24.5 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

May aungwa mkono na mawaziri kujitoa EU

LONDON, UINGEREZA



WAZIRI Mkuu Theresa May ameungwa mkono na baraza lake la mawaziri kuhusiana na rasimu ya makubaliano kati ya Serikali yake na Umoja wa Ulaya (EU) juu ya masharti ya kujiondoa ndani ya umoja huo ifikapo Machi mwakani.

Kwa mujibu wa vyanzo vya habari, mazungumzo yalichukua zaidi ya saa tano, ambayo May ameyaelezea kuwa ‘marefu, yaliyogusa undani wa mambo na yenye mjadala wa wazi’.

Katika taarifa fupi aliyoisoma kwa vyombo vya habari baada ya kukubaliana na mawaziri wake, May alisema ana imani thabiti kwamba rasimu ya makubaliano ya kuondoka katika Umoja wa Ulaya ndio mwafaka bora ambao ungeweza kufikiwa baina ya Uingereza na umoja huo.

Kizingiti kikubwa katika majadiliano juu ya mchakato wa Uingereza kupeana talaka na Umoja wa Ulaya, maarufu kama Brexit, kilikuwa juu ya mpaka kati ya Jamhuri ya Ireland inayoendelea kuwa mwanachama wa Umoja wa Ulaya na Ireland ya Kaskazini, sehemu ndogo iliyo kaskazini mwa kisiwa cha Ireland, ambayo ni himaya ya Uingereza.

Upo wasiwasi kwamba kurejeshwa kwa mpaka baina ya sehemu hizo kunaweza kurudisha hisia za utaifa zinazoambatana na ghasia.

Rasimu hii ya makubaliano kuhusu Brexit inaruhusu kipindi cha mpito cha miezi 21 kitakachoanza baada ya Uingereza kuondoka rasmi katika Umoja wa Ulaya na kipengele cha kuibakisha  Uingereza nzima katika muungano wa forodha wa umoja huo hadi pale mpango wa kudumu wa biashara baina ya pande hizo utakapopatikana.

Waziri Mkuu May alisema anaamini kwa akili na moyo wake, kwamba uamuzi ulio katika rasimu hiyo ya makubaliano unatilia maanani masilahi ya taifa la Uingereza.

Kufuatia maendeleo hayo nchini Uingereza, Rais wa Kamisheni ya Ulaya, Jean Claude Juncker aliziandikia barua nchi 27 zinazobaki ndani ya Umoja wa Ulaya akiziomba kuunga mkono makubaliano ambayo aliyaita ‘hatua muhimu’.

Kiongozi wa mazungumzo ya Brexit wa upande wa Umoja wa Ulaya, Michel Barnier alisema makubaliano yaliyopatikana kuhusu mpaka wa Ireland ni tofauti na wazo lake la awali, lililonuia kuichukulia Ireland Kaskazini tofauti na sehemu nyingine za Uingereza, ambalo lakini lilikataliwa katakata na Serikali ya London.

Pamoja na yote hayo yaliyofikiwa, bado May anakabiliwa na kibarua kigumu kuweza kuileta pamoja nchi yake kukubali makubaliano hayo na Umoja wa Ulaya.

Chama cha Democratic Union (DUP) cha Ireland ya Kaskazini chenye wabunge 10 wanaomuunga mkono May, kimesema makubaliano yaliyofikiwa hayaridhishi, na kwamba ni yale yale ambayo hapo awali mwanamama huyo alisema asingeyakubali. Waziri Kiongozi wa Scotland – sehemu nyingine yenye mamlaka ya ndani nchini Uingereza, Nicola Sturgeon, alizungumza kwa simu na Waziri Mkuu May, na kulalamika kwamba makubaliano hayo hayatilii maanani masilahi ya Scotland.

Kiongozi wa chama kikuu cha upinzani cha Labour, Jeremy Corbyn pia ameiponda rasimu hiyo ya makubaliano kuhusu Brexit, akisema haina tija kwa sababu hayazingatii mahitaji ya maeneo yote ya nchi.

Hata hivyo, upinzani mkali zaidi unaomkabili May unatoka ndani ya chama chake cha Conservative.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Heiko Maas amekaribisha hatua iliyofikiwa, na kuongeza kwamba nchi yake inasikitishwa na kuondoka kwa Uingereza ndani ya Umoja wa Ulaya.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles