30.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Mbizo za Mwijage zazua mjadala bungeni

Na RAMADHAN HASSAN-DODOMA

MBIO za aliyewahi kuwa Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage zimewashangaza wengi, huku wabunge wameomba mwongozo kwa Naibu Spika, Dk. Tulia Ackson wakidai kama wangepewa elimu ya majanga kusingekuwa na tukio hilo.

Juzi bungeni kulitokea hali ya sintofahamu mara baada ya king’ora kulia na wabunge kutimua mbio nje ya ukumbi ili kujiokoa, huku Mwijage alionekana kukimbia kwa kasi zaidi ili kujiokoa. 

Wabunge walioomba mwongozo jana mara baada ya kumalizika kwa kipindi cha maswali na majibu ni Mbunge wa Rombo, Joseph Selasini (Chadema) na Mbunge wa Ileje, Janeth Mbene (CCM).

Selasini alidai kwamba juzi kulikuwa na taharuki kwa wabunge hadi kufikia Mwijage kutimua mbio kwa kasi kutokana na king’ora kulia.Mbunge huyo alihoji ni kwanini hawapewi elimu kuhusu majanga.

“Hapa kulikuwa na taharuki kubwa kutokana na sauti iliyosikika ndani ya Bunge, lakini siku za nyuma pia kuna mwenzetu mmoja alikuwa anachaji simu mtafaruku kama huo ukatokea, nimekuwa nikiwaza sisi wabunge hakuna mafunzo yoyote tumepewa.

“Lakini pamoja na hayo watu wenyewe wa Zimamoto walikuwa wamezubaa zubaa tu, walikuwa hawajui cha kufanya, sasa mheshimiwa Naibu Spika ili kuondoa hali hiyo na wengine hatuna mbio kama za mheshimiwa Mwijage (Charles), naomba mwongozo wako.

“Mheshimiwa Naibu Spika, kwanini Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ikishirikiana na Bunge zisiwape mafunzo maalumu wabunge jinsi ya kukabiliana na hali kama hiyo inapotokea tena,” aliuliza Selasini.

Akijibu, Naibu Spika alisema kutokana na jambo hilo inaonesha kwamba mitambo ya Bunge ipo vizuri na inaweza kunusa vizuri.

“Nieleze machache tu waheshimiwa wabunge, yale maeneo tunayoingia wengi tumezoea kuingia kwa kutumia mlango mkubwa, lakini ipo milango iliyoandikwa sehemu ya kutokea katika maeneo mbalimbali humu humu bungeni.

“Kwa hiyo likitokea jambo kama lile japo hatuombei litokee, lakini tutokee milango mengine ya dharura sio lazima wote tuje huku mbele, hata Mwijage alitokea huku mbele, hivyo angalieni pale unapokaa mlango upo wapi,” alisema Dk. Ackson.

Alisema juzi hakukuwa na tatizo kubwa na ndiyo maana vikao vya Bunge siku ya jana vimeendelea.Kutokana na majibu hayo ya Naibu Spika, alisimama Mbunge wa Ileje, Mbene na kuomba mwongozo kuhusu jambo hilo.Mbene alidai kwamba milango ya dharura ya kutokea baadhi ina makufuli, hivyo wabunge hawawezi kutoka nje.

 “Tunashukuru kwa maelekezo ya milango ya kutokea, lakini milango ya kutokea mwisho wa yote ‘ina-convert’ kwa mlango mkubwa kwa sababu hapa pembeni kuna kufuli, upande huu wa kushoto kule huwezi kutoka kwani kuna makufuli, naomba hilo liangaliwe,” alisema.

Akilitolewa ufafanuzi, Naibu Spika alisema milango ya dharura ipo wazi na kuna askari ambao wamekaa na kwamba hata yeye aliitumia kutoka nje.“Hakuna tena milango inayofungwa, ila ukitokea huku inatakiwa uende huko huko, tutumie hayo maeneo,” alisema.

Katika hatua nyingine, Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola aliomba mwongozo kwa Dk. Ackson kuhusu Mbunge wa Rombo, Selasini kuwaita askari wa Jeshi la Zimamoto ni legelege.

 “Maneno ambayo yametolewa na Baba Paroko Joseph Selasin kwamba askari wetu wamezubaa nimeona tusipoweka kumbukumbu inaweza ikatafasiriwa Jeshi la Zimamoto lina askari goigoi.

“Tukio hili baada ya kutokea mimi nilihusika kuwaonesha maeneo ya kutoka, mimi mwenyewe nilikuwa wa mwisho kutoka mpaka waheshimiwa wabunge wengine wakawa wananiuliza mimi siogopi.

“Tukiwa hapo nje, Kamanda wa Zimamoto Mkoa wa Dodoma akiwa na askari walikuwa wakifuatilia kuona tukio hili ni la namna gani. Hii sio lugha sahihi,” alisema Lugola.Akijibu, Dk. Ackson alilishukuru Jeshi la Zimamoto kwa kufika kwa wakati.  

“Hili sikulitolea sana maelezo kutokana na jinsi lilivyowasilishwa, lakini tulishukuru Jeshi la Zimamoto kwani walifika kwa muda mfupi, maana yake kama kungekuwa na changamoto wangechukua hatua za haraka. Tunawashukuru kwa hatua walizochukua,” alisema.

Kuhusu mafunzo kwa wabunge, Lugola alisema kabla ya Bunge lijalo wizara yake kwa kushirikiana na Ofisi ya Bunge watatoa mafunzo.      

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles