28.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 16, 2024

Contact us: [email protected]

Mbaroni kumuua binti wa kazi kwa kichapo akimtuhumu kuiba sh 50,000

Waandishi wetu – Arusha/Sumbawanga

JESHI la Polisi Mkoa wa Arusha, leo linatarajia kumfikisha mahakamani Mkami Shirima (33), mkazi wa eneo la Ilkiurei jijini hapa kwa tuhuma za kumuua msaidizi wake wa kazi za ndani, Salome Zacharia (17), akidai ameiba Sh 50,000.

Mtuhumiwa huyo anadaiwa kutenda kosa hilo Machi 9 mwaka huu, kwa kumpiga kwa fimbo msichana huyo kisha kumfungia katika chumba kimojawapo katika nyumba yake kwa siku mbili bila kumpa chakula wala maji ya kunywa.

Inadaiwa alipobaini kwamba hali ya msichana huyo imekuwa mbaya, alimpeleka hospitalini.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Jonathan Shanna, jana alisema baada ya mtuhumiwa kukamatwa na kuhojiwa, amekiri kuhusika na tukio hilo.

“Mtuhumiwa alikamatwa na polisi na baada ya kuhojiwa amekiri, upelelezi umekamilika na kesho (leo) atafikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazomkabili,” alisema Kamanda Shanna.

Aidha katika mitandao kumeonekana video inayomwonyesha Salome akichapwa huku mwanamke huyo akisema; ‘baba Sharifa, huyu mimi naenda nae magereza, nisamehe tu mume wangu kwa kitu ninachomfanya, naenda nae Magereza’.

Mama mzazi wa marehemu, Mariam Athanas, akizungumza nje ya chumba cha kuhifadhia maiti katika Hospitali ya Mkoa ya Mount Meru, mara baada ya kupata taarifa za kifo cha mwanae, aliomba Serikali na wadau wengine kumsadia kumsafirisha marehemu hadi Itigi, Singida kwa maziko.

“Naomba wanisaidie kumrudisha mwanangu Singida kwa ajili ya maziko, mimi huku sina ndugu, niko peke yangu tu, nilikuwa na kaka yangu basi.

“Nimeambiwa amefariki kwa kupigwa, bora ningemuuguza, Serikali inisaidie, hata mshahara walikuwa hawampi, nilikuwa nikiagiza wamlete hawataki, jamani inauma mwenzenu inauma, nimebaki na katoto kamoja, Mungu naomba unisaidie jamani ukiwa nilionao mimi,” alisema mama huyo huku akilia.

Awali inadaiwa fedha ambazo mwajiri wake alikuwa akimuuliza zilipo, zilikuwa zimehifadhiwa katika kisanduku – ‘kibubu’.

Akielezea tukio hilo juzi, mtoto wa mtuhumiwa, Sonia Bakari, alisema siku ya Alhamisi iliyopita, mama yake alikuwa anatafuta kisanduku hicho ambapo baada ya kukikosa katika chumba chake, aliwauliza yeye na Salome iwapo wamekichukua.

Alisema baada ya wao kusema hawajakiona, ndipo mama huyo alipoanza kumpiga Salome.

Alisema alilazimika kumwambia mama yake kwamba aache kumchapa kwa kuwa yeye ndiye aliyekichukua kisanduku hicho na kukivunja na kutoa Sh 100,000 na kumpatia Sh 50,000 ili amtumie mama yake aliyekuwa Singida.

Sonia anadai licha ya kumweleza mama yake hivyo ili asiendelee kumwadhibu Salome, bado aliendelea kumchapa mfululizo huku damu zikimchuruzika na kisha kumfungia katika chumba kimojawapo bila kumpatia huduma yoyote.

“Baada ya mama kutokuona kisanduku alituuliza na akasema kilikuwa na Sh milioni moja, mwanzo tulimwambia hatufahamu akasema anatupeleka kituoni na nikamweleza ukweli kuwa nilichukua mimi na kutoa laki moja na nikampa Salome Sh 50,000.

“Tulipigwa sana, mama akampigia baba akaja akaongea naye, akasema tumpeleke kwa wakala ambaye Salome alituma fedha, akatuambia tukae mpaka asubuhi na kulipokucha alituambia tukafanye usafi chumbani kwake, akamfungia dada chumba kingine akaanza kumchapa,” alidai Sonia.

Inadaiwa Jumamosi wifi ya mama huyo (jina limehifadhiwa) alimweleza mama huyo kwamba Salome alikuwa akitapika damu, ndipo aliamua kumpeleka katika Hospitali ya Mount Meru na alifikwa na mauti Machi 9, mwaka huu.

 Balozi wa Mtaa wa Ilkiurei, Japhet Manangwa, alidai kusikia taarifa za tukio hilo na akalazimika kutoa taarifa kwa Mwenyekiti wa Mtaa kwa ufuatiliaji.

“Sikuwepo na tulipopata taarifa hizo kwa kweli tunasikitika kwani haijawahi kutokea eneo hili na kwa mujibu wa majirani, wanadai walisikia kelele ila geti lilikuwa limefungwa wakashindwa kuruka ukuta, hadi walipokuja kusikia taarifa za kifo cha binti huyo,” alisema Manangwa.

SERIKALI KUSIMAMIA MAZISHI

Katika hatua nyingine, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo, ameongoza mamia ya wananchi katika kuuaga mwili wa marehemu kwa safari kuelekea Itigi mkoani Singida kwa maziko.

Akizungumza na waombolezaji, Gambo alisema alikuwa katika ziara wilayani Ngorongoro, ila amelazimika kuikatiza ili kuungana na waombolezaji akiwemo mama wa marehemu.

Alisema Serikali imesikitishwa na tukio hilo na kuwa kutokana na maombi ya mama mzazi wa marehemu, inatoa Sh milioni moja kwa familia hiyo, gari kwa kusafirisha mwili na jeneza.

“Mara baada ya kupata taarifa za tukio hili, nimelazimika kukatisha ziara kuja kuungana na familia kutokana na mtihani mkubwa walioupata, Serikali imesikitishwa sana na kitendo hiki na tunasubiri hatua zaidi katika vyombo vya sheria.

“Serikali itasaidia gharama za jeneza, hivyo ile 80,000 mliyokuwa mmeitoa awali ambapo mnadaiwa kiasi kingine, mrudishiwe na gharama za hospitali Sh 45,000 watu wa hospitali wawe na utu wakati mwingine, wawarudishie, wakiihitaji waje kwangu nitawapa, nakuagiza Katibu Tawala wa Mkoa Richard Kwitega simamia Sh milioni moja kwa ajili ya rambirambi kwa familia,” alisema Gambo.

Akitoa neno la shukrani kwa Serikali, mama wa marehemu aliishukuru kwa kumsaidia kumsafirisha mwanae na kuomba hatua zichukuliwe kwa aliyehusika na kitendo hicho.

“Naomba Serikali ishughulike kwa kitendo kilichotendeka kwani pengo aliloniachia mwanangu ni kubwa sana, nilidhani atanisaidia kwani wakati mwingine nikiumwa alikuwa akiniuliza na kunisaidia matibabu,” alisema mama huyo.

MAMA ACHINJWA, MTOTO ANYONGWA

Wakati huo huo, mwanamke aliyefahamika kwa jina la Vaileth Mafunda (21) mkazi wa Mtaa wa Vuta, Kijiji cha Kizwite, Manispaa ya Sumbawanga, ameuawa kwa kuchinjwa na huku mtoto wake mwenye mwaka na nusu akinyongwa, na maiti zao kutupwa nje ya nyumba ya mjomba wake.

Akizungumzia tukio hilo, mjumbe wa Serikali ya Mtaa wa Vuta, Milton Boniface, alisema tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia juzi ambapo watu wasiojulikana walidaiwa kufanya mauaji hayo.

Boniface alisema asubuhi ya siku hiyo walipata taarifa kutoka kwa majirani kuwa kuna mwanamke kauawa kwa kuchinjwa akiwa na mtoto wake mgongoni ambaye anadhaniwa kuwa naye alinyongwa katika tukio hilo la mauaji.

Alisema baada ya taarifa hizo, walifika eneo la tukio na kukuta maiti ya mwanamke ikiwa imechinjwa na huku akiwa amevuliwa sketi na nguo za ndani, huku akiwa amebeba mtoto mgongoni ambaye naye alikuwa amefariki dunia.

Walipoukagua mwili huo walibaini kuwa ni wa Vaileth ambaye ni mkazi wa mtaa huo na kisha kutoa taarifa polisi ambao walifika na kuchukua miili hiyo kuifanyia uchunguzi.

Mjomba wa marehemu, Kefas Lemizio, alisema walipoamka asubuhi waligongewa na jirani yao na kuambiwa nyuma ya nyumba yake kuna maiti ya mpwa wake.

Mwandishi wa habari hizi alimtafuta kwa njia ya simu Kamanda wa Polisi mkoani Rukwa, Justin Masejo, ambaye alisema yupo kwenye kikao.

Habari hii imeandaliwa na JANETH MUSHI (ARUSHA) NA GURIAN ADOLF (SUMBAWANGA)

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles