27.5 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

MAWAZIRI WANNE, SPIKA NA WABUNGE WATIFUANA

MAZUNGUMZO: Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Paramagamba Kabudi (kushoto) na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu), Jenista Mhagama (kulia), wakijadili jambo na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Dk. Adelardus Kilagi, bungeni Dodoma jana. | Picha na John Dande

Maregesi Paul na Ramadhani Hassan – Dodoma


BAJETI ya Wizara ya Maliasili na Utalii, imepitishwa huku kukitokea msuguano mkali kati ya Spika wa Bunge, Job Ndugai, wabunge na mawaziri wanne waliokuwa wanajibu hoja zilizotolewa.

Dalili za ugumu wa upitaji wa bajeti hiyo zilianza kuonekana wakati wa kikao cha asubuhi wabunge walipokuwa wakali juu ya utekelezaji mradi wa kufua umeme wa Stiegler’s Gorge na athari za mazingira zinazoweza kutokea katika Pori la Akiba la Selous, huku Spika Ndugai alionekana kuungana nao.

Pia kiongozi huyo wa Bunge, alionekana kuungana na wabunge juu ya udhaifu ulio kwenye kuweka mipaka katika mbuga za wanyama na mapori tengefu.

Hoja nyingine ambazo wabunge waliziibua, ni ukuzaji wa utalii nchini na wananchi kunyang’anywa mifugo na watu wa hifadhi.

Hali hiyo ilikuja kujidhihirisha jioni wakati Bunge lilipokaa kama kamati kujadili bajeti ya wizara hiyo inayosimamia sekta ya utalii, ikikadiriwa kuchangia asilimia 17.2 ya pato la taifa na asilimia 25 ya fedha za kigeni.

Katika hali hiyo, mawaziri wanne ilibidi wasimame kuinusuru, ambao ni Dk. Hamisi Kigwangalla (Maliasili na Utalii), Dk. Merdad Kalemani (Nishati), Mhandisi Isack Kamwelwa (Maji na Umwagiliaji) na Kangi Lugola (Ofisi ya Makamu wa Rais – Mazingira).

MTIFUANO ULIVYOANZA

Hali hiyo ilitokea baada ya Mbunge wa Ulanga, Goodluck Mlinga (CCM), kutishia kushika shilingi ya Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Kigwangalla kama Serikali itashindwa kumpa majibu ya madhara ya watu watakaopitiwa na mradi wa huo.

“Mheshimiwa Spika, nilikuwa naomba ‘commiment’ ya Serikali kwani mradi utakaotekelezwa utakuwa katika zaidi ya hekta 85,000.

“Kwahiyo, nilikuwa naomba Serikali ‘iji-commit’ kwa wale watakaopisha mradi wawe kipaumbele katika mradi huo ambao utatokana na Bonde la Mto Rufiji,” alisema Mlinga.

Akilitolea ufafanuzi suala hilo, Dk. Kigwangalla alisema. “Kwanza ni ngumu sana kuja kubaini kwamba hawa ndio wanakuja kunufaika na programu ya umwagiliaji katika hatua hii ya sasa.

“Lakini pia ni ngumu kwani kuna wananchi ambao watatolewa kupisha mradi wa Stiegler’s Gorge kwa sababu hilo halipo, kwani mradi utatekelezwa katika pori la akiba na hautekelezwi Wilaya za Malinyi, Kilombero.

“Lakini pia, tunachora mipaka upya kwa Kilombero Game Control Area, tumeachia eneo kubwa sana kwenye vijiji, kwa sababu mwanzoni ilikuwa na ukubwa kilomita 7,500 na leo hii tumepunguza mpaka 2,500.

“Tunatengeneza miradi ya skimu za umwagiliaji ili kutumia maji hayo ili Mto Kirombero usiharibike.”

Pamoja na majibu hayo, Mlinga hakuridhika na kuomba kwa Spika Ndugai kutoa hoja ili wabunge waijadili.

“Mheshimiwa Spika, hivi ninavyoongea, jimboni hakukaliki na sio Ulanga tu, Malinyi, Kilombero na Mlimba pia. Sasa naona mheshimiwa waziri anachukulia kama masihara, nomba wabunge wenzangu mniunge mkono tujadili suala hili,” alisema Mlinga na kuungwa mkono na wabunge wenzake.

Pamoja na kutoa hoja hiyo, Spika Ndugai alidai mbunge huyo hakusema kitu chochote kuhusu nia yake hiyo.

Baada ya kuona suala hilo linawagusa wabunge wengi, Spika Ndugai alitaka Wizara ya Nishati nayo ilizungumzie.

“Mheshimiwa Waziri wa Nishati, kwenye hii hoja ambayo inasemwa miti sijui milioni ngapi itakatwa, Stiegler’s Gorge na athari ambazo zitatokea, Tanesco hawajihusishi na miradi ya mazingira, lazima waanze kujihusisha na utunzaji wa mazingira.

“Yaani, badala ya Tanesco kujishughulisha na umeme pekee, lazima wajue wanawajibika kwa kiasi fulani katika mazingira,” alisema Spika.

Hoja hiyo ilimwibua Dk. Kalemani aliyesema kuna mambo mawili ya kufanya katika mradi huo.

“Ni sahihi mheshimiwa mbunge, lile bwawa ambalo litajengwa litaweza kuhifadhi maji za hekta za umwagiliaji zaidi ya 250,000 na maji hayo yatasaidia.

“Mradi haujaanza kutekelezwa, taratibu zitazingatiwa, sio kwamba mradi utaanza tu, na hadi saa hakuna mti hata mmoja uliokatwa,” alisema Dk. Kalemani.

Baada ya hatua hiyo, Spika alimruhusu Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Kamwelwe ambaye alisema skimu ya umwagiliaji itakapokamilika, watu watakaopewa nafasi ya kwanza ni wale wanaoishi katika maeneo hayo.

Kwa upande wake, Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT Wazalendo), alisimama na kuomba taarifa akidai miradi ya umwagiliaji haiisaidii nchi.

“Mwenyekiti, nilikuwa nataka tunapojadili mambo ya kitaifa, tuwe wakweli kwa saababu tuna mifano ambayo tayari tumeishaiona kwa Mkoa wa Dodoma ambapo Mtera wana bwawa, lakini hakuna umwagiliaji, Kidatu wana bwawa, lakini hakuna umwagiliaji na Kihansi wana bwawa, lakini hakuna umwagiliaji.

“Mimi nadhani hoja ya msingi ni hii ambayo Mwenyekiti umeileta, kwamba kuna ukataji wa miti shirika ambalo linanufaika na mradi lazima lije na hoja.

“Hayo ndiyo maelekezo yachukuliwe na Serikali, siyo blabla zinazoletwa hapa,” alisema Zitto.

Akilitolea ufafanuzi hilo, Dk. Kalemani alisema kila mradi una ‘dizaini’ yake na mradi wa Stiegler’s Gorge ni wa kisasa.

“Ethiopia ambayo ina jumla ya megawati 4,822 inatekeleza mradi mwingine mkubwa zaidi ya megawati 6,450 lakini kwa ‘dizaini’ ya mradi huu ni tofauti kabisa.

“Mheshimiwa Mwenyekiti, Mtera kuna hifadhi kama ya Selous kwa vyovyote lazima ‘dizaini’ zitofautiane, hivyo baianuai haiwezi kuathirika,” alisema.

Kutokana na maelezo hayo ya Dk. Kalemani, Spika Ndugai alisema waziri huyo hajawaelewa hata kidogo.

“Mheshimiwa Waziri yaani hujatuelewa kabisa, yaani suala letu ni dogo sana. Katika mambo ya mazingira kuna hiyo miti ambayo itakatwa, hilo ni lazima lifanyike wala hatulaumu.

“Bwana Tanesco anatakiwa kuwa pia na mawazo ya mazingira baadae huko,” alisema Spika huku akishangiliwa na wabunge.

Kutokana na maelezo hayo, Dk. Kalemani aliomba nafasi ya kutaka kulifafanua hilo lakini Spika alimkatalia.

Akilitolea ufafanuzi hilo, Kigwangalla alisema: “Tunakubaliana na mapendekezo yako na ndiyo mapendekezo ya wizara yetu, sisi tumepeleka mapendekezo katika kamati ambapo tunataka tutumie kanuni ya PPP ili itengenezwe tozo kwa ajili ya jambo hilo.

“La pili, katika uvunaji wa miti kuna matarajio ya kuuza miti hiyo kibiashara, tunaivuna, katika uvunaji kuna mauzo yatafanyika na mauzo yake yana thamani ya kati ya Sh bilioni 400 mpaka 600, hizi pesa zitatumika katika uhifadhi wa maeneo hayo.

“Hili suala la vigingi, kuna maeneo nimekwenda nikakuta kuna misikiti, nyumba za watu na makanisa vimewekwa vigingi.

“Kwahiyo, niko tayari kumwomba Mheshimiwa Rais akubali kubadilisha sheria ili maeneo hayo yanayoonekana kuwa katika maeneo ya hifadhi, yaruhusiwe kuendelea kuwapo,” alisema Kigwangalla.

Kuhusu mapori ya akiba, alisema baadhi yake yatapandishwa hadhi na barabara zinazoelekea katika maeneo hayo, zitajengwa ili kurahisisha usafiri.

Naye Lugola, alisema lazima mradi huo utatekelezwa na atakayeupinga, atafungwa.

Pamoja na hayo, aliwataka wabunge warejee ripoti ya Profesa Raphael Mwaryosi aliyoitoa na kueleza jinsi mradi huo utakavyotekelezwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles