MAWAKALA WA PEMBEJEO WAONYWA

0
624

Na AHMED MAKONGO -BUNDA

HALMASHAURI ya Wilaya ya Bunda, imewaonya mawakala wanaosambaza pembejeo za kilimo kutofanya hujuma ya aina yoyote   msimu huu wa kilimo, hususan mbegu za mazao mbalimbali.

Onyo hilo lilitolewa  na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda, Isack Mahela, wakati wa majumuisho ya kikao cha wadau Jukwaa la Mnyororo wa Thamani wa zao la mpunga kilichofanyika mjini Bunda.

Mahela alisema   baadhi ya mawakala wanaosambaza pembejeo siyo waaminifu na hivyo kuwaonya kutokuthubutu kufanya hujuma yoyote kwa kuwa Serikali ipo makini kufuatilia.

Alisema katika musimu uliopita baadhi ya mawakala walichakachuwa pembejeo za wakulima na kutokuzifikisha kwa walengwa huku wakidai kuwa wamezisambaza kwa ufasaha hali ambayo ilikwamisha uzalishaji wenye tija.

“Katika halmashauri yangu sitaki kuona jambo hili linatokea na niwaombe maofisa wote wanasosimamia kuhakikisha mchezo huo mchafu unaowaumiza wakulima hautokei na ukutokea wanaohusika wawajibishwe mara moja,” alisema.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Macc Group Ltd, Sunga Kusekwa alisema lengo la jukwaa hilo ni kuendeleza zao la mpunga ambapo mradi huo ukimaliza muda wake wakulima hunufaika zaidi.

Meneja wa mradi huo katika Wilaya ya Bunda, Johanes Bucha, alisema wakati wanaandika andiko la mradi huo, uzalishaji wa   mpunga katika wilaya hiyo ulikuwa juu wakati sasa hali inaonyesha kushuka.

Alisema jitihada zaidi zinahitajika na wakulima wafuate ushauri wa wataalamu wa kilimo.

Baadhi ya wakulima wa zao hilo walisema kilimo hicho lazima kiwe endelevu na ni aibu kwa wilaya ya Bunda yenye fursa nyingi kuomba chakula cha msaada.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here