27.9 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Mauaji ya watoto Njombe yatikisa Bunge

>>Mbunge aeleza wafanyabishara wakubwa walivyotiwa  mbaroni

RAMADHAN HASSAN Na ELIZABETH KILINDI-Dodoma/Njombe

MATUKIO ya mauaji ya watoto mkoani Njombe, yametua bungeni huku Mbunge wa Lupembe, Joram Hongoli (CCM), akitoa hoja bungeni akiwataka wabunge wajadili suala hilo kwa dakika 20.

Hatua hiyo ilikuwa baada ya mbunge Hongoli, kuomba mwongozo jana baada ya kumalizika kwa kipindi cha maswali na majibu.

Akitoa  hoja aliwaomba wabunge wajadili kwa dakika 20  kuhusiana na mauaji yanayoendelea   mkoani Njombe.

“Mheshimiwa Spika, Mkoa wa Njombe kuanza mwanzoni mwa mwaka huu Januari, Halmashauri ya Wilaya ya Njombe na Halmashauri ya Mji wa Njombe watoto watatu walishauawa na baada ya hapo wameshahamia Halmashauri yangu ya Njombe DC kwa maana ya Jimbo la Lupembe.

“Mpaka ninavyoongea hivi watoto wanne tayari wameshauawa, watoto watatu kutoka kwenye familia moja na mtoto mmoja katika Kijiji cha Matembwe aliuawa   Ijumaa na kuzikwa Jumamosi.

“Mheshimiwa Spika, pamoja na mauaji hayo lakini pia kuna taharuki kubwa   na watu wamekuwa na hasira   kwa sababu   hivi sasa shughuli zote za  uchumi katika Mkoa wa Njombe hazifanyiki.

“Kina mama kila asubuhi wakiamka wanatakiwa kwenda kuwasindikiza watoto shuleni na mchana kwenda kuwachukua na jioni kwa hiyo mambo yote yamesimama.

“Lakini kama vile haitoshi Mheshimiwa Spika, kutokana na hiyo hasira tayari kuna mauaji yameshajitokeza katika baadhi ya halmashauri.

“Kwa mfano juzi kule Ludewa wameshaua mtu mmoja ambaye anadhani   ni kati ya watu wanaotafuta hao watoto wadogo chini ya miaka 10 lakini kumbe alikuwa si mtu anayeshughulika na shughuli hizo,” alisema katika hoja yake.

Mbunge huyo alidai   kuna watu sasa wamejitokeza ambao ni kama wanaongeza hasira ambao wamekuwa wakituma picha katika mitandao ya  jamii ambako hoja hiyo iliungwa mkono na wabunge wote waliokuwamo ukumbi.

Baada ya hoja hiyo ya mbunge, Spika wa Bunge, Job  Ndugai,  alisema hajawahi kuona hoja iliyoungwa mkono kwa kiasi kikubwa kama hiyo.

“Hoja imetolewa na sijawahi kuona hoja imeungwa mkono kama hii, imeungwa mkono sana lakini kabla sijaamua nimpe dakika mbili Mbunge mmojawapo wa Njombe, nimekuona Mheshimiwa Deo Sanga na leo umepiga suti. Hebu tupe kidogo nini kinaendelea huko,”alisema Ndugai.

Akichangia hoja hiyo, Mbunge huyo wa Makambako, Deo Sanga (CCM), alisema hali katika eneo hilo ni mbaya kwa vile  kuna baadhi ya wafanyabiashara wakubwa wamekamatwa.

“Hali ya Njombe ni tete na imeleta taharuki kubwa na baadhi ya watu kama wageni wakifika katika maeneo mbalimbali inaonekana hao wamekuja kuteka watoto na kuua.

“Na hivi sasa tunavyozungumza, baadhi ya wafanyabiashara wakubwa wamekamatwa katika Mji wa Makambako katika Wilaya ya Njombe.

“Hao wafanyabiashara wakubwa wana siku nne ndani na hivi sasa  hatujui nini kinachoendelea, japo wafanyabiashara wengine walikuwa ni wakazi wa Makambako na walikuwa wako Dar es Salaam na ni wawekezaji wakubwa katika Mji wa Makambako, hivi sasa wamekamatwa,” alisema Sanga

Alisema mpaka sasa wafanyabiashara 10 wamekamatwa kutokana na tukio hilo.

“Na watu waliokamatwa mpaka sasa ni takribani watu 10 ambao ni wafanyabiashara wakubwa, kuna baadhi yao wana viwanda, wana watumishi zaidi ya 200.

“Shughuli sasa zimesimama na baadhi ya watu wengine wamewekeza hapo Njombe pia wafanyabiashara hao wakubwa,” alisema.

Alisema hali ni mbaya hasa kwa wafanyabiashara ambao hufanya biashara ya mbao.

“Ukienda kule Lupembe aliposema Mheshimiwa Hongoli, Mji wa Lupembe katika Wilaya ya Njombe ndiyo unaozalisha mbao kwa wingi, sasa watu wanapokwenda kule kama alivyosema, watu wamekwenda na pikipiki (bodaboda)…

“Walipofika mahali wamesimama watu wakasema, hee, hao hao watu wakakimbia na bahati nzuri wakampigia simu Mheshimiwa mbunge, nikasema msiwaue,” alisema.

Kwa maelezo hayo, Spika Ndugai aliiomba Serikali itoe maelezo kuhusiana na jambo hilo.

Maelekezo hayo ya Spika Ndugai, yalimfanya Mnadhimu Mkuu wa Serikali ambaye pia ni Waziri wa Nje Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Ajira na Wenye Ulamavu,

Jenista Mhagama, kusimama na kuomba serikali ipewe nafasi na katika siku za hivi karibuni itatoa majibu ya kueleweka.

“Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu na serikali, jambo hili kama mlivyolisikia ni jambo ambalo ni zito na linachukua taswira nzito ndani ya taifa na tunadhani kwamba sisi kama serikali ili tuweze kutoa maelezo ya kina, ni bora kiti chako kitupe nafasi…

“Tutayarishe kauli ya serikali na   tuweze kuileta ndani ya Bunge lako haraka, Bunge lako liweze kujua hatua kubwa ambayo serikali tumechukua pia katika jambo hili,” alisema.

Kwa upande wake, Spika Ndugai alikubaliana na ombi la Jenista huku akiitaka itoe majibu kabla ya kumalizika  kikao hicho. 

“Ni kweli jambo hili ni jambo kubwa, linahuzunisha, linasikitisha sana. Nakubaliana na ushauri uliotolewa na upande wa serikali, kabla hatujamaliza Bunge hili, mwisho wa wiki hii tupate maelezo kutoka serikalini ya nini kinachoendelea huko Njombe,” alisema.

POLISI WATOA ONYO

Wakati huohuo, Jeshi la Polisi Mkoa wa Njombe  limetoa onyo kwa baadhi ya wananchi wanaotoa taarifa ambazo siyo sahihi juu ya mauaji ya watoto wadogo mkoni hapa na badala yake wasikilize taarifa kutoka   vyombo husika.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe, Renatha Mzinga, alisema   jambo hilo linakuzwa kutokana na wananchi kuweka katika mitandao ya  jamii taarifa ambazo hazina ukweli.

“Matukio haya yapo hata mikoa mengine lakini tunashangaa Mkoa ya Njombe, kwetu limekuwa kubwa   kwa sababu wananchi wetu wamechukua maneno ya mitaani na kuyaweka kwenye mitandao,’’ alisema Mzinga.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles