31.2 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Mbelgiji afichua Okwi alivyoigomea Simba

NA MWAMVITA MTANDA-KIGALI


KOCHA Mkuu wa Simba, Patrick Aussems amefichua kuwa alifanya jitihada za kumshawishi aliyekuwa mshambuliaji wa timu hiyo, Emmanuel Okwi ili asalie Msimbazi, lakini nyota huyo wa kimataifa wa Uganda aligoma katakata.


Okwi mwenye umri wa miaka 27, ameachana na Simba, baada ya mkataba wake kumalizika msimu msimu uliopita wa Ligi Kuu Tanzania Bara, huku kukiwa na taarifa kuwa anakaribia kujiunga na Fujairah FC inayoshiriki Ligi Kuu ya Falme za Kiarabu (UAE).


Mshambuliaji huyo, amekuwa na mchango mkubwa katika kikosi cha Simba, tangu alipojiunga nayo mwaka 2009, akitokea klabu ya SC Villa ya nyumbani kwako Uganda.


Akiichezea Simba, Okwi amefanikiwa kutwaa mataji matatu ya Ligi Kuu Tanzania Bara huku pia akiiwezesha timu hiyo kutinga robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika katika mashindano yaliyopita.


Katika fainali za mataifa ya Afrika(Afcon)zilizomalizika hivi karibuni na Algeria kutwaa ubingwa, Okwi aliisaidia Uganda kutinga hatua ya 16 bora, huku akifunga mabao mawili.


Akizungumza na MTANZANIA kwa njia ya mtandao, Aussems alisema mshambuliaji huyo ambaye msimu uliopita wa Ligi Kuu alifunga mabao 14, ameacha pengo katika kikosi chake.


“Nilizungumza na Okwi akiwa Misri na timu yake ya Taifa iliyokuwa inashiriki michuano ya mataifa ya Afrika(Afcon), nilimwambia bao nataka kufanya naye kazi.

“Aliniambia anataka kubadilisha mazingira kwani amekaa sana Tanzania na ametumikia timu kubwa za Simba na Yanga hivyo anataka kumaliza muda wake wa soka nchi zingine,”alisema Mbelgiji huyo na kuongeza.

“Pia niliongea na mabosi wa Simba wamuongeze dau maana nilifikiri labda tatizo lilikuwa fedha lakini bado hakuwa tayari.”

Wakati huo huo, Aussem alizungumzia fununu za mshambuliaji wa kimataifa wa Tanzania na klabu ya Difaa El Jadida ya Morocco, Simon Msuva kuwa yu mbioni kujiunga na Simba kwa kusema hakuwahi kuuomba uongozi wake umsajili, lakini akakiri ni mchezaji mzuri na anatamani kufanya naye kazi.

“Namfahamu Msuva, ni mchezaji mzuri na ningependa kufanya naye kazi Simba,”alisema Aussems.

Katika hatua nyingine, Klabu ya Simba imetangaza ratiba ya michezo minne ya kirafiki ya kikosi chake ambacho kwa sasa kimepiga nchini Afrika Kusini, kwa ajili ya maandalizi ya msimu mpya wa Ligi Kuu na Ligi ya Mabingwa Afrika.


Ratiba hiyo inaonyesha Julai 23, kikosi hicho kitashuka dimbani kujipima na Orbret TVET, Julai 24 itapepetana na Platinum Stars, Julai 27 kitavaana na Township Rollers na kukamilisha kwa mchezo dhidi ya miamba ya Afrika Kusini, timu ya Orlando Pires kwa kumenyana nayo Julai 30.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles