26.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Matapeli wamjaribu Waziri Mkuu

 

Na MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM

Kundi la matapeli kwenye mtandao wa kijamii wa Facebook limeibuka na kubandika matangazo yanayodai kwamba Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, ameshiriki sherehe ya uzinduzi wa tovuti ya www.boreshamaisha.ml ambayo inatoa mikopo ndani ya dakika 45.

Taarifa iliyotolewa jana na Ofisi ya Waziri Mkuu, ilikanusha kuwapo kwa mfumo huo kwani hautambuliki  na wala kiongozi huyo hajapata kushiriki kwenye jambo lolote la aina hiyo.

Taarifa hiyo ilieleza kwamba watu hao waliofungua ukurasa huo wa facebook hawana uhusiano wowote na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

“Tovuti hii ya www.boreshamaisha.ml inaonesha ni ya Malaysia wala siyo ya Tanzania. Wanasema wanatoa mikopo hiyo kutoka mfuko wa VICOBA TANZANIA ambao umeanzishwa katika mfumo wa intaneti pekee (online).

“Wanadai wanatumia mawasiliano ya teknolojia kwa uchukuzi wa haraka kupitia tovuti kwa lengo la kurahisisha upatikanaji wa mikopo kwa kila Mtanzania popote alipo.

“Wafunguaji wa akaunti hiyo, wametumia jina la Kassim Majaliwa na wameweka picha yake akiwa bungeni. Wanadai kwamba Waziri Mkuu alipokea barua kutoka vyama vya upinzani wakilalamika kwamba utoaji wa mikopo hiyo online kutoka kwenye mfuko wa VICOBA TANZANIA ni rushwa kwa ajili ya uchaguzi wa mwaka 2020.

“Pia wanadai Waziri Mkuu pamoja na viongozi wengine wamechangia fedha zao kwenye mfuko huo wa kijamii unaolenga kuwapatia Watanzania wote mikopo bila ubaguzi wa aina yoyote kwamba alishiriki uzinduzi wa tovuti hiyo,” ilieleza taarifa hiyo.

Kutokana na hali hiyo Watanzania wametakiwa kutambua kwamba Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, hajashiriki uzinduzi wa tovuti hiyo, hana uhusiano wowote na watu hao na wala hana akaunti ya facebook inayohamasisha Watanzania wapate mikopo kwa dakika 45 kupitia njia ya mtandao.

“Tunawaomba Watanzania wajiepushe na akaunti hiyo ya FACEBOOK kwa kuwa si halali na haina nia njema kwa watumiaji. Aidha, hiyo si akaunti ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa wala ofisi yake haijawahi kuunda akaunti ya mtandao yenye jina lake kwa matumizi yake binafsi au ya ofisi,” ilieleza taarifa hiyo

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles