24.4 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 23, 2024

Contact us: [email protected]

‘MATUMIZI SAHIHI YA ARVS YANAPUNGUZA MAAMBUKIZI’

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu

Na Mwandishi Wetu – Ruvuma               |           


SERIKALI imesema mtu akitumia dawa za kufubaza makali ya Ukimwi (ARVs) kwa usahihi na ukamilifu anapunguza uwezekano wa kumwambukiza mtu mwingine virusi vya ugonjwa huo (VVU) kwa takribani asilimia 60.

Kauli hiyo ilitolewa mjini hapa jana na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, wakati akizindua kampeni ya ‘Furaha Yangu, Pima, Jitambue, Ishi’.

“Kwa mujibu wa wataalamu wa afya, ikiwamo wanasayansi, imedhihirika kwamba mtu akianza mapema kutumia dawa anapunguza uwezekano wa kupata magonjwa nyemelezi, anaongeza muda wa kuishi na anapunguza uwezekano wa kuwaambukiza watu wengine,” alisema.

Ummy alisema mtu akigundulika kuwa na maambukizi ya VVU ataanzishiwa dawa za kupunguza makali ya Ukimwi badala ya kusubiri hali yake kuwa mbaya zaidi.

Pia alisema wakati takwimu za kitaifa zikionyesha maambukizi ya VVU yamepungua kutoka asilimia 5.7 hadi 4.7, lakini bado maambukizi mapya yameendelea kuwapo na vijana wenye umri kati ya miaka 15 na 24, sawa na asilimia 40 wanaambukizwa.

Alisema asilimia 52 ya watu wanaoishi na maambukizi ya VVU wanajifahamu kuwa wana virusi hivyo na katika kila watu 100, basi 48 wenye maambukizi hayo hawajui kuwa wana VVU, jambo ambalo ni hatari katika kaya zao na taifa kwa ujumla.

Aliwaagiza watoa huduma kupitia kampeni hiyo kwamba wote wanaotumia ARVs kwa kuzingatia masharti wapewe dawa za miezi mitatu badala ya mwezi mmoja kama inavyofanywa sasa.

“Watu wote wanaotumia ARVs vizuri kwa kuzingatia masharti, wapewe dawa za miezi mitatu badala ya kila mwezi kwenda kuchukua dawa katika vituo vya kutoa huduma za afya, tunaamini kwamba hatua hii itachochea watu wengi zaidi kwenda kupima na kujiandikisha kupata huduma za dawa,” alisema.

Ummy aliwaagiza waganga wakuu wa mikoa kuhakikisha vituo vya afya vyote nchini ambavyo vimesajiliwa na kutambulika, vinatoa huduma za kupima VVU, kutoa ushauri nasaha na kutoa dawa.

“Maelekezo ambayo tumetoa Serikali, hatuoni ni kwanini katika kila kituo cha afya kisitoe huduma za kupima VVU, ushauri nasaha na kutoa huduma za ARVs,” alisema.

Katika hatua nyingine, alisema katika kila watoto 100 wanaozaliwa nchini, 11 walikuwa wanazaliwa na maambukizi ya VVU na ndani ya miaka miwili maambukizi hayo yamepungua kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto hadi kuwa chini ya asilimia tano kutoka 11.

Alisema katika kila watoto 11 wanaozaliwa na VVU, watano ndio wanazaliwa na maambukizi hayo na inawezekana kuwa na mtoto anayezaliwa bila maambukizi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles