33.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Masheikh walia na Katiba Mpya

Waumini wa Kiislamu wakiswali
Waumini wa Kiislamu wakiswali

Na Waandishi Wetu, Dar na mikoani

SUALA la Mahakama ya Kadhi ambalo wiki chache zilizopita lilileta mgogoro ndani ya Bunge Maalumu la Katiba hadi kufikia Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kulitolea ufafanuzi, limeibuka tena katika swala ya Eid El-Hajj nchini.

Hatua hiyo imewafanya masheikh mbalimbali nchini kusema katu hawako tayari kuitambua Rasimu ya Katiba inayopendekezwa hadi pale suala la Mahakama ya Kadhi litakapotambuliwa.

Wamesema kitendo cha Bunge Maalumu la Katiba kukiondoa kipengele cha mahakama hiyo kwenye rasimu hakikubaliki kwao.

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana katika Baraza la Idd lililoandaliwa na Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania na kufanyika katika Msikiti wa Magomeni Kichangani, Msemaji wa jumuiya hiyo, Sheikh Rajab Katimba, alisema sasa wanajipanga kuzunguka nchi nzima ili kukwamisha Rasimu ya Katiba inayopendekezwa.

Alisema hatua ya kutupwa kwa mapendekezo ya Waislamu katika Katiba hawakubaliani nayo kwani hata maneno ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda ni kuwahadaa kuliko hali halisi.

“Sababu yetu sisi Waislamu kuikataa Rasimu ya Katiba inayopendekezwa ni kutupwa na kupuuzwa kwa madai ya muda mrefu ya Waislamu, kila siku tumekuwa ni watu wa kusubiri huruma hali ya kuwa ni haki yetu.

“Suala la Mahakama ya Kadhi lilikuwa kwenye Ilani ya Uchaguzi ya CCM lakini halikufanyiwa kazi kwani hata ahadi ya Waziri Mkuu kwetu ni sawa na danganya toto,” alisema Sheikh Katimba.

DODOMA

Kwa upande wake, Sheikh wa Mkoa wa Dodoma, Mustapha Shaaban, alisema kutokuwepo kwa Mahakama ya Kadhi katika rasimu inayopendekezwa hawataiunga mkono Katiba hiyo.

Alisema kwa muda mrefu Waislamu wamekuwa wakiomba kuwepo kwa mahakama hiyo lakini bado Serikali na watendaji wake wamekuwa hawaoni uzito kuhusu suala hilo.

“Mahakama hii ya kadhi ni muhimu sana kwetu Waislamu na itashughulikia masuala ya ndoa, talaka, mirathi, eda pamoja na migogoro ya misikiti, hatutampa mtu adhabu ya viboko kama Serikali inavyodhani,” alisema Sheikh Shabaan.

Alisema ni lazima Serikali itambue kuwa sasa si wakati wa kudanganyana kama kuku na kifaranga na kinachotakiwa ni kutenda kuliko kusema bila utekelezaji.

Sheikh huyo alisema kuwa Uislamu ni dini ya amani na utulivu na kwamba endapo wakimuona mtu anauchezea Uislamu ni lazima wawe wakali kutokana na kuishi kwa kufuata mafunzo ya Mtume Muhammad (S.A.W).

Mwanza

Naye Sheikh wa Mkoa wa Mwanza wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA), Sheikh Salum Fereji, amesema suala la Mahakama ya Kadhi ni muhimu kwa imani ya Kiislamu na lazima iwepo ili mambo yanayohusu Uislamu yahukumiwe kwa mujibu wa utaratibu uliowekwa na Mwenyezi Mungu.

“Sisi tunahitaji na tunasubiri watangaze kama alivyoahidi Waziri Mkuu, tunategemea ije na ikae kwenye sheria, hatutachoka kuidai hadi kieleweke, sitegemei Serikali kama itavunja ahadi yake,” alisema.

Akizungumza juu ya makadhi waliochaguliwa Dodoma, Sheikh Fereji alisema hawatambuliki katika Katiba kwa hiyo inakuwa haina maana uwepo wao ambapo alisisitiza madhehebu na dini nyingine kutoingilia suala hilo kwani liko kati ya Serikali na Waislamu.

Awali Mjumbe wa Baraza la Masheikh Mkoa wa Mwanza, Sheikh Hassan Kabeke, aliiasa Serikali itekeleze ahadi aliyotoa Waziri Mkuu kabla suala la Mahakama ya Kadhi halijaleta machafuko, pia aliitaka Serikali imalize suala hilo kwani lilianza kipindi cha awamu ya pili ya Rais Alhaji Ali Hassani Mwinyi, lakini mpaka leo halijapatiwa ufumbuzi.

“Waislamu ni raia wa Tanzania, wana haki kama raia wengine kudai mahitaji yao ya msingi, tunaomba suala hilo litekelezwe hapo Januari mwakani kama lilivyoahidiwa na Serikali kupitia kwa waziri mkuu,” alisema Sheikh Kabeke.

Septemba 29, mwaka huu Waziri Mkuu, Mizengo Pinda alilazimika kuokoa jahazi  ili kunusuru Katiba Mpya kwa kupoza hasira za Waislamu kuhusu Mahakama ya Kadhi kutoingizwa kwenye Katiba inayopendekezwa.

Pinda aliwaahidi kuwa Januari mwakani, Serikali itawasilisha bungeni muswada wa sheria ili kuutambua uamuzi unaofanywa na Mahakama za Kiislamu.

Tamko hilo lilitokana na kuwapo kwa hali tete bungeni baada ya Waislamu kuhamasishana kupiga kura ya Hapana iwapo mahakama hiyo isingeingizwa kwenye Katiba.

Wakati wajumbe Waislamu wakishikilia msimamo huo, baadhi ya wajumbe dini nyingine waliweka msimamo kupiga kura ya Hapana kama ibara hiyo ingeingizwa kwenye Katiba.

Hali hiyo iliisukuma Kamati ya Uongozi ya Bunge Maalumu chini ya Mwenyekiti, Samuel Sitta, kukutana mfululizo na baadhi ya viongozi wa dini na Waziri Mkuu kwa ajili ya kutafuta mwafaka.

Akitoa tamko la Serikali, Pinda aliahidi kuwa Januari mwakani, Sheria ya Mahakimu sura ya 11 na Sheria ya Kiislamu sura ya 375 zitafanyiwa marekebisho ili kutambua uamuzi wa Mahakama ya Kadhi. Lengo ni kuhakikisha umoja na mshikamano vinadumu kwa Watanzania, ikiwamo kuyakubali maeneo saba yanayolalamikiwa na Waislamu. Alisema wajumbe katika kamati ya uongozi walijiridhisha kuwa madai ya Waislamu kuhusu mahakama hiyo ni ya msingi.

Habari hii imendaliwa na Shabani Matutu (Dar) Abubakari Akida (Mwanza), Ramadhan Hassan na Pendo Mangala (Dodoma).

- Advertisement -

Related Articles

1 COMMENT

  1. mahakama hii mbona zipo na zinatenda kazi kama huku singida , hii nyingine ni ipi au mnataka ruzuku ya serikali kodi ya watu wote, hii ndiyo baba wa taifa alikataa. hapo kuna mtego msipounasua mtashuhudia ya nigeria.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles