31.7 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Matumizi ya dola yalivyoipiku Shilingi Jiji la Dar

BOTNa Bakari Kimwanga, Dar es Salaam

MATUMIZI ya dola ya Marekani dhidi ya Shilingi ya Tanzania yameshika kasi jijini Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT), umebaini matumizi hayo ya dola jijini Dar es Salaam yamefikia asilimia 0.3 ikiwa ni tofauti na mikoa mingine.

Licha ya hali hiyo baadhi ya viongozi na wananchi kwa muda mrefu wamekuwa wakipendekeza kuhusu matumizi ya shilingi katika sehemu zote kubwa yakiwamo maeneo ya biashara.

Utafiti huo ambao umefanyika katika mikoa ya Dar es Salaam, Arusha, Dodoma, Mbeya, Morogoro na Mwanza, pamoja na mikoa mitatu ya Visiwani Zanzibar.

Kutokana na hali hiyo, imebainika kuwa mfanyabiashara au mtoa huduma katika maeneo hayo hakuwa tayari kukubali malipo kwa fedha za Kitanzania huku akitaka malipo kwa dola ya Marekani kutokana na wateja wao kuwa ni wageni wa kitalii.

“Hii ilikuwa hasa kesi na nafasi ya ofisi za kukodisha vyumba katika baadhi ya maeneo hasa ya Masaki, Mikocheni, Upanga na Mbweni jijini Dar es Salaam. Na kwa Mkoa wa Arusha katika eneo la Kilombero pamoja na barabara zinazokwenda maeneo ya watalii,” unaeleza utafiti huo.

 

Ununuzi wa bidhaa

Kwa mujibu wa utafiti wa Benki ya Tanzania (BoT), inaelezwa kwamba kwa kawaida wakati ununuzi kwa bidhaa na huduma, Watanzania hawana utamaduni wa kubeba fedha za kigeni katika pochi zao na kama ingekuwa hivyo wangeshindwa kufanya shughuli kwa kutumia fedha za ndani.

Hali hiyo inatoa baadhi ya ushahidi kwamba kiwango ambacho fedha za kigeni hutumika kama si muhimu.

Katika jitihada za kutoa ushahidi wa kuaminika juu ya hilo, watafiti walitaka kutambua fedha ambazo wafanyabiashara nchini Tanzania ungependelea  kupokea kama malipo ya bidhaa na huduma.

“Kama zoezi hili lilikuwa likifanywa kwa siri katika maduka makubwa Shoppers. Matokeo yanaonyesha kuwa matumizi ya Dola kwa ajili ya shughuli za ndani si muhimu.

Asilimia 0.1 tu ya washiriki  walitaka malipo kwa dola  huku kwa upande wa Zanzibar walikuwa tayari kukubali malipo katika fedha za Kitanzania, hata kama bei waliitaja kwa kiwango cha dola za Marekani.

“Asilimia 3.1 ya washiriki kwa upande wa Bara na asilimia 4.5 Zanzibar walikuwa tayari kukubali malipo kati ya Dola au Shilingi za Kitanzania, wakati asilimia 96.8 ya washiriki (Bara) na asilimia 95.5 (Zanzibar) hupendelea malipo kwa kwa Shilingi ya Tanzania,” ilieleza sehemu ya taarifa ya utafiti huo.

 

Mbinu

Untitled-1 Mbinu zilizotumika katika utafiti huo ni pamoja na sampuli ya juu  ambapo watu 3945 waliohojiwa kwa upande wa Tanzania Bara na watu 290 walihojiwa kutoka Zanzibar.

Kwa upande wa Bara, sampuli alichukuliwa kutoka mikoa sita ya utawala, yaani Dar es Salaam, Arusha, Dodoma, Mbeya, Morogoro na Mwanza, wakati Zanzibar sampuli ilichukuliwa kutoka mikoa mitatu: Mjini Magharibi, Pemba Kaskazini na Kusini Pemba.

 

Matokeo ya utafiti

Pengine matumizi muhimu zaidi ya fedha yoyote ni kati ya kubadilishana au  malipo kwa bidhaa na huduma.

Uzoefu unaonyesha kwamba kwa hapa nchini ingekuwa zinaonyesha matumizi ya dola hufanyika kwa nadra hasa katika baadhi ya maeneo.

Kwa kawaida, wakati ununuzi kwa bidhaa na huduma, Watanzania hawana  utamaduni wa kubeba fedha za kigeni katika pochi zao na kwamba wakifanya hivyo wengi wao hukwama hasa inapofika kwenye matumizi hivyo kulazimika kutumia fedha za ndani.

Katika jitihada za kutoa ushahidi wa kuaminika kuhusu hali hiyo, watafiti walitaka kutambua fedha ambazo wafanyabiashara wa nchini wangependelea au kuwa kwao tayari kupokea kama malipo ya bidhaa na huduma pindi wanapouza.

Matokeo yanaonyesha kuwa matumizi ya Dola kwa ajili ya shughuli za ndani si muhimu ambapo asilimia 0.1 tu ya washiriki katika malipo kwa upande wa  Bara ndio hutumia  wakati waliohojiwa kwa upande wa Zanzibar walikuwa tayari kukubali malipo za fedha za Kitanzania.

 

Kauli ya BoT

Akizungumzia utafiti huo, Mkurugenzi wa Masoko na Fedha wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Paul Maganga, anasema utafiti huo ulifanyika kwa lengo la kubaini juu ya matumizi ya fedha ya Tanzania dhidi ya dola ya Marekani.

Kutokana na hali hiyo anasema walifanya utafiti katika maeneo yote yaliyotajwa ambapo kwa Jiji la Dar es Salaam walianza katika eneo la Manzese, Mbagala, Temeke hadi kufika Masaki, Mikocheni, Upanga na Mbweni.

“Unajua kiwango hiki cha matumizi ya dola hasa katika maeneo kama Masaki yanatokana na kuwa na wageni wengi ambao hupanga nyumba kwa dola na hata matumizi yao ya kawaida pia.

“Si huko tu hata Mikocheni na Mbweni pia na hili husabaishwa na namna maeneo yenyewe yalivyokaa lakini bado BoT pamoja na yote imekuwa na jukumu la kuhakikisha matumizi ya shilingi yanapewa kipaumbele katika huduma,” anasema Maganga.

Anasema katika utafiti huo ambao ulifanyika mwaka jana na matokeo yake kutolewa Mei, utasaidia kuchochea na kuangalia namna idara yake ambayo ndani ya BoT kuwa na ufuatiliaji zaidi.

 

Bunge na matumizi ya dola

Wakati wa Bunge la 10,  iliyokuwa Kamati ya  Kudumu ya  Bunge ya Viwanda, Uchumi na Biashara, ilieleza kutoridhishwa na kushamiri kwa matumizi ya dola ya Marekani badala ya shilingi ya Tanzania katika manunuzi ya ndani jambo  ambalo  limekuwa chanzo  kikubwa  cha kuporomoka  kwa  uchumi  wa  nchi.

Kutokana na hali hiyo waliitaka Serikali  kuchukua  hatua  mara moja katika kukabiliana nayo.

Katika maelezo hayo ya kamati yaliyosomwa na aliyekuwa mwenyekiti wake, Mahmoud Mgimwa, wakati akiwasilisha    taarifa ya kamati yake, alisema kitendo cha kutumia dola ni kosa kisheria.

Wakichangia taarifa hiyo, Mbunge wa Sumve, Richard Ndasa (CCM), alisema inashangaza kuona  agizo hilo japo lipo kisheria lakini halitekelezwi jambo alilodai kuwa inawezekana kuwa mfumo huo  unatumika kama uchochoro wa kutorosha fedha nje ya nchi.

 

Wachumi wanena

Mhadhiri wa Uchumi wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Profesa Honest Ngowi, anasema matumizi ya dola yameshika kasi kwa sababu thamani ya shilingi imeshuka.

“Shilingi inazidi kupoteza thamani, sera za fedha za nchi zinaweza zikashindwa kusimama vizuri na matokeo yake BoT itakuwa na uwezo mdogo kusimamia sera yake ya fedha.

“Cha msingi tuimarishe shilingi na kuuza bidhaa zaidi nje ya nchi, kuwepo mazingira wezeshi bidhaa za ndani zizalishwe zenye ubora wa kutosha ili watu wapende kuzitumia badala ya kuagiza kutoka nje kwa sababu tunapoagiza matumizi ya dola yanaendelea kuwa juu,” anasema Profesa Ngowi.

Naye Mhadhiri wa Uchumi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Humphrey Moshi, anasema hatua hiyo itasababisha kuongezeka kwa mfumuko wa bei kwa sababu shilingi na dola vinabadilika kila siku.

“Watu watapoteza imani na sarafu yao, hivyo kasi ya kuporomoka kwa shilingi yetu itazidi. Tuache kutumia sarafu mbili kwa wakati mmoja.

“Wenzetu wa Afrika Kusini na Kenya kama ukienda nchini mwao huwa hawataki sarafu nyingine zaidi ya za kwao,” anasema Profesa Moshi.

Profesa huyo anashauri sheria ambayo hairuhusu matumizi ya dola nchini itumike ili kusaidia kuimarisha shilingi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles