24.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Mawaziri 11 walioonja shubiri miaka mitatu ya JPM

Na Markus Mpangala


KESHO Rais Dk. John Magufuli, anatimiza miaka mitatu tangu alipoingia madarakani Novemba 5, 2015. Katika kipindi chote hicho amefanya maamuzi katika mashirika ya umma pamoja na nafasi mbalimbali za uteuzi kuanzia ngazi za wilaya, mkoa, kanda, mabalozi na Jamhuri ya Muungano kwa ujumla wake. Aidha, amefanya mabadiliko ya wenyeviti bodi wa mashirika ya umma, baraza la mawaziri na kadhalika.

Eneo ninaloangazia leo ni katika baraza la mawaziri ambalo limekuwa kaa la moto, katika miaka hiyo mitatu mawaziri 11 wameondolewa. Msimamo wa Rais Magufuli ni kuona ufanisi na uchapakazi wa kiwango cha juu kwa kila waziri anayekabidhiwa dhamana. Uchambuzi huu ni sehemu fupi tu ya kuangazia masuala yaliyomo nchini.

Dk. Susan Kolimba, alikuwa kiongozi wa 11 kuondolewa kutoka Baraza la Mawaziri tangu kuingia madarakani. Kolimba alikuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki inayoongozwa na Dk. Augustine Mahiga.

Dk. Kolimba ambaye alishindwa kufahamu sababu za kuondolewa kwake, amekuwa akilalamikiwa na Rais Magufuli kuwa hajamridhisha kwa utendaji wake tangu kuingia madrakani.

Nafasi ya Kolimba ilichukuliwa na Mbunge wa Songea Mjini, Dk. Damas Ndumbaro. Kolimba ni mbunge wa viti maalumu akiwakilisha Mkoa wa Njombe tangu mwaka 2015.

Hata hivyo, wakati akimwondoa Dk Kolimba, Rais Magufuli, hajawahi kutamka hadharani juu ya mambo ambayo yanasababisha kutoridhishwa na mwenendo wa utendaji wa kazi wa wizara hiyo.

Si Kolimba pekee, bali Katibu Mkuu Profesa Adolf Mkenda, naye aliondolewa wizarani hapo na kupelekwa Wizara ya Maliasili na Utalii, huku Rais Magufuli akimwomba kuhakikisha anaongeza mapato ya sekta ya maliasili na utalii ambayo ni miongoni mwa wizara nyeti mno nchini.

Duru za kisiasa na kitaaluma zinaonyesha historia yenye kusisimua baina ya viongozi hawa wawili yaani Dk. Ndumbaro na Dk. Susan Kolimba kutoka Chama Cha Mapinduzi-CCM.

Wote kitaaluma ni wanasheria wanaotokea Kitivo cha Sheria cha Chuo Kikuu Huria katika nafasi ya uhadhiri.

Dk. Kolimba alikuwa Mkuu wa Kitivo cha Sheria cha Chuo Kikuu Huria kabla ya mwaka 2015 kuingia rasmi katika siasa, akigombea na kushinda ubunge kupitia viti maalumu, Mkoa wa Njombe. Mwaka 2016, Dk. Kolimba, aliteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje.

Vivyo hivyo kwa Dk. Ndumbaro, naye ni mwanasheria kitaaluma na Wakili wa Mahakama Kuu. Ndumbaro alikuwa Mhadhiri wa Chuo Kikuu Huria na alirithi ukuu wa Kitivo cha Sheria cha Chuo hicho kutoka kwa Dk. Kolimba.

Dk. Ndumbaro alishiriki na kushinda nafasi ya ubunge wa Jimbo la Songea Mjini kwenye uchaguzi mdogo baada mbunge wa jimbo hilo, Leonidas Gama, kufariki dunia.

Septemba 26 mwaka huu, Rais Magufuli alimteua Dk. Ndumbaro kurithi nafasi ya Dk. Kolimba katika nafasi ya Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Historia hii ingeweza kutumiwa na wataalamu wa falaki na kusema Dk. Ndumbaro na Dk. Kolimba ni ‘marafiki’ ambao wamekuwa wakiachiana au kuwa na tabia ya kurithishana madaraka. Hii ni kulingana na vile walivyopita kuanzia ngazi ya kitaaluma hadi siasa (kuteuliwa kwenye unaibu).

MAWAZIRI 11

 

Kama nilivyomtaja awali Dk. Kolimba, mawaziri na manaibu walioondolewa na kufikisha idadi hiyo ni pamoja na:-

Charles Kitwanga; Mbunge wa Misungwi, ambaye aliondolewa katika nafasi yake ya uwaziri wa mambo ya ndani kwa madai ya ulevi wakati akijibu swali la papo kwa papo bungeni.

Mwigulu Nchemba; Mbunge wa Iramba Mashariki (Singida) tangu mwaka 2010, alirithi nafasi ya Kitwanga. Naye aliondolewa wakati akiwa ziarani mkoani Kigoma huku akiorodheshewa mambo 19 yaliyochangia kung’olewa katika wadhifa wake.

Miongoni mwa mambo hayo ni usajili wa asasi za kiraia, magari 777 ya Jeshi la Polisi, mabadiliko ndani ya jeshi la polisi na Zimamoto, ajali za barabarani na usajili wa asasi zisizo za Serikali. Nafasi yake imechukuliwa na Kangi Lugola.

Profesa Sospetr Muhongo; Mbunge wa Musoma Vijijini (Mara) alikuwa Waziri wa Nishati na Madini. Profesa Muhongo amekumbwa na kashfa mara mbili ndani ya Serikali tofauti. Kuelekea mwishoni mwa uongozi wa awamu ya nne, Profesa Muhongo alilazimika kung’atuka katika nafasi yake kutokana na kashfa ya Escrow. Baada ya kuondolewa nafasi yake imechukuliwa na Angellah Kairuki.

Nape Nnauye; Mbunge wa Mtama (Lindi) tangu mwaka 2015, alikuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo. Nafasi yake imechukuliwa na Dk. Harrison Mwakyembe ambaye alibadilishwa wizara kutoka ile ya Katiba na Sheria.

Profesa Jumanne Maghembe; Mbunge wa Mwanga (Kilimanjaro) tangu mwaka 2000. Aliondolewa katika nafasi ya Waziri wa Maliasili na Utalii. Kabla ya kushika wadhifa huo alikuwa Waziri wa Maji na Umwagiliaji. Nafasi yake imechukuliwa na Dk. Hamis Kigwangalla.

George Simbachawene; Mbunge wa Kibakwe (Dodoma) tangu mwaka 2005. Aliondolewa katika nafasi ya Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) na nafasi yake kuchukuliwa na Seleman Jafo.

George Lwenge; Ni Mbunge wa Njombe tangu mwaka 2010. Aliondolewa katika nafasi ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji. Nafasi yake imechukuliwa na Profesa Makame Mbarawa.

Anastazia Wambura; Mbunge wa Viti Maalumu-CCM tangu mwaka 2005. Aliondolewa katika nafasi ya Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo. Nafasi yake imechukuliwa na Juliana Shonza.

Ramo Makani; Mbunge wa Tunduru (Ruvuma) tangu mwaka 2010. Aliondolewa katika nafasi ya Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii alikuwa chini ya Profesa Maghembe.

Dk. Abdallah Possi; Mbunge wa kuteuliwa na Rais. Aliondolewa katika nafasi ya Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu. Baadaye aliteuliwa kuwa balozi.

Uongozi wa Rais Magufuli umejenga taswira tofauti na ule wa Rais Mstaafu Jakaya Kikwete, pamoja na wengine waliopita. Kwamba Kikwete alikuwa kiongozi anayetumia diplomasia zaidi kuelezea sababu za kuwaondoa baadhi ya mawaziri ama kutumia mbinu ya kimya kimya hata pale walipokabiliwa na shinikizo kutoka vyama vya upinzani.

Kwa upande wake Rais Mafuguli amewaondoa mawaziri huku akilalamika sababu mbalimbali za wazi kabisa (hata kama hayasemwi yote).

Aidha, sifa ya uongozi wa awamu ya tano ni kwamba, umeondoa ile dhana ya Serikali kufanya mabadiliko ya uongozi hadi pale kunapoibuka kashfa fulani inayolazimisha baraza la mawaziri kupanguliwa au kufanya mabadiliko madogo na makubwa pale kunapoibuka shinikizo la kisiasa. Rais Magufuli ameondoa kasumba hiyo kwa kufanya mabadiliko haraka iwezekanavyo.

Swali moja pekee kwa sasa, mabadiliko hayo yataleta tija gani kwa wananchi wa Tanzania?

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles