29.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 18, 2024

Contact us: [email protected]

Maswali magumu Mo Dewji kutekwa

Andrew Msechu na Patricia Kimelemeta-Dar es Salaam

TUKIO la kutekwa kwa mfanyabiashara Mohammed Dewji maarufu Mo,  ambalo lilichukua takribani sekunde tano, limeacha maswali magumu huku baadhi ya watu wakionyesha hofi zaidi kuhusu usalama wa raia nchini.

Mo ambaye ni Mkurugenzi wa kampuni za Mohammed Enterprises, alitekwa jana alfajiri na watu ambao hawajajulikana   baada ya kufika kwenye Hoteli ya Colosseum,   Dar es Salaam, kwa ajili ya kufanya mazoezi ya viungo.

Kwa mujibu wa mashuhuda, Mo ambaye ni miongoni mwa mabilionea vijana Afrika, alifika kwenye hoteli hiyo na gari yake huku nyuma kukiwa na gari jingine lililokuwa likimfuatilia.

Baada ya kufika eneo la maegesho ya magari, Mo hakukawia kutoka katika gari yake na alipotoka tu, watekaji hao walimvamia na kumkamata kabla ya  kumwigiza kwenye gari yao.

Kwa mujibu wa vyanzo kutoka ndani ya hoteli hiyo, picha za kamera za usalama hotelini hapo, zinaonyesha kitendo cha kumvamia Mo na kumwingiza kwenye gari ya watekaji, kilichochukua karibu sekunde tano, kwa vile hakubisha.

Chanzo hicho kiliieleza Mtanzania kuwa picha hiyo ya kamera inaonyesha jinsi watekaji hao walivyoingia wakiwa nyuma ya gari yake  wakimfuatilia Mo.

Kilieleza kuwa  tofauti na gari lililoingia likimfuatilia Mo kwa nyuma, kuna gari jingine ambalo lilitangulia na lilikuwa limeegeshwa eneo la maegesho ya hoteli hiyo kabla ya Mo kufika.

Gari lililotangulia eneo hilo liliegeshwa pembeni mwa eneo ambalo mfanyabiashara huyo hupendelea kuegesha gari lake.

Mo alipofika eneo hilo, aliegesha gari lake pembeni mwa gari lililokuwa limetangulia eneo hilo na lile lililokuwa likimfuatilia  lilipofika hapo, liliegeshwa ubavuni mwa gari la Mo.

Kutokana na hali hiyo, magari mawili ambayo yanaaminika ni ya watekaji, yalikuwa sambamba na Mo, na aliposhuka tu kwenye gari lake  alimvamiwa na kutekwa.

Chanzo kingine kilieleza kuwa  wakati tukio hilo likitokea, walinzi wa hoteli hiyo, awali hawakuonyesha upinzani kwa watekaji lakini  walipotaka kutoka walinzi walichelewa kufungua lango kuu.

Walisema hali hiyo  ilifanya watekaja hao kushuka kwenye gari lao na kufyatua risasi juu na kufungua lango wenyewe na kutokomea.

Gazeti hili lilifika nyumbani kwa mfanyabiashara huyo eneo la Oysterbay  ambako walinzi walisema familia ilikuwa  kwenye vikao na haikuwa tayari kuzungumza wakati huo.

Hata waandishi walipofika nyumbani kwa baba yake, Gulam Hussein, pia walielezwa na walinzi kuwa familia yote ilikuwa  nyumbani kwa Mo ikiendelea na  vikao.

 

Mswali yaibuka

Tukio la kutekwa kwa mfanyabiashara huyo, limeibua maswali mengi ikiwa ni pamoja na ni nani aliyemteka? Je, ni tukio la ujambazi au la kisasi? Je, ni wafanyabiashara wenzake waliofanya tendo hilo?

Mengine ni; Je, watekaji wana dhamira ya kutaka fedha kutoka kwa familia hiyo tajiri au wanataka kulipiza kisasi? Je, ni tukio la siasa?

Je, ni watu gani walikuwa na ugomvi na mfanyabiashara huyo? Je, alikuwa ametoa taarifa polisi juu ya kuhofia usalama wake?

Je, walijuaje  kuwa huwa anaenda kwenye hoteli hiyo   kufanya mazoezi? Je, tabia ya Mo kuweka taarifa zake muhimu ikiwa ni pamoja na ratiba zake za kila siku ndiyo iliyofanya watekaji waweze kumpata kwa urahisi?

Je, baada ya risasi kufyatuliwa  kwa nini askari wa nje ya hoteli hiyo iliyo karibu na eneo ambalo wanaishi viongozi, hawakutoka?

 

Doria njia za kutoka, kuingia Dar

Wakati huohuo, Kamanda  wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa, alisema jeshi la polisi lilidhibiti njia zote za usafiri za kuingia na kutoka Dar es Salaam kwa kushirikisha kanda maalumu za polisi.

Alisema ili kuhakikisha   wahusika wanakamatwa,   polisi walikuwa wametawanywa kila kona kwa ajili ya kufanya msako.

Aliwaomba  wananchi wenye taarifa yoyote kuhusiana na suala hilo wafike ofisini kwake   kumueleza  aweze kuongeza nguvu.

“Tunawakaribisha wananchi wenye taarifa muhimu kuhusiana na suala hili waje ofisini nitawapa ushirikiano, tutawasikiliza na kuzifanyia kazi taarifa zao,” alisema Mambosasa.

Alisema  kuanzia sasa (jana) suala la kupotea kwa Mo litazungumzwa na yeye na si mtu mwingine  kuepusha upotoshaji.

“Tunajua watekaji wamemchukua na kumficha mahali, naomba niwaambie hakuna njia watakayoweza kumsafirisha kwa sababu tumedhibiti kila kona,” aliongeza.

Aliwataka wananchi wawe watulivu katika   kipindi hiki ambacho jeshi hilo linaendelea kufanya kazi yake.

“Vijana wangu wametawanyika kila kona, kila wakati wananipa taarifa ya kinachoendelea katika operesheni yao.

“Hivyo basis suala hili nitakua nalitolea majibu mimi na siyo mtu mwingine   kuepusha uvumi unaoweza kusababisha upotoshaji wa taarifa,” alisema.

Awali, akiwa kwenye eneo la tukio, Mambosasa alisema tukio hilo ni la utekaji nyara na ilikuwa haijajulikana sababu za utekaji huo.

Alisema   Jeshi la Polisi limeshajipanga katika maeneo yote kuhakikisha Mo anapatikana na wahalifu wanakamatwa.

Alisema zilipatikana  taarifa   saa 1.00 asubuhi na kwamba tukio hilo lilitokea majira ya saa 11.00 alfajiri, lakini hasa ilionekana yalikuwapo mazingira ya   taarifa kuchelewa kumfikia.

“Ninatoa onyo kwa hao walioshiriki katika tukio hilo, salama yao ni kuhakikisha   tunampata Dewji akiwa hai. Vinginevyo ni mambo mengine,” alisema.

Mambosasa alisema polisi wanaendelea kufanya upelelezi wa tukio hilo na matokeo ya awali ya upelelezi huo ndiyo yatakayowapa mwelekeo.

Alisema kuna mazingira magumu kidogo kwa sababu tukio la aina hiyo ni nadra kutokea nchini.

“Utekaji wa aina hii ni mpya hapa kwetu, kitendo hicho si chepesi hasa kwa namna watekaji walivyotekeleza tukio hilo bila hata walinzi kupiga filimbi na bila hata kelele ya aina yoyote, hata yowe ya kushtua watu waliokuwa Jirani. Tunaomba wananchi watupe ushirikiano katika hili,” alisema.

 

Makonda azua utata

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, naye alizua utata kutokana na taarifa aliyotoa akidai Mo amepatikana akiwa mzima lakini baada ya muda akakanusha taarifa hiyo.

Taarifa hizo zilizosambaa kwa kasi zilikanushwa na mkuu huyo wa mkoa ambaye alivitaka vyombo vya habari vilivyodaiwa kurusha taarifa hiyo kurekebisha na kukanusha.

Awali, Makonda alisema hilo ni tukio la ajabu ambalo halijazoeleka katika Mkoa wa Dar es Salaam na nchini kwa ujumla.

Alisema Mo ni mfanyabiashara mkubwa mwenye uwezo wa kulipa walinzi wowote anaowataka  lakini kwa sababu ya amani na usalama hakuwa na sababu ya kufanya hivyo, ndiyo maana alikuwa peke yake.

“Jambo kubwa kwetu ni kuhakikisha Dewji anapatikana akiwa salama, tuaendelea na kumtafuta na vikosi vyote vya ulinzi na usalama viko kazini kuhakikisha vinatekeleza wajibu wake wa kulinda uhai, usalama na mali za watu wetu,” alisema.

Alisema ni lazima wabainike waliohusika ni raia wa wapi.

Makonda alisema amwaagiza polisi kufanya ukaguzi kwenye hoteli zote, apartments na  viwanja vya ndege kupata taarifa za watu walioingia lakini pia katika mipaka yote, ikiwamo kuhakikisha wanazuia watu kutoka nje holela kwa sasa.

Alisema ana uhakika na weledi wa jeshi la polisi na vyombo vyote vya usalama kwa hiyo ana uhakika Mo atapatikana mapema.

 

Msikiti wa Jamatini

Mtanzania lilifika katika msikiti wa Jamatini ambao amekuwa akisali Mo na kuonana na uongozi jumuiya hiyo, ambao ulieleza kuwa haukuwa tayari kuzungumza kwa sasa.

Kiongozi wa Jumuiya hiyo, Sajjad Mustafa, alisema kulikuwa na  dua zilizokuwa zinaendelea msikitini hapo kumwombea  Mo.

Alisema uongozi   kwa sasa hauwezi kuzungumza lolote kwa kuwa msemaji wao ni Rais wa Jamatini, Azim Dewji ambaye kwa sasa yuko nje ya nchi.

Mijadala kwenye mitandao

Baada ya kusambaa  taarifa za Mo kutekwa kwenye mitandao  ya jamii jana asubuhi, watu walijitokeza wakilaani kitendo hicho na wengine kuonyesha hofu yao kuhusu usalama wa raia.

Kwa mfano baada ya taarifa tata ya Makonda, Rais wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS), Fatuma Karume, aliandika; “nimeshukuru sana watu waliomteka Mo wamepatikana baada dakika chache tu.

“Lakini mwaka mmoja baada ya mabomu kulipuka ofisini kwetu bado wahalifu hawajulikani na wewe Makonda unayesema mkoa wa Dar ni wako hujathubutu hata kuja kwenye tokeo! Tusemeje?

“Miaka miwili  baada ya Ben Saanane kutekwa bado mnasema hamjui katekwa na nani. Sasa mnataka tukueleweni vipi?

“Mwaka mmoja baada ya Tundu Lissu (Mbunge wa Singida Mashariki) kupigwa risasi 17 tena kwenye jiji dogo sana kama Dodoma, bado mnatwambia hamjui nani mhalifu.

“Mnataka tukueleweni vipi wakati tunajua kwamba mkitaka mna uwezo wa kukamata wahalifu katika  dakika chache tu?

“Wameichafua nchi walivyoteka watu, kutesa watu, kupiga risasi watu, kupiga mabomu maofisi ya watu!”

Mbunge wa Nzega, Hussein Bashe,  kupitia ukurasa wake wa Twitter aliandika, “inasikitisha na kustua tuko hili la Mo kutekwa, aina hii ya uhalifu inaota mizizi, ana familia ana watoto ana ndugu tuendelee kumuombea kwa Allah na kila mmoja wetu kutoa taarifa yoyote atakayopata ambayo itasaidia kumpata akiwa salama, Allah amlinde.”

Waziri wa Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais – Mazingira na Muungano,   January Makamba, katika ukurasa wake wa Twitter aliandika, “nimezungumza na baba yake Mo, habari za kutekwa kwa rafiki yetu Mo ni za kweli.

“Nimetikiswa sana. Naamini polisi watatoa taarifa kamili. Mohammed ana familia na watoto wadogo. Tumuombee yeye na familia yake. Tusaidie kutoa taarifa zitakazosaidia kupatikana kwake”.

Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe, aliandika, “Nimeshtushwa na kuumizwa na habari za kutekwa kwa ndugu yetu Mo leo alfajiri akiwa anakwenda mazoezini hapa Dar.

“Kila mmoja wetu mwenye taarifa zozote zinazoweza kusaidia kumwokoa asaidiane na vyombo vyetu vya dola. Mola atamsaidia MO na familia yake katika mtihani huu.”

Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa, aliandika, “kwa hali mbaya ya usalama wa Wantanzania ! Je ni sawa kuendelea kukiunga mkono Chama cha Mapinduzi! Wafanyabiashara, wakulima, wasanii, wanasiasa wa upinzanivyuo vikuu? Makanisa, misikiti, nani yuko salama? We want Mo back!”

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles