30.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Mbegu mpya ya chai itakavyowanufaisha wakulima Rungwe

Mkufunzi Msimamizi, Tuntufye Magila, akiwaelekeza wakulima kutumia mbegu mpya ya chai kuleta tija katika zao hilo. Picha zote na Eliud NgondoNA ELIUD NGONDO, RUNGWE

WILAYA ya Rungwe imekuwa ikipata zaidi ya Sh bilioni 9.7 kutokana na chai inayouzwa na wakulima.

Lakini kiasi hicho cha mapato kilikuwa kikishuka kwa asilimia 27 kila mwaka kutokana na kukosekana kwa malighafi katika viwanda vya wakulima.

Lakini baada ya kupata mbegu mpya ya zao hilo malighafi imeanza kuongezeka na wananchi wengi wameshaanza kuona manufaa makubwa kutokana na mbegu

hizo kuonyesha uzalishaji wa majani mengi tofauti na ilivyokuwa awali.

Wanasema wamekuwa wakihangaika na mbegu ambayo ilipandwa na mababu zao
miaka ya nyuma, iliyopitwa na wakati huku ikitoa majani kidogo ya chai.

Mmoja wa wakulima hao Tuntufye Magila, anasema baada ya kuambiwa juu ya
mbegu hizo mpya aliamua kununua na kupanda na kuona mafanikio tofauti na awali.

Ambapo chai aliyopanda mwaka 2013 ameshaanza kuvuna mwaka huu. Magila anasema wakulima wanatakiwa kununua mbegu hizo ili kuachana na kilimo ambacho hakina tija.

Mkulima huyo anasema awali walikuwa wakilima zao hilo na kupata mavuno kuanzia miaka mitatu hadi minne tofauti na sasa ambapo kwa miaka miwili wanaanza kuvuna.
“Mbegu mpya ambazo tumeshauriwa na watalamu wetu zimekuwa ni msaada mkubwa kwetu kwani uzalishaji wake unakuwa wa tija tofauti na ilivyokuwa awali,” anasema.

Anasema baada ya mbegu hizo kupelekwa kwenye Umoja wa Wakulima wa Chai
Rungwe (RSTGA), walihamasishwa kuanza kuzitumia lakini matumaini ya wakulima yalikuwa ni kinyume kutokana na kutegemea mbegu za zamani.

“Tulivyoambiwa kuna mbegu mpya ambazo zimeletwa kwenye kikundi tulikuwa na wasiwasi kuwa wamekuja kutuharibia zao letu lakini kumbe ni tofauti. Mbegu ya zamani ilikuwa inakatisha tama kwa sababu ilikuwa ikichukua muda mrefu hadi kuanza kuvunwa tofauti na mbegu ya sasa,” anasema.

Mkulima mwingine Rephson Mwaisupula, toka Kata ya Masukulu, anasema wakulima wamekuwa wakijilaumu kutokuwa na mbegu hizo mpya ambazo zingeweza kuinua kipato chao zaidi ya hapo walipo.
Anasema mbegu za zamani ziliwakatisha tama na wengi waliona kama wanatumikishwa hali ambayo ilisababisha thamani ya zao hilo kushuka na kuonekana halina maana tena.
Mwaisupula anasema kupatiwa mbegu hizo mpya kutoka kwenye umoja wao imekuwa ni hamasa ya wakulima wengine kujiunga katika umoja huo ambao umekuwa ukiwakopesha pembejeo za kilimo na kununua majani ya chai kwa bei elekezi ya serikali.

“Mbegu za zamani zilisababisha hata ubora kupungua kutokana na miche ya zamani kuzeeka na kutotoa majani mengi ambayo yatakuwa na manufaa kwa mkulima.

“Lakini mbegu mpya zimesababisha kupanda kwa thamani ya zao hili, majani yanayovunwa ni mengi na yamekuwa ya kiwango cha juu hadi kuweza kushindanishwa na nchi zingine,” anasema Mwaisupula.

 

Meneja Kilimo wa Kampuni ya Wakulima wa Chai (WATIKO), John Mhagama, anasema mbegu hizo zimefanyiwa utafiti ili wakulima wanufaike na kilimo hicho.

Anasema kumekuwapo na mbegu aina nne ambazo zimefanyiwa utafiti na kubaini kuwa zinaweza kuwa na manufaa kwa wilaya hiyo ya Rungwe ambazo zinafahamika kwa 301/5, 430/63, 303/178 na 381/5.

Mhagama anasema sifa nyingine ya mbegu hizo ni kustahimili ukame, magonjwa na wadudu waharibifu tofauti na mbegu ya zamani iliyokuwa ikishambuliwa sana na magonjwa.

Kulingana na meneja huyo, mbegu ya zamani wakulima walikuwa wakivuna majani kwa hekta moja kilo 1,500 wakati kwa mbegu hizo mpya mkulima anaweza kuvuna majani kwa hekta moja kilo 3,000 hadi 3,500.
“Mbegu ya zamani ilikuwa ukipanda unaanza kuvuna baada ya miaka mitatu hadi minne lakini kwa mbegu hii mpya unaanza kuvuna baada ya mwaka moja na nusu hadi miwili hali ambayo inakuwa na manufaa kwa mkulima kunufaika kwa muda mfupi,” anasema.

Mkurugenzi wa Umoja wa Wakulima wa Chai Rungwe-(RSTGA), Gabriel Lebi, anasema wakulima wa zao hilo wanatakiwa kutumia mbegu mpya zilizofanyiwa utafiti na wataalamu ili kupata mazao bora.

“Tulianza kwa kupanda mbegu mpya katika shamba la chai Kyimbila na kuona matunda baada ya miaka miwili, hivyo wakulima wakaanza kuona tija ya kutumia mbegu hii kwa kupanda katika mashamba yao,” anasema Lebi.

Anasema mbegu mpya hizo zina uzito wa kutosha hivyo ni fursa kwa mkulima kwani majani yake huwa na uzito wa kutosha hata inapopelekwa sokoni inafanya vizuri tofauti na ile ya kwanza.

[email protected]  / [email protected]
0757670059 / 0782338802 & 0652664939.

 

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles