26.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Maswa awatangazia vita wabunge

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

Eliachim Maswi,
KATIBU Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliachim Maswi,

, ameingia katika vita ya maneno na wabunge kwa kuwaporomoshea   matusi huku akisema anataka kukabiliana nao nje ya Bunge.

Aliyasema hayo Dar es Salaam jana alipozungumza  na waandishi wa habari kuhusu mkakati na mwelekeo wa sekta ndogo ya umeme.

Maswi alitangaza ‘vita’ hiyo na wabunge alipokuwa akijibu maswali ya waandishi baada ya kumaliza kueleza mkakati wa sekta hiyo.

Waandishi walimtaka aeleze  mkakati wa wizara yake wa jinsi inavyokabiliana na mikataba mibovu  na matumizi mabaya ya fedha, mambo ambayo yanaweza kuigharimu wizara  na kuifanya ifikie malengo yake.

Akitoa maelezo, Maswi alisema wizara hiyo haijawahi kupitisha mikataba mibovu tangu awe katibu mkuu wake.

Maswi alisisitiza kuwa hakuna ukweli wowote kuhusiana na  madai ya matumizi mabovu ya fedha na kwamba hata ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali (CAG) iliipa wizara hiyo hati safi.

Hata hivyo, wakati akiendelea kutoa ufafanuzi wa masuala hayo,  ghafla alitaja majina ya baadhi ya wabunge kama vile Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila (NCCR-Mageuzi)  na mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (Chadema) akidai kuwa ni wezi.

“Tatizo la nchi hii kuna watu wanaongea tu… sasa wanatudhalilisha.  Mimi nataka mtu anayejiona ni mwanaume aje hapa aseme siyo tunatishana tishana tu hapa. Ukiwa bungeni ndiyo unajifanya ni mwanaume. Hawa Kafulila na Zitto ni wezi na washenzi.

“Wakati mtu mwenyewe ni mshenzi tu.  Hakuna hapa… kama mwanaume aseme huku nje na mimi niwaambie waandishi mkija mje na ushahidi.

“Mimi simtetei mtu najiamini sili rushwa. Mimi sichukui rushwa na sintochukua, niliwaambia mkitaka nifuatieni… unaweza kuja nyumbani kwangu nikakuonyesha vitu vyangu na kukuambia nilivipataje.

“Lakini mshenzi mmoja ananyanyuka huko… hoo Maswi mwizi, sijui nini, mshenzi tu.  Mimi nasema kama akiwa ni mwanaume aseme nje huku.

“Kwa nini usemee bungeni? Kwa sababu pale kuna immunity (kinga), kama wewe ni mwanaume useme kama mimi hapa halafu utanitambua kwamba mimi nani, nitakushughulikia tu.

“Hata na mimi juzi nilivyomsikia Werema (Mwanasheria Mkuu wa Serikali Jaji Frederick) anasema tumbili nikasema kweli katumbili kale, hatuwezi kuchezeana,” alisema na kuongeza:

“Naomba ukitoka hapa ukamwambie Kafulila kwa sababu najua ni mtu wake, ni mshenzi na mwambie nimesema ni mshenzi.  Kafulila na mwenzake Zitto wamechukua hela, mnafikiri sijui, najua na ni kwa sababu ya njaa, njaa zao tu, na nimemwambia kama yeye ni mwanaume aseme open hapa.”

Maswi alisema kwa sababu hiyo ndiyo maana   Zitto    hajawahi kuchangia hotuba ya Wizara ya Nishati na Madini   tangu yeye awe katibu mkuu wa wizara hiyo.

“Hawezi kuchangia kwa sababu namjua, mwizi mtupu… tangu niingie hajawahi kuchangia labda juzijuzi kwa sababu alikuwa na matatizo….naye Kafulila hivyohivyo tu.  We know (tunajua) kwa sababu mimi siyo mwanasiasa  siwezi kusema ovyo.

“Mimi nina ethics (miiko).  Mimi nimelelewa na kama hujalelewa nyumbani kwenu utalelewa na dunia, kwa hiyo (anamtaja mwandishi) kamwambie kwanza mimi namsubiri sana yaani nina usongo naye,” alisisitiza Maswi.

Katibu Mkuu huyo alisema aliwahi kumpigia simu Kafulila na kumwambia kama yeye ni mwanaume ayazungumze masuala hayo  nje ya Bunge.

Zitto ajibu

Akijibu tuhuma hizo dhidi yake, Zitto alisema  amemsikia Maswi. “Nimesikia na nimeona video, aseme nimeiba wapi? Mimi nasema wao wezi wameiba IPTL na nyaraka zimetoka, waseme wao nimeiba wapi na watoe ushahidi.”

Juzi Kafulila aliandika barua  kwenda kwa Spika wa Bunge, Anne Makinda, pamoja Mkuu wa Jeshi la Polisi  (IGP), Ernest Mangu, akilalamikia kile alichodai kutishiwa maisha na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Frederick Werema, kwamba atamkata shingo.

Makinda amshangaa Kafulila

Wakati huohuo,   Spika wa Bunge, Anne Makinda, jana alimtolea uvivu Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila (NCCR-Mageuzi) kwa kuvujisha taarifa za barua yake, akisema huo ni utovu wa nidhamu.

Makinda aliyasema hayo baada ya mbunge huyo kuomba mwongozo wa Spika akitaka kujua anashughulikiaje malalamiko yake ya kutishiwa maisha na   Werema.

Kafulila aliomba mwongozo huo   baada ya kipindi cha maswali na majibu, hatua ambayo ilionekana kumkera Spika kutokana na  kitendo chake cha kuvujisha barua yake  bila kusubiri majibu.

Makinda alishangazwa na malalamiko hayo na kueleza kuwa msingi wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuhamaki ulitokana na Kafulila kumuita mwizi.

Akiomba mwongozo wa Spika Kafulila alisema: “Wakati wa mjadala wa bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini niliibua ufisadi wa escrow. Mimi na mwenzangu John Mnyika tuliwasilisha ushahidi hapa bungeni kuhusiana na suala hili.

“Ni bahati bahati mbaya sana, hadi leo hatujui ushahidi ule uliupeleka wapi zaidi ya kuambiwa kwamba waziri anautumia kukosoa.

“Mwenendo wa jambo hili tangu lilipoanza kwa namna linavyokwenda hata jana Mwanasheria Mkuu wa Serikali alionyesha kusudio la kutaka kunipiga na baadaye tukiwa nje ya Bunge alitoa kauli ambayo inahatarisha usalama wangu.

“Jambo hili linalohusu zaidi ya Sh bilioni 200 katika nchi ambayo imeshindwa kutatua tatizo la shuka hospitalini na madawati shuleni.  Ni dhahiri kwamba linaleta shaka kuhusu dhamira ya Kiti ya kulishughulikia hata kuhatarisha maisha yangu mimi mwenyewe na wengine.

Akijibu mwongozo huo, Makinda,  alishangazwa na kitendo cha Kafulila kulizungumza suala hilo wakati akijua ni juzi tu alimuandikia barua   na kwamba ofisi yake bado inalishughulikia.

“Mheshimiwa Kafulila, kwanza kabisa wewe umeniandikia barua… kabla sijaiona barua, leo (jana) naisikia kwenye vyombo vya habari… kweli ni adabu hizo?  La pili, suala hili lina uamuzi kamili kabisa tumepeleka kwa CAG na TAKUKURU… madokument yako yote yanakwenda huko, ulitegemea sisi tufanye hukumu hapa? Hata ulivyoleta juzi nilikushangaa sana.

“Mheshimiwa Kafulila tunafanya naye kazi katika IPU (Umoja wa Mabunge Duniani) na ni mmoja wa vijana hodari sana lakini hili anaona kama nalimisshandle (silitalii maanani) sasa tunaanza kupata shaka ni suala la kawaida au si la kawaida,” alisema Spika.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles