24.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Mbowe ahamasisha wananchi kujiandikishaji kupiga kura uchaguzi Serikali za Mitaa

ELIZABETH HOMBO-DAR ES SALAAM

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimesema hakitasusa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 24, huku kikiwataka Watanzania kujitokeza kwa wingi kujiandikisha katika daftari la wapigakura.

Kimesema pamoja na kwamba walifungwa mikono na miguu kwa miaka minne kwa kutokufanya siasa, lakini watashiriki katika uchaguzi huo na wana uhakika watashinda.

Msimamo huo wa chama hicho kikuu cha upinzani nchini, ulitolewa na Mwenyekiti, Freeman Mbowe wakati akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam.

Pamoja na mambo mengine, Mbowe ambaye pia ni Mbunge wa Hai, alisema hawataruhusu matokeo ya uchaguzi huo kuvurugwa na vyombo vya dola wala watumishi wa Serikali.

“Tulizuiliwa kufanya siasa kwa miaka minne. Kujiandikisha na kupiga kura ni majumuisho ya michakato ya kisiasa iliyoendelea kwa miaka minne, leo unasema Watanzania tupige kura, tumpigie kura nani na yupi ambaye tumeweza kumpambanua na kumtofautisha na wengine,” alisema Mbowe.

Alisema ikulu ya wananchi iko katika ofisi za Serikali za mitaa kwa sababu wanaishi na viongozi wake kila siku, hivyo Watanzania wasichukulie uchaguzi huo kama jambo jepesi.

Mbowe alisema kutokana na siasa zinazoendelea, athari kubwa sio kujiandikisha, bali Watanzania wote wataathirika kwa namna ya viongozi watakaowapata.

Kutokana na hilo, alisema kususia uchaguzi huo sio suluhisho kwani itawaondolea nafasi ya kuwachagua viongozi wanaowataka.

“Sasa wakijaribu kuvuruga au kuchakachua uchaguzi huu tutawatuma wananchi, Serikali itambue kuwa wananchi wana ghadhabu.

“Watanzania waache woga, hatuwezi kuingiza woga tukategemea tutabadilisha nchi, haya ni mapambano ya kisiasa, wacha watumie mbinu zao zote, sisi tutatumia nguvu ya umma kuhakikisha kuwa tunashinda.

“Tunapaswa kuweka kando tofauti zetu, twendeni kwa wingi tukajiandikishe ili tushiriki kwenye uchaguzi huu muhimu. 

“Leo tumeona tutumie siku tatu zilizobaki kuhamasisha watu waende kujiandikisha na washiriki kwenye uchaguzi na wala wasisusie.

“Ni makosa makubwa na aibu kususia. Kwa muda wa siku tatu zilizoongezwa, viongozi wote wa kada zote, wahamasishane watoke kwa wingi kwenda kujiandikisha, hatuna sababu za kususia kwani tutakuwa tumesusia maisha yetu.

 “Tunakwenda kushiriki uchaguzi huu na tutashinda, hatutakuwa waoga na haya ni mapambano ya kisiasa, tutatumia nguvu za umma kuhakikisha tunashinda uchaguzi huu,” alisema Mbowe.

Alisema wako watu ambao wamekuwa wakikishauri chama hicho kuwa kisusie uchaguzi huo, lakini kamwe hawatafanya hivyo.

ACT NA UCHAGUZI

Chama cha ACT Wazalendo, kupitia kwa Mwenyekiti wa Kamati ya Kampeni na Uchaguzi, Joran Bashange kimetoa mapendekezo kwa kuitaka Tamisemi itazame upya mchakato wa uchaguzi huu na kurekebisha mapungufu ili kuwatendea haki wananchi.

“ACT-Wazalendo inalaani kitendo cha kuwatisha na kuwatenza nguvu watumishi wa umma kulazimishwa  kwenda kujiandikisha na tishio la kuchukuliwa hatua za kinidhamu kwa kutojiandikisha kupiga kura. 

“Tunatoa wito kwa Jeshi la Polisi kutekeleza wajibu wake kwa mujibu wa sheria za nchi na liache kujihusisha na ushabiki wa kisiasa unaolivunjia heshima na imani kwa wananchi,” alisema Bashenge katika taarifa ya chama hicho.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles