33.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Mauaji ya Dada wa Bilionea Msuya kiza kinene

Anethe MsuyaNa Asifiwe George,

MAUAJI ya Mtumishi wa Wizara ya Fedha, Anethe Msuya (30)  ambaye ni mdogo wa Bilionea Erasto Msuya ambaye naye aliuawa katika mazingira ya kutatanisha, yameacha kiza kinene.

Anethe ambaye aliuawa juzi nyumbani kwake Kibada, Block 16 jijini Dar es Salaam kwa kuchinjwa na watu ambao vyombo vya dola havijawabaini bado, kifo chake kimezidi kuacha wingu zito baada ya jana Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro kusema kifo hicho kina utata.

Bila kufafanua utata huo, Kamanda Sirro aliliambia MTANZANIA Jumamosi kuwa hawezi kutoa ufafanuzi zaidi juu ya tukio hilo kwa sababu uchunguzi bado unaendelea.

“Jaribu kunitafuta kesho kama nitakuwa nimepata ufafanuzi nitakupa majibu” alisema Kamanda Sirro kwa ufupi huku akisisitiza kuwa hawezi kujibu maswali zaidi.

Taarifa ambazo gazeti hili limezipata toka Mbezi Makonde ambako umetengwa msiba wa Anethe zinaeleza kuwa matukio yanayofanana na hayo yamekuwa yakiiandama familia hiyo tangu kaka yao Erasto Msuya auawe mwaka 2013.

Mmoja wa wanafamilia hiyo alisema baada ya Erasto kupigwa risasi dada yao aliyetajwa kwa jina la Antuja naye alimwagiwa kitu kinachohisiwa kuwa ni sumu wakati akiwa amelala chumbani na hivyo kumuathiri.

Wakati akimwagiwa ‘sumu’ hiyo inaelezwa kuwa Antuja ambaye ni mfanyabiashara wa maduka ya nguo alikuwa amelala pamoja na mtoto wa marehemu Anethe aitwae Allan.

Tukio lingine ni lile lililotokea Desemba mwaka jana ambapo dada yake aitwae Ester na muwewe walipigwa risasi za mgongoni na kifuani wakiwa katika baa ya Hongera iliyopo Bamaga, Dar es Salaam.

Kutokana na matukio hayo kuiandama familia yao, baadhi ya ndugu wamesema yanatokana na visasi ambavyo wanasema kuisha kwake kutatokana na Rais John Magufuli kuingilia kati.

Kuhusu maisha ya kimapenzi ya marehemu Anethe, ndugu huyo alisema hayakuwa mazuri.

Alisema Anethe aliolewa na kwa bahati mbaya ndoa yake ilikaa mwaka mmoja ikaingia migogoro na hivyo kuachana na baba watoto wake.

MTANZANIA Jumamosi pia lilifika nyumbani kwa marehemu Anethe na kukuta nyumba imefungwa na hakukuwa na mtu yeyote zaidi ya gari iliyokuwa imeegeshwa nje nyumba hiyo.

Majirani wa marehemu Anethe walikataa kuzungumza chochote juu ya tukio hilo wakisema hakuna wanalolifahamu zaidi ya kuona maaskari wakiwa na gari waliofika nyumbani hapo juzi  na kisha kuuchukua mwili na kuondoka nao.

Mmoja wa majirani ambaye hakutaka jina lake litajwe alisema kabla hawajajua Anethe ameuawa, juzi gari la shule anayosoma mtoto wake lilifika na kupiga honi kwa muda mrefu lakini hakuna aliyetoka.

“Dereva akamuuliza jirani yetu mwingine hapa kwamba wanaokaa nyumba hiyo wako wapi, yule jirani akaita jina la mtoto na akaitika ila akasema mama bado amelala sijaandaliwa halafu akasema ana njaa, asijue kama mama yake ameuawa” alisema.

Taarifa nyingine mpya ambazo gazeti hili limezipata zinaeleza kuwa Anethe alikuwa mstari wa mbele katika kesi ya mauaji ya kaka yake Bilionea Erasto Msuya ambayo inaendelea kusikilizwa hadi sasa Moshi, Mkoani Kilimanjaro.

Kaka yake huyo aliuawa kwa kumiminiwa risasi 22 Agosti 7, 2013 katika Uwanja wa ndege wa KIA na hadi sasa watu saba wanashikiliwa kwa kosa hilo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles