24.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Mawazo humuweka hatarini zaidi mwanamke kupata ugonjwa wa moyo

AVELINE KITOMARY 

MSONGO wa mawazo umekuwa ukiwaathiri watu wengi duniani. Suala hili linaweza kusababisha athari mbaya kwa mhusika kama kumkosesha usingizi, kuvuruga mfumo wa chakula, maumivu ya kichwa, kupunguza kinga za mwili, kuathiri moyo na mengineyo. 

Wakati mtu anapokuwa na msongo wa mawazo, kiwango cha uzalishaji wa homoni za cortisol katika mwili huongezeka, na hivyo kuweza kubadilisha mfumo wa kinga. 

Inaweza kuzuia uzalishaji mzuri wa homaoni za ‘prostaglandin’ unaohusika katika kusaidia kinga ya mwili. 

Msongo wa mawazo huwa unaathiri vibaya kinga hivyo, kumuweka mtu kwenye hatari kubwa ya maambukizi ya corona. 

Sio corona tu, bali hata magonjwa mengine ikiwamo ya moyo kwa sababu unapokabiliwa na hali hiyo, mwili hutoa homoni inayoweza kuharibu misuli ya moyo. 

Matokeo yake kiwango cha mapigo ya moyo huongezeka na kuzuia mishipa ya damu na hivyo kusababisha shinikizo la damu. 

Wakati hali hiyo inapotokea mara kwa mara, shinikizo la damu linaweza kuongeza nafasi ya kuwa na mashambulizi ya moyo au kiharusi. 

Watu wengi wana tabia ya kupunguza msongo wa mawazo kwa kunywa pombe kwa kiasi kikubwa, kuvuta sigara, tabia zote hizi sio tu hudhuru afya ya moyo bali pia hufanya hali ya mhusika kuwa mbaya zaidi. 

UTAFITI MAGONJWA YA MOYO 

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), magonjwa ya moyo husababisha takribani vifo vya watu milioni 18 kila mwaka, idadi hiyo ni sawa na asilimia 31. 

Kulingana na Shirika hilo, asilimia 75 ya vifo vinavyotokana na magonjwa ya moyo hutokea barani Afrika na kwamba idadi kubwa ya vifo hutokea huko Latin Amerika na sehemu za Bara la Asia. 

Hapa nchini, takwimu zilizotiolewa mwaka 2019 na Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsi Wazee na Watoto, zinabainisha kuwapo kwa ongezeko la asilia tatu ya magonjwa ya moyo nchini. 

Kwa mujibu wa utafiti mpya uliyofanywa nchini Uingereza, wanawake wanastahili kupewa ushauri sawa na wanaume, pia kushauriwa kujiepusha na mazingira yanayosababisha magonjwa ya moyo. 

Watafiti wanatoa wito kwa madaktari kusaidia harakati ya kuwatambua wanawake walio katika hatari ya kupata mshtuko wa moyo. 

Utafiti uliofanywa na watafiti wa Chuo Kikuu cha Oxford, ulijumuisha karibu watu 500,000 walio na miaka kati ya 40 hadi 69, ambao wameorodheshwa katika data ya afya ya Uingereza. 

Watafiti walibaini kuwa watu 5,081 waliofanyiwa uchunguzi walikabiliwa na mshtuko wa moyo zaidi ya miaka saba na wengi wao ni wanawake. 

Utafiti huo pia ulibainisha kuwa wanawake wanaovuta sigara wako katika hatari ya kupata mshtuko wa moyo kuliko wale wasiovuta sigara. 

Dk. Elizabeth Millett, Mtafiti Mkuu wa Taasisi ya Kimataifa ya Afya kutoka Chuo Kikuu cha Oxford, anasema ugonjwa wa moyo pia unawaathiri wanawake na kwamba hilo linastahili kutiliwa maanani. 

“Wanawake wanatakiwa kujua kuwa wapo hatarini, lakini licha ya kampeni nyingi kuhusiana na ugonjwa huo bado baadhi yao hawajalitilia maanani. 

Anaongeza kuwa siku zijazo idadi ya wanawake wanaofariki kutokana na ugonjwa wa moyo itakuwa sawa na ya wanaume. 

Kuna magonjwa kadhaa ambayo hayo yanawasibu zaidi wanawake kama saratani ya matiti na mfuko wa uzazi. 

Lakini pia ugonjwa wa moyo umekuwa ukihatarisha zaidi maisha yao. Tafiti zinaonesha kuwa mabadiliko ya mapigo ya moyo ni ya hatari kwa wanawake zaidi kuliko wanaume, hii ni kwa mujibu wa tafiti 30 zilizohusisha zaidi ya wagonjwa milioni nne. 

Kwa mujibu wa utafiti huo, wanawake wenye mapigo ya moyo yanayobadilika badilika (AF) walikuwa na uwezekano wa kufariki dunia kutokana na maradhi ya moyo ama kiharusi mara mbili zaidi. 

Wanawake mara nyingi hawaponi vizuri kwa dawa za kudhibiti mabadiliko ya mapigo ya moyo ama hupatikana na maradhi ya moyo baadae kuliko wanaume. 

Daktari Bingwa wa Magonjwa ya moyo kutoka Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Dk. Honoratha Maucky, anasema tatizo linalomfanya mwanamke kuwa hatarini zaidi kupata magonjwa ya moyo ni msongo wa mawazo. 

“Tafiti zinaonesha kuwa wanawake wengi wanaishi katika mazingira ya msongo ikilinganishwa na wanaume, mbaya zaidi ni kwamba wanaonesha mihemko yao, tafiti zinaonesha kwamba jinsia hizo mbili wakiwa na msongo wa mawazo wenye uwiano sawa, mwanamke hupata matatizo ya moyo zaidi kuliko ilivyo kwa mwanamume. 

“Ni wakati wetu sasa kuamka kuangalia haya mambo yote kwa pamoja, ili tuweze kuona je, ni namna gani tunaweza kupunguza hatari ya magonjwa ya moyo tuweze kuondokana na tatizo hili ambalo ni janga kwa wanawake,” anaeleza Dk. Maucky. 

Kwa mijibu wa Dk Maucky, msongo wa mawazo unaweza kuepukika endapo mtu ataamua kujitoa katika mazingira yanayomsababishia hali hiyo. 

“Tunatakiwa tujifunze leo, ni kweli huwezi kuepuka ‘stress’ ni kitu ambacho kipo nje ya uwezo wa kila mmoja wetu, unapoingia kwenye hali kama hiyo unatakiwa kutazama zaidi namna ya kuondokana na hiyo hali kwani ukidumu nayo muda mrefu kuna uwezekano wa kupata matatizo ya moyo. 

“Unapokuwa katika hali hiyo, tafuta haraka njia ya kuondokana nayo, unaweza ukabadilisha mazingira, ukatafuta marafiki au hata kumwona mwanasaikolojia ukaamua kumshirikisha ili kukusaidia kuondokana nayo. 

Anasema kwa tafiti zilizofanyika, hakuna sababu yoyote inayowafanya wanawake kuwa na msongo wa mawazo, ila inaonesha kwamba mwanamke akiwa katika hali hiyo huwa hatarini zaidi kupata magonjwa ya moyo kuliko wanaume. 

“Mfano ugonjwa wa moyo unaoitwa ‘Takotsubo cardiomyopathy’ huwapata zaidi wanawake pindi wanapokuwa na msongo wa mawazo unaodumu kwa muda mrefu. 

“Hutokea pale ambapo moyo wa mwanamke hasa palipochongoka (apecks) pakiongezeka upana,” anasema. 

Anasema kuwa yapo mambo ambayo bado hayajajulikana lakini yanachangia maradhi hayo, licha ya kwamba kimaumbile hakuna tofauti kati ya moyo wa mwanamke au mwanamume, wanadamu wote ukubwa wa moyo hulingana na ngumi yake. 

Kwa mujibu wa mtandao wa huduma ya kitaifa ya afya nchini Uingereza, mtu anapaswa kutafuta ushauri wa kimatibabu iwapo atahisi dalili za mshtuko wa moyo. 

Dalili hizo ni kama kuumwa na kifua hasa sehemu ya katika, kujihisi kubanwa kifua hadi unashindwa kupumua vizuri, kuumwa na viungo vya mwili au kuhisi kama uchungu unatoka kifuani kuelekea upande wa mkono wa kushoto. 

Dalili zingine ni kutokwa na jasho, kuishiwa pumzi, kujihisi mgonjwa, kuwa na wasiwasi kupita kiasi na kukohoa. 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles