31.2 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Masoko haramu ubadilishaji fedha yaibuka

*Benki Kuu yasema wapo waliokamatwa

Na WAANDISHI WETU -DAR ES SALAAM

WAKATI Serikali ikidhibiti biashara ya ubadilishaji fedha kwa kufunga maduka yaliyokuwa yanafanya biashara hiyo kinyume cha sheria na kutoa kanuni mpya zitakazoongoza sekta hiyo, imebainika kuwa baadhi ya wafanyabiashara wameanzisha biashara haramu (black market) ya kuuza fedha za kigeni.

Benki Kuu ya Tanzania (BoT), ilipotafutwa na MTANZANIA Jumapili kuzungumzia hali hiyo, ilikiri kufahamu tatizo hilo na kusema baadhi ya watu tayari wametiwa nguvuni.

Maeneo yanayotajwa kukithiri kwa biashara hiyo ni Kariakoo, Dar es Salaam huku zikiwepo taarifa za aina hiyo pia mkoani Arusha. 

Uchunguzi wa MTANZANIA Jumapili umebaini kuwa biashara hiyo hufanywa katika maduka ya kawaida yanayouza bidhaa nyingine tofauti kama nguo, sabuni na nyinginezo.

MTANZANIA Jumapili pia limebaini kuwa biashara hiyo hufanywa kwa usiri na mara nyingi huhusisha watu wanaofahamiana.

Katika kuthibitisha hilo, mmoja wa waandishi wa MTANZANIA Jumapili alijidai anataka kubadilisha dola za Marekani 20,000 na alipitia kwa mtu anayefahamiana na anayeendesha biashara hiyo.

Mtu huyo ambaye duka lake linauza sabuni katika eneo la Kariakoo, alihakikisha kupitia simu yake ya kiganjani kwamba anaweza kubadili kiasi hicho kwenda kwenye shilingi ya Tanzania.

Mwandishi huyo alipotaka kwanza abadilishiwe dola 100 kwa ahadi ya kurudi na kubadili nyingine 20,000 mfanyabiashara huyo alifanya hivyo.

Watu hao wanabadili dola moja ya Marekani kwa kati ya Sh 2,300 na 2,700. Inategemea kama unanunua dola ama unataka shilingi.

Pia MTANZANIA Jumapili limebaini kuwa wanaofanya biashara hiyo wana mtandao na ikitokea mteja anahitaji kiasi kikubwa cha fedha ambacho yeye hana, basi huwasiliana na wenzake.

Mbali na Dar es Salaam, pia MTANZANIA Jumapili limedokezwa kuwa mkoani Arusha ambako operesheni ya BoT ya kufunga maduka yasiyo na leseni ilianzia, nako biashara hiyo inaendelea kufanywa kwa njia hiyo hiyo, hasa katika maeneo ya mipakani na katikati ya mji.

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, akiwa ameambatana na Gavana wa BoT, Profesa Florens Luoga, aliwahi kueleza waandishi wa habari walichobaini hadi kufikia uamuzi wa kuyafunga maduka hayo ya kubadili fedha.

Dk. Mpango alisema walibaini uondoshwaji wa fedha katika mfumo rasmi na kuekelezwa katika utakatishaji wa fedha haramu.

Alisema katika operesheni iliyofanywa mikoa ya Arusha na Dar es Salaam, walibaini pia upokeaji wa amana kutoka kwa wafanyabiashara kinyume cha matakwa ya leseni za biashara husika.

UFAFANUZI WA BOT

Meneja Uhusiano wa BoT, Zalia Mbeo, alikiri kuwapo wafanyabiashara na watu binafsi wanaojihusisha na biashara ya kubadilisha fedha za kigeni bila kuwa na leseni ya Benki Kuu.

“Kama Benki Kuu ilivyoutangazia umma katika vipindi mbalimbali, kufanya biashara ya kubadilisha fedha za kigeni bila kuwa na leseni ni kinyume na sheria ya nchi na yeyote atakayepatikana atachukuliwa hatua za kisheria.

“Vyombo mbalimbali vya usalama vinaendelea kuwasaka wafanyabiashara na watu wote wanaojihusisha na biashara hii bila kufuata utaratibu ili wachukuliwe hatua stahiki,” alisema Zalia.

Alisema bila kutaja idadi kuwa tayari wafanyabiashara kadhaa na watu binafsi wamekwishakamatwa na kufunguliwa mashtaka kwa kujihusisha na biashara hiyo haramu.

“Benki Kuu inapenda kutoa tena rai kwa umma kushirikiana na vyombo vya usalama na Benki Kuu kwa kutoa taarifa pale wanapoona wafanyabiashara au mtu yeyote anafanya biashara ya kubadilisha fedha za kigeni kinyume na utaratibu ili hatua ziweze kuchukuliwa,” alisema Zalia.

Alisema ushiriki wa umma katika kudhibiti uhalifu ni muhimu ili kumaliza uhalifu wowote ule, ikiwemo ‘black-market’.

Zaidi Zalia alisema zipo baadhi ya hoteli zimekuwa zikiuza dola kwa kuongeza bei kinyume na bei elekezi ya soko jambo ambalo pia si sahihi.

Alisema hoteli zinaruhusiwa kutoa huduma ya kubadilisha fedha za kigeni kwa wateja wake, hasa pale wanapokuwa wanahitaji kufanya malipo kwa huduma walizopokea katika hoteli husika. 

“Benki Kuu inatambua kuwa katika baadhi ya hoteli, mabenki yamefungua maduka ya kubadilisha fedha za kigeni baada ya kupata kibali cha Benki Kuu.

“Watu binafsi pia wanaruhusiwa kufungua maduka hayo katika hoteli ili kuwahudumia wateja kwa ujumla, wanapokuwa wamekidhi vigezo na kupewa leseni na Benki Kuu.

“Aidha, hakuna bei elekezi ya kubadilisha fedha za kigeni,” alisisitiza.

Alipoulizwa na MTANZANIA Jumapili kuhusu idadi ya maduka yaliyopewa leseni, yanayotoa huduma hiyo kwa sasa ukiacha hoteli na benki, Zalia alisema ni matatu.

“Maduka ya kubadilisha fedha za kigeni ambayo leseni zao za biashara hazikusitishwa kupisha uchunguzi ni matatu,” alisema.

Alisema maduka hayo yanayo matawi katika sehemu mbalimbali nchini.

“Baada ya uchunguzi kukamilika, maduka yatakayokuwa hayana makosa ya kikanuni au kisheria yataruhusiwa kuendelea na biashara kwa kuzingatia vigezo vipya vilivyoainishwa katika kanuni za biashara ya kubadilisha fedha za kigeni 2019 iliyochapishwa katika Tangazo la Serikali Na. 450 Juni 7, 2019 na kuwekwa kwenye tovuti ya Benki Kuu,” alisema Zalia.

KANUNI

Chini ya kanuni hizo, baadhi ya masharti yaliyowekwa kwa mtu atakayetaka kuanzisha maduka ya kubadili fedha ni pamoja na kutakiwa kujaza fomu, barua mbili kutoka kwa wadhamini ambao si jamaa.

Mengine ni chanzo cha mtaji kilichoambatana na maelezo ya kuanzisha biashara hiyo, mfumo wa uendeshaji biashara.

Pia atatakiwa kuwa na uthibitisho wa mtaji wa kiasi cha shilingi bilioni moja kutoka kwa msajili wa kampuni.

Atatakiwa kutoanzisha biashara hadi pale mifumo ya kiusalama kama vifaa vya kiusalama na mawalisiano vimefungwa na kukaguliwa.

Kulipa ada ya mwaka ambayo ni shilingi milioni moja katika kila tawi.

Masharti mengine ni uthibitisho wa uraia kwa kila mbia na kila mkuu wa tawi.

Lakini pia itatakiwa kuwa na wakurugenzi wa bodi angalau wawili na ambao watathitibishwa na Benki Kuu na kazi yao itakuwa ni kuangalia operesheni karibu zote zinazofanywa na duka la kubadili fedha.

Duka litakalojihusisha na biashara ya kusafirisha fedha litatakiwa kuweka fedha kwenye akaunti maalumu kwa ajili ya biashara hiyo na fedha zote zinazopokewa kutoka kwa wateja kwa ajili ya malipo.

Kusafirisha fedha nje itatakiwa wawasilishe nyaraka kama ‘invoice’ ya shughuli yenyewe kama shule, matibabu au kazi.

Zaidi duka la kubadili fedha litatakiwa kuwa na mkaguzi ambaye amesajiliwa na Bodi ya Wakaguzi na Wahasibu.

Kanuni hizo pia zinataka Benki Kuu kutoa ama kutotoa taarifa wakati itakapotaka kufanya uchunguzi kwenye duka lolote.

Pia zimetamka wazi kwamba mtu yeyote anayejihusisha na biashara ya kubadili fedha atakuwa amefanya kosa iwapo muhusika atakuwa ametoa taarifa zisizo sahihi wakati wa mchakato wa kupata leseni.

Kwamba atakuwa amejipatia fedha za kigeni kinyume na sheria.

Au kama mahakama imemtia hatiani kwa makosa ya udanganyifu na utakatishaji fedha, adhabu yake kwa mujibu wa kanuni hizo ni wenye leseni watasimamishiwa huduma hiyo kwa kipindi kisichozidi mwaka mmoja ama kunyang’anywa kabisa.

Atatozwa faini ya dola za Marekani 3,000.

IDADI YA MADUKA

Ukiacha kanuni hizo, kuhusu idadi ya maduka yaliyokuwepo kabla ya operesheni ya kuyafunga nchi nzima, Zalia alisema yalikuwa takriban 107.

“Maduka mengi yalifungwa kwa muda kupisha uchunguzi ambao uko katika hatua za mwisho,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles