24.7 C
Dar es Salaam
Tuesday, March 19, 2024

Contact us: [email protected]

MATOKEO KIDATO CHA SITA: MCHUANO MKALI SHULE ZA SERIKALI, BINAFSI, SEMINARI

Na Mwajuma Kombo, Zanzibar

BARAZA la Taifa la Mitihani (NECTA) limetangaza matokeo ya mitihani ya kidato cha sita iliyofanyika mwaka huu, huku ufaulu ukishuka kwa asilimia 1.26 baada ya jumla ya watahiniwa 70,552 sawa na asilimia 96.06 kufaulu tofauti na mwaka jana ambao watahiniwa 71,551 sawa na asilimia 97.32 walifaulu.

Pia katika matokeo hayo, shule za sekondari za Serikali na binafsi zimechuana katika nafasi 10 bora kitaifa, huku wanafunzi nao wakichuana katika kipengele cha waliofaulu vizuri zaidi kitaifa katika masomo mbalimbali.

 SHULE 10 BORA KITAIFA

Akitangaza matokeo hayo kwa waandishi wa habari mjini Unguja jana, Katibu Mtendaji wa Necta, Dk. Charles Msonde, alizitaja shule 10 bora zilizopata matokeo mazuri zaidi kitaifa na mikoa inayotoka ikiwa katika mabano kuwa ni Feza Girls (Dar es Salaam), Marian Boys (Pwani), Kisimiri (Arusha), Ahmes (Pwani), Marian Girls (Pwani), Mzumbe (Morogoro), St. Mary Mazinde Juu (Tanga), Tabora Boys (Tabora), Feza Boys (Dar es Salaam) na Kibaha (Pwani).

“Ubora wa shule umepangwa kwa kutumia kigezo cha wastani wa pointi (GPA) na upangaji wa shule zilizofanya vizuri umezingatia shule zenye idadi ya watahiniwa wasiopungua 30,” alisema Dk. Msonde.

Kati ya shule 10 bora kitaifa, za Serikali ni Kisimiri yenye idadi ya watahiniwa 58 ambayo kwa mwaka huu imeshika nafasi ya tatu na katika matokeo ya mwaka jana ya kidato cha sita iliongoza kitaifa kwa kushika nafasi ya kwanza, Mzumbe yenye watahiniwa 144 nayo imepanda kwa kushika nafasi ya sita kitaifa baada ya mwaka jana kushika nafasi ya nane, Tabora Boys yenye watahiniwa 129 imeshuka kwa kushika namba nane kutoka sita iliyoshika mwaka jana, huku Kibaha yenye watahiniwa 173 nayo imeshuka kwa kushika namba 10 kutoka saba mwaka jana.

Pia kati ya shule hizo 10 bora kitaifa, za binafsi ni Feza Girls yenye idadi ya watahiniwa 67 ambayo kwa mwaka huu imepanda na kuwa ya kwanza kutoka nafasi ya nne iliyoshika katika matokeo ya mwaka jana, Marian Boys yenye watahiniwa 94 na inayomilikiwa na Kanisa Katoliki imepanda kwa kushika nafasi ya pili kutoka nafasi ya tano iliyoshika mwaka jana, Ahmes iliyoko Bagamoyo, Pwani yenye watahiniwa 40 imeshika nafasi ya nne mwaka huu na imeingia kwa mara ya kwanza katika kundi hili licha katika matokeo ya mwaka jana watahiniwa wake wote 22 walipata kati ya daraja la kwanza na la pili, Marian Girls inayomilikiwa na Kanisa Katoliki yenye watahiniwa 108 nayo imeingia kwa mara ya kwanza kwa kushika nafasi ya tano, St. Mary Mazinde Juu yenye watahiniwa 149 na inayomilikiwa na Kanisa Katoliki nayo imeingia kwa mara ya kwanza kwa kushika nafasi ya saba, huku Feza Boys nayo imeshuka kwa kushika nafasi ya tisa kutoka nafasi ya pili iliyoshika mwaka jana.

Dk. Msonde alisema kwa mwaka huu, kati ya wanafunzi waliofaulu, wasichana ni 27,577 sawa na asilimia 97.21 wakati wavulana ni 42,975 sawa na asilimia 95.34.

Alisema jumla ya watahiniwa walioandikishwa ni 75,116 na waliosajiliwa kufanya mitihani ni 73,692 sawa na asilimia 98.10 na watahiniwa 1,424 hawakufanya mitihani.

Dk. Msonde alisema wanafunzi wa shule pekee waliofaulu mwaka huu ni 61,308 sawa na asilimia 98.12 ya waliofanya mitihani na idadi ya watahiniwa wa kujitegemea waliofaulu ni 9,244 sawa na asilimia 84.31.

Pia alisema ubora wa ufaulu kwa kuangalia madaraja waliyopata watahiniwa wa shule unaonyesha kuwa jumla ya watahiniwa 58,556 sawa na asilimia 93.72 wamefaulu katika daraja la kwanza hadi la tatu wakiwamo wasichana 22,909 sawa na asilimia 94.07 na wavulana 35,647 sawa na asilimia 93.49.

Alisema takwimu za ufaulu kwa watahiniwa wa shule zinaonyesha kuwa ufaulu katika masomo ya sayansi, biashara, lugha na sanaa haukuonyesha tofauti kubwa ya msingi ikilinganishwa na mwaka jana isipokuwa kwa somo la General Studies ambalo ufaulu wake umeshuka kwa asilimia 7.54 kutoka 71.24 ya mwaka jana hadi 63.70 ya mwaka huu.

WASICHANA WATAMBA

Dk. Msonde alisema katika mitihani ya mwaka huu, ufaulu katika madaraja unaonyesha wasichana wamefanya vizuri zaidi ikilinganishwa na wavulana na ubora wa ufaulu kwa wasichana ni asilimia 94.07 na kwa wavulana ni asilimia 93.49.

 WANAFUNZI BORA SAYANSI

Dk. Msonde aliwataja wanafunzi bora waliofanya vizuri katika masomo ya sayansi na shule zao katika mabano wakiongozwa na Sophia Richard Juma wa St. Mary Mazinde Juu.

Wengine waliomfuatia Sophia ni Agatha Julius Ninga (Tabora Girls), Nathanael Philemon Ndagiwe (Mzumbe), Mugisha Reynold Lukambuzi (Feza Boys), Innocent Beda Labule (St. Mary Goreti Kilimanjaro), Paschal W. Masaba (Kibaha).

Pia wamo Arsen J. Mwantuke (Marian Boys), Atuganile Cairo Jimmy (Feza Boys), Donel Lot Chihoma (Marian Boys) na Erck Gilbert Philipo (Kibaha).

WANAFUNZI 10 BORA KWA MASOMO YA BIASHARA

Dk. Msonde aliwataja wanafunzi bora waliofanya vizuri katika masomo ya biashara na shule zao katika mabano kuwa ni Rajabu Ally Mabaranga (Kibaha) aliyeongoza wakifuatia Gasto Theobald Kimario (Umbwe), Rashid Abdala (Tusiime), Munira J. Said (Benjamin William Mkapa High), Twalib Juma Namwake (Kibaha), Kassim Mohammed Kassim (Benjamin William Mkapa High), Emmanuel Amos (Umbwe), Zawadi F. Kisanga (St. Mary Goreti), Joyceline N. Nnkuu (Weruweru) na Amani S. Daima (St. Joseph Catherdal).

 WANAFUNZI 10 BORA KITAIFA MASOMO YA LUGHA NA SANAA

Mbali na hao, pia aliwataja wanafunzi wengine bora waliofanya vizuri katika masomo ya lugha na sanaa na shule zao katika mabano wakiongozwa na na Francis T. Samkyi (Feza Boys).

Wengine ni Jophray Ernest (Ilboru), Andrea Msafiri Nkondo (Ilboru), Rahel Malolela (Rugambwa), Innocencia Castory Ngowi (Kisimiri), Beatrix Fredick Gwanchele (Ganossa), Prosper Sabinus Komba (Kamene), Mwanahamis Mussa Patrick Mission, Zamda Hassan Msangule (Roneca Girl’s) na Isaya Warioba Kanire (St. Joseph Cathedral).

 

UBORA WA UFAULU WAIMARIKA

Dk. Msonde alisema ufaulu wa ujumla katika matokeo ya mwaka huu unaonyesha kuendelea kuimarika hadi kufikia asilimia 98.12 tofauti na mwaka jana ambao ulikuwa asilimia 97.94.

“Ubora wa ufaulu umezidi kuimarika. Pia idadi ya watahiniwa waliofaulu vizuri katika daraja la kwanza hadi la tatu imeongezeka kutoka asilimia 93.13 mwaka jana na asilimia 93.72 mwaka huu ikiwa ni ongezeko la asilimia 0.59, huku wasichana wakiwa wamefanya vizuri zaidi kuliko wavulana,” alisema.

Pia alisema takwimu zinaonyesha kuwa asilimia ya ufaulu wa jumla kwa wasichana ni asilimia 98.48 ikilinganishwa na asilimia 97.89 ya ufaulu wa jumla kwa wavulana na asilimia ya ubora wa ufaulu kwa wasichana  ni asilimia 94.07 na wavulana ni asilimia 93.49.

Alisema Necta itafanya uchambuzi wa kina wa matokeo kwa kila somo na kutoa machapisho yatakayowasilishwa kwa wadau wa elimu, zikiwamo shule zote za sekondari za juu nchini kwa lengo la kuwawezesha walimu kuzitumia kuboresha ufundishaji shuleni.

 SHULE 10 ZA MWISHO KITAIFA

Dk. Msonde, alizitaja shule 10 za mwisho kitaifa na mikoa zinakotoka ikiwa katika mabano kuwa ni Kiembesamaki (Unguja), Hagafilo (Njombe), Chasasa (Pemba), Mwenyeheri Anuarite (Dar es Salaam), Benbella (Unguja), Meta (Mbeya), Mlima Mbeya (Mbeya), Njombe (Njombe), Al-hisan Girls (Unguja) na St. Vicent (Tabora).

Kati ya hizo 10, Kiembesamaki yenye idadi ya watahiniwa 120 imeendelea kufanya vibaya zaidi baada ya kushika nafasi ya kwanza katika kundi la shule za mwisho tofauti na mwaka jana iliposhika nafasi ya sita, Benbella yenye watahiniwa 108 imeshika nafasi ya tano tofauti na mwaka jana iliposhika nafasi ya pili, Chasasa yenye watahiniwa 76 kutoka Pemba imeingia kwa mara ya kwanza, Al-hisan Girls yenye watahiniwa 41 imeshika nafasi ya tisa tofauti na mwaka jana iliposhika nafasi ya nane na kufanya idadi ya shule zilizofanya vibaya zaidi kutoka Zanzibar kupungua na kufikia nne tofauti na mwaka jana zilikuwa saba na nyingine zilizobaki zimeingia kwa mara ya kwanza katika kundi hili.

 MATOKEO YAFUTWA

Dk. Msonde alisema watahiniwa 10 walifutiwa matokeo yao kwa sababu ya udanganyifu na kati yao, saba ni watahiniwa wa shule na watatu wa kujitegemea.

Pia alisema wamezuia kutoa matokeo kwa watahiniwa 15 waliopata matatizo ya kiafya na kushindwa kufanya mitihani kwa baadhi ya masomo na watahiniwa 69 walipata matatizo ya kiafya na kushindwa kufanya mitihani kwa masomo yote na wamepewa fursa ya kufanya mwakani.

ALLIANCE GIRLS YAFUNGIWA

Dk. Msonde alisema wameifungia Shule ya Alliance Girls ya Mwanza kuendesha mitihani ya taifa hadi hapo Necta itakapojiridhisha kutokana na tukio lililolafanywa na shule hiyo la kuhatarisha usalama wa mitihani, kukiuka kanuni za mitihani na sheria ya usalama wa nchi ya utunzaji wa siri.

Dk. Msonde alisema shule hiyo ambayo katika matokeo ya mwaka jana ilishika nafasi ya tatu kati ya shule 10 bora zilizofanya vizuri kitaifa, inadaiwa kupitia Msimamizi Mkuu wa Mitihani, Justine Mtendamema, Msimamizi Msaidizi, Jackson Erasto na Askari mwenye namba H.5742D/C Elias aliyekuwa analinda wanadaiwa, kufungua bahasha ya kurudisha majibu kisha wakaving’oa na kuviondoa vielelezo vyote na kuifunga upya.

Alisema wanaamini kuwa uongozi wa shule hiyo uliwawezesha wasimamizi hao kukusudia kutenda uovu huo.

Dk. Msonde alisema wanaamini hivyo kutokana historia ya kuwapo kwa matukio ya ukiukwaji wa makusudi wa kanuni za mitihani ya taifa yaliyofanywa na mkuu wa shule na mmiliki wa shule hiyo na walishawapa onyo kwa maandishi kuwa endapo watarudia kukiuka kanuni za mitihani, hatua kali zitachukuliwa dhidi yao.

Alisema shule hiyo ikiachwa inaweza kupanga na kufungua bahasha yenye maswali ya mitihani na kusababisha taharuki na uvujaji kusambaa nchi nzima na kuisababishia Serikali hasara kubwa kwa sababu italazimika kuandaa mitihani upya.

- Advertisement -

Related Articles

1 COMMENT

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
584,000SubscribersSubscribe

Latest Articles