23.3 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

Mauaji ya Khashoggi kwa Trump umiza kichwa, fursa kwa Erdogan

Na JOSEPH HIZA

TAIFA la Uturuki ni moja ya yale yanayoshutumiwa kwa rekodi ya ukiukwaji wa haki za binadamu duniani kiasi cha uwapo tishio la kuiwekea vikwazo, mtazamo ambao unaonekana kusahaulika angalau kwa muda kipindi hiki.

Naam, kipindi hiki ambacho dunia iko katika mshtuko unaotokana na sinema mbaya zaidi katika historia ya karibuni kufanywa na tawala za dunia hii ya mauaji ya kikatili ya mwandishi wa habari wa Gazeti la Washington Post la Marekani, Jamal Khashoggi (59).

Mengi yameshaelezwa kuhusu mauaji hayo yaliyotokea Oktoba 2 mwaka huu ndani ya ubalozi mdogo wa Saudia Arabia mjini Istanbul, Uturuki, lakini kwa ufupi, rafiki huyo aliyegeuka mkosoaji mkubwa wa utawala huo chini ya uongozi wa mwana mfalme mrithi wa kiti hicho Mohamed bin Salman.

Khashoggi, raia wa Saudia mwenye asili ya Uturuki, alikuwa ameenda ubalozini humo kupata nyaraka zitakazomsaidia kumuoa mchumba wake raia wa Uturuki, Hatice Cengiz.

Hata hivyo, alipoingia hakutoka tena. Na bahati nzuri alikuwa amejiandaa, akifahamu hatari inayoweza kumkabili akaandaa mazingira yatakazoziwezesha mamlaka za Uturuki kunasa ushahidi dhidi ya Taifa lake.

Akamwachia simu mbili mchumba wake na kumtaka amsubiri na iwapo hatorudi awasiliane na mmoja wa wasaidizi wa Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan.

Kwa sasa Uturuki inamlinda Cengiz mafichoni.

Hivyo, kutoweka kwake kulifahamika kirahisi na kushadidiwa mno na Serikali ya Rais Erdogan iliyojizolea sifa sasa.

Hilo pia limesababisha dunia ipige kelele dhidi ya Saudia na kuitaka Marekani itangulize haki kwa kumuadhibu mshirika wake huyo mkubwa Mashariki ya Kati.

Ni suala linalotishia kuuchafua utawala wa Saudia na hata kukwamisha ndoto ya Mohamed bin Salman maarufu kama MBS kurithi kiti cha ufalme, ndiyo maana juhudi zinafanyika kumsafisha na kumtenga na lawama za mauaji hayo.

Wanadiplomasia nchini Marekani wamekiri kuwa mzozo huu ni mzito, ni moja ya ile mizito zaidi kwa sera za kigeni Mashariki ya Kati katika urais wa Trump.

Marekani ina uchaguzi wa kuchagua manufaa ya kibiashara au kuyakosa kwa kutanguliza heshima ya ubinadamu.

Wakati Ujerumani ikitanguliza maadili na haki za binadamu kwa kutangaza kusitisha mauzo ya silaha kwa Saudi Arabia, Trump amesita.

Kwake ni bora kukosa heshima hizo kutanguliza manufaa ya kibiashara kwa taifa lake. Lingine anaonekana kusita kuiadhibu Saudi Arabia kwa hofu kuwa itakimbilia kwa mahasimu wake wakubwa Urusi au China, jambo ambalo Marekani haitaki litokee asilani.

Hata hivyo, Marekani kwa kuchagua kuweka mbele masilahi yake si tu itapoteza heshima na taswira yake kama mtetezi wa maadili na haki za binadamu bali pia nguvu na ushawishi wake duniani. Hivyo, yanaiumiza kichwa mno!

Na kwa Rais Erdogan ni fursa kubwa si tu kujijenga bali pia kukarabati uhusiano wake na Marekani na Saudia uliodorora na hata kuzibomolea mbali katika taswira chanya ulimwenguni tawala hizo mbili.

Wakati akiwa mgombea urais, Donald Trump kwa mara ya kwanza alipokuja na kauli mbiu yake maarufu ya Marekani kwanza linapokuja suala la sera ya kigeni, alidai taifa hilo chini ya Rais Obama lilipoteza heshima na liligeuka kichekesho duniani kote.

Hivyo katika hotuba yake hiyo ya Aprili 2016, aliapa kuifanya Marekani kuwa na nguvu, kuogopwa na kuheshimiwa zaidi  duniani.

Lakini namna alivyoshughulikia na kuitikia mauaji hayo ya Khashoggi na kauli za kujaribu kumtetea MBS, kunatazamwa na wengi kuwa yu rais dhaifu zaidi kutokea.

Licha ya ushahidi kuashiria wazi uhusika wa MBS, Trump alikuwa akikataa kuchukua uamuzi wa kuwaadhibu Wasaudia.

Badala yake, ingawa kuna wakati amemuonya, amemsifu wazi wazi MBS (33), ambaye ni kiongozi asiyepingika na mrithi wa kiti cha ufalme.

“Ni mtu mwenye nguvu. Ameidhibiti nchi na anaonekana mwenye uwezo wa kuhakikisha vitu vyote viko sawa. Namaanisha kwa njia nzuri

Lakini baadhi ya washauri wake wanamuonya iwapo ataiacha Saudi isalimike na mauaji hayo ya kikatili, Wasaudia hawatomheshimu kama kiongozi mwenye nguvu — wala tawala nyingine za kiimla duniani kama Korea Kaskazini na Iran.

Washauri hao waliongea naye na kumtaka atume ishara ya wazi Mashariki ya Kati kuonesha nguvu ya uwapo wake eneo hilo.”

Ili kupunguza shinikizo nchini mwake na kupata uungwaji mkono wa wafuasi wake, ambao wamejitolea kumsaidia kwa kumtangaza Khashoggi kuwa Muislamu mwenye itikadi kali, Trump ameonesha wazi kuweka mbele uhusiano na uongozi wa Saudia kwa sababu ya manufaa inayopata hasa mauzo ya silaha.

Licha ya kuwahi kuionya Saudia iwapo itabainika kumuua Khashoggi, Trump amekataa mwito wa Bunge la Marekani kuuwekea vikwazo utawala huo wala kusitisha mauzo ya silaha.

“Mnataka waende kununua Urusi au China? Hili halina manufaa kwetu zaidi ya kutuumiza bure,” Trump alikaririwa akiliambia gazeti la The Post baada ya kuulizwa kuhusu msimamo wake huo bungeni.

Lakini wataalamu wa sera za kigeni wanaonya kuwa ni wazi, Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong-un, Rais wa Urusi Vladi­mir Putin na watawala wengine wengi wa kiimla duniani wanamsoma Trump namna anavyoshughulikia filamu ya Khashoggi.

Kwamba si tu watapenda achemshe kwa maana ya kuegemea upande wa wauaji ili kuleta uwiano bali pia kumshukia kuwa hana mamlaka kimaadili ya kuwanyooshea kidole.

Kwamba itakuwa ni unafiki kwa Marekani kuwanyooshea kidole ilhali wakiukaji wengine wa wazi wazi inawatetea.

Lakini wakati viongozi wengine wakimchukulia Trump kama mdhaifu, yeye mwenyewe ana mtazamo tofauti. Anajihesabu mwenye nguvu kwa kulinda uwekezaji wake nchini Saudi Arabia.

Haikushangaza kumsifu sana Kim, anayefahamika kwa ukiukaji wa haki za binadamu duniani.

Kim, mbali ya shutuma nyingi zinazomkabili kuhusu haki za bindamu pia alimuua kaka yake akiwa uwanja wa ndege mjini Kuala Lumpur, Malaysia lakini Trump amekuwa akitamka wazi ‘nampenda kiongozi huyu, najivunia kukutana na kuwasiliana naye.’

Hata hivyo, kilicho wazi Trump ana hisia tata kuhusu Mashariki ya Kati na hata washauri wake wanasema hana ufahamu wa kutosha kuhusu eneo hilo.

Trump aliziita vita za Rais George W. Bush nchini Irak na Afghanistan miongoni mwa makosa makubwa kabisa katika historia ya urais wa Marekani.

Lakini pia akamkosoa vikali Obama kwa kutoishambulia Syria baada ya Rais Bashar al-Assad kuvuka mstari mwekundu uliowekwa na Obama alipotumia kemikali zenye sumu.

Mbali ya madai ya kuendekeza biashara, kisingizio kingine anachotumia Trump kuilinda Saudia ni kuiepuka kuipa kicheko Iran, hasimu mkuu wa Saudia.

Trump anasema bora Saudia kutawala eneo hilo kwani Iran inaongoza kwa madhambi na ushetani mwingi.

Alisema, “Ni mshirika wetu (Saudia) muhimu sana. Hasa wakati unapokuwa na Iran inayofanya mambo mengi mabaya, inakuwa bora kuleta uwiano kwa dunia.

Iran ni shetani mbaya sana, huku akisisitiza Prince Salman kamhakikishia hakufahamu uwapo wa mauaji hayo na atachukua hatua.

Lakini utetezi wake huo pamoja na ule wa Saudia, ambayo awali ilikana kuhusika na mauaji kabla ya kukiri lakini ukidai bahati mbaya ulilaaniwa duniani.

Kwa sababu maofisa wa Saudia 15 wakiwamo wasaidizi wa karibu wa Mohammed, wameonekana wazi wakiwasili uwanja wa ndege Istanbul na haiwezekani kundi lote hilo lije Uturuki bila MBS kufahamu.

Dhana kuwa mwandishi huyo alijirekodi kwa dunia kupitia saa yake ya Apple wakati akiteswa, kuuawa na kupotezwa haraka haraka ikabadili utetezi wa awali wa Saudia uliokana mauaji.

Vyombo vya usalama kupitia vifaa vyake vilivyokwepa kubainika vilinasa mkanda wa sauti na chanzo kimoja cha habari kinasisitiza kuwa pamoja na faili la video ya mauaji ya Khashoggi.

Na muhimu zaidi, Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan amelivalia njuga suala hilo, kupitia wasaidizi wake wa karibu hutoa kidogo kidogo ushahidi wa kilichojiri.

Mafanikio zaidi ya juhudi za Rais Erdogan yalionekana Ijumaa iliyopita wakati Serikali ya Saudia ilipotangaza kuwafukuza maofisa waandamizi watano na kukamata wengine 18 ikiwa ni matokeo ya uchunguzi, ambao kiongozi huyo wa Uturuki alishinikiza kufanyika.

Ukabadilisha hadithi ya msisitizo wa Saudia kuwa Khashoggi aliondoka ubalozini akiwa hai kuwa aliuawa bahati mbaya baada ya mahojiano kwenda mrama.

Miongoni mwa waliotimuliwa ni pamoja na Saud al-Quahtani, mshauri wa MBS, anayesemekana alikuwepo eneo la tukio na Naibu Mkuu wa Usalama Meja Jenerali Ahmed al-Assiri.

Rais Donald Trump aliita hatua hiyo ya Saudia kama mwanzo mzuri na kuifanya dunia ibaki kujiuliza nini mwisho wa simulizi hii ya kusisimsha hata kuliko sinema za kubuni.

Nchini Uturuki, Rais Erdogan ameonesha umadhubuti wake katika kushughulikia suala hili na kuchochea hasira ya dunia dhidi ya Saudi Arabia pamoja na shinikizo dhidi ya Marekani kumwadhibu mshirika wake huyo.

Wanadiplomasia wa Magharibi wanaamini kasi ya mwitikio wa kiongozi huyo wa Uturuki imechochewa na mseto wa uhasama wa kieneo, kidini na ujanja ujanja wa kidiplomasia.

Kwa mtazamo huo, Uturuki kwa ukweli au uongo wanaonekana kughadhibika kuwa majirani wao Saudia wameweza kufanya unyama katika ardhi yao.

Zaidi ya hayo, Erdogan ametumia fursa hiyo kupunguza kama si kusitisha kabisa kupanda kwa nguvu, ushawishi na umaarufu wa mrithi huyo wa ufalme, Mohammed bin Salman.

Zaidi ya hayo ikibidi yupo tayari kubomoa taswira ya Rais Trump, kutokana na ukweli uhusiano wa Marekani na Uturuki ziko chini kutokana na mlolongo wa mambo yakiwamo yanayomhusisha Erdogan na ukiukaji wa haki za binadamu.

Hata hivyo, Waturuki wana matumaini kubadilishana taarifa za kiinteljensia na Marekani kutachochea juhudi zao za kuboresha uhusiano na Taifa hilo.

Ijapokuwa Erdogan si kama alitaka janga hili litokee, kuna mtazamo kuwa ameitumia fursa hiyo vyema kistadi.

Wanaamini anachelewesha kutoa taarifa za kushtusha, akifanya kidogo kidogo ili kupima mwitikio wa Saudia na Marekani katika harakati zake za kuzishinikiza zije mezani kukarabati uhusiano.

Ikatoa ripoti katika magazeti ya Washington Post, the New York Times na Sabah, gazeti lililo karibu na utawala wa Erdogan ikiwamo maelezo ya ndege mbili binafsi zilizowasili na kuondoka kutoka Istanbul na maelezo ya majina na umri wa abiria wake wote 15, ambao wengi wanatokea vyombo vya usalama vya Saudia.

Mmoja wapo ni Maher Abdulaziz Mutreb, ambaye husafiri mara kwa mara na Mohammed bin Salman katika ziara za kidiplomasia.

Maelezo ya mkanda wa sauti wa gazeti la Sabah na lile rasmi la Uturuki nao ukawa silaha nyingine ya kuonesha.

Katika mkanda huo inasikika sauti ya Balozi mdogo, Mohammed al-Otaibi, akiwaambia wauaji, “Fanyeni nje si ofisini mwangu. Jamani mtaniingiza matatizoni.”

Mmoja wa maajenti anajibu, “Iwapo unataka kuishi wakati utakaporudi Arabia, funga mdomo wako.”

Maofisa wa Uturuki pia wameripoti katika mkanda huo ni sauti ya daktari wa Saudia, mtaalamu wa alama za vidole, ambaye amekuja kwa kazi maalumu;-kupoteza ushahidi wa kufanyika mauaji ya Khashoggi.

Daktari huyo kachero anakata kichwa na vidole vya Khashoggi na kusikika akitoa ushauri kwa wenzake kusikiliza muziki kama anavyofanya ili kupunguza uwezekano wa matatizo ya kisaikolojia kwa kushuhudia ukatili huo.

Iwapo ingekuwa filamu, ingekuwa mbaya mno kuitazama na ngumu kuamini kama inaweza kufanywa na watu wanaodai kuongoza wananchi katika nyakati hizi zilizostaarabika.

Hizo bado hazijatolewa kwa jumuiya ya kimataifa, Rais Erdogan anazishikilia kama silaha za manufaa ya baadaye.

Kwa ushahidi wote alionao ikiwamo pia wa mmoja wao kupewa kazi ya kujifanya kuwa ni Khashoggi akiwa amevaa mavazi, saa, miwani na ndevu bandia ili kuudanganya ulimwengu kuwa alitoka jengoni akiwa hai na kupotelea kusikojulikana.

Kwa sasa hakuna anayeweza kutabiri mwisho wa filamu hii kwa uongozi wa Saudia, uhusiano wa Marekani, Saudia na Uturuki na ushawishi wa kikanda wa Rais Erdogan.

Jana, Erdogan alitarajia kulihubutia Bunge la Uturuki na alisubiriwa kwa hamu kama atatoboa zaidi kama alivyoahidi.

Lakini huenda akafanya kidogo kidogo hadi kumaliza filamu akitegemea kunufaika na mchezo huu.

Erdogan ameshikilia ushahidi wenye nguvu zaidi ya kuibomoa Saudia na MBS, hivyo Saudia haingependa kuathirika zaidi.

Erdogan ni kama anawaambia Saudia na hata Marekani ‘kama hamtaki kuathirika zaidi na mmeanini ninao ushahidi njooni mezani tuyamalize.’

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles