajaitisha kikao hicho.

Alisema aliona katika mazingira hayo, kuna walimu wanachangia choo na wanafunzi ambao wote wako Wilaya ya Hai na ndani ya jimbo hilo hilo.

“Kisailkolojia na katika mazingira ya kawaida, walimu hawawezi kuchangia vyoo na wanafunzi, fedha hatuzipeleki Dafur (Sudan), tunazipeleka Hai, ndiyo maana nimetoa maelekezo ziende kusaidia walimu wajengewe vyoo ili kuwasaidia wanafunzi na walimu.

“Hayo ndiyo maelekezo niliyotoa kwa kifupi, yamkumbushe mbunge fedha hizo ni za umma na zingerudi serikalini kwa sababu si za mtu binafsi, ninamkumbusha wajibu wake ambao hakuufanya bila maelezo yoyote,” alisema.

Alipoulizwa kuhusu kukiuka maagizo ya Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mwita Waitara aliyoyatoa bungeni Mei 13, mwaka huu, alipotoa onyo kwa wakurugenzi wa halmashauri kutozitumia fedha za mifuko ya jimbo bila idhini ya mbunge kwa sababu hawana uamuzi na fedha hizo, alisema agizo hilo haliingiliani na uamuzi wake.

Alisema waziri alitoa maagizo na onyo kuhusu wakurugenzi kutotumia, hakuzungumzia wabunge wanaopaswa kwenda kusimamia mgawanyo wa fedha hizo kwenye jimbo yao wanaposhindwa kufanya hivyo.

“Kila mbunge amekuwa akienda kuidhinisha fedha na kusimamia mgawanyo kwenye jimbo lake, huyu ni mbunge unique (wa kipekee) ambaye haji, sasa katika mazingira kama hayo tungefanyeje, turudishe fedha?

“Mkurugenzi amekuwa akimwandikia barua huyu bwana, hajibu barua zake, hiyo ni kama kukomoa wananchi. Hilo agizo la waziri linahusu wakurugenzi wanaochukua fedha na kuzitumia katika matumizi mengine. Hizi zimekuja, mbunge hajaja kusimamia ugawaji wake hilo ni suala jingine,” alisema.

MAAGIZO YA WAZIRI

Katika maagizo yake, Waitara alitoa onyo la matumizi ya fedha hizo za jimbo wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Konde (CUF), Khatibu Said Haji katika swali lake ambapo alitaka kujua iwapo kuna baadhi ya wakurugenzi hufanya matumizi ya fedha za mfuko wa jimbo bila kuwashirikisha wabunge hususan Zanzibar, iwapo suala la kusimamia fedha hizi ni la mbunge au wakurugenzi.

Waitara alisema mwenyekiti wa fedha za mfuko wa jimbo, ni mbunge na wajumbe wanajulikana kwa mujibu wa sheria, kanuni na mkurugenzi anapaswa kuheshimu uamuzi wa kamati hiyo ambayo mbunge ndiyo mwenyekiti wake.

Alisema kama mbunge ataridhia fedha hizo kutumika sehemu fulani, mkurugenzi hawezi kuzuia, kama mbunge atakwenda eneo A au B na kusikiliza kero za wananchi na kuahidi kutoa Sh 500,000 mkurugenzi hawezi kubadilisha.

“Wale wakurugenzi wenye tabia ya kutumia fedha za mfuko wa jimbo tunaomba majina yao na ndio maana fedha zikishapitishwa na kamati ya mfuko wa jimbo mkurugenzi hawezi kubadilisha,” alisema Mwita huku wabunge wakishangilia.

Baada ya majibu ya Waitara, Spika wa Bunge, Job Ndugai alitumia fursa hiyo kuwakumbusha wabunge kuzingatia miongozo ya kamati ili isije kufikiriwa ni mbunge pekee pasipo kamati ya fedha kuhusishwa.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Ajira, Kazi na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama alisimama kuzungumzia suala hilo akisema, “Kwa makofi haya ya wabunge kutokana na majibu ya Serikali inaonyesha yako matatizo katika uendeshaji wa fedha hizi”

“Usimamizi wa mfuko wa jimbo, lengo lake ni kuhakikisha wabunge wanachochea maendeleo katika maeneo yao hivyo tunaomba Serikali mtuachie ili tukashauriane na waziri mwenye dhamana ikiwezekana Serikali itoe tena waraka ili kila halmashauri iweze kusimamia utekelezaji wa mfuko huo na tuwaombe wabunge ambao ni wenyeviti wa fedha hizo matumizi yazingatie sheria,” alisema Waziri Mhagama.

Spika Ndugai akahitimisha kwa kusema, “Hilo litasaidia mkitoa waraka.”

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles