23.3 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

MASHA: NINA MAISHA YANGU, SIHITAJI MADARAKA

Na ELIZABETH HOMBO

MIAKA miwili iliyopita, jina la Lawrence Kego Masha liliibuka katika ulingo wa kisiasa nchini, baada ya kukihama Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kujiunga na  Chama cha Demokrasia na Maendeleo-Chadema, Agosti 17, mwaka 2015.

Masha ni miongoni mwa baadhi ya makada na viongozi wa CCM waliokumbwa na upepo wa kukihama chama hicho kabla ya kufanyika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, kwa kile kilichodaiwa kuwa ni kumfuata Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, ambaye jina lake lilikatwa katika kura za maoni za kugombea urais ndani ya CCM.

Masha, aliyepata kuwa waziri wa mambo ya ndani ya nchi wakati wa utawala wa awamu ya nne, pia alikuwa mbunge wa Nyamagana, kabla ya kushindwa na Ezekiah Wenje wa Chadema katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010. Kitaaluma Masha ni wakili wa kujitegemea.

Hivi karibuni Masha alibadili tena uamuzi na kutangaza kurejea CCM, akidai kuwa, upinzani wa sasa umeridhika na hali ya kuendelea kuwa wakosoaji ili kukisaidia chama tawala kujirekebisha.

MTANZANIA Jumapili limefanya mahojiano maalumu na Masha nyumbani kwake, Mikocheni, jijini Dar es Salaam, pamoja na mambo mengi, amezungumzia maisha yake ya kisiasa.

MTANZANIA JUMAPILI: Baada ya kurudi CCM, unadhani safari yako ya kisiasa ndiyo imeishia hapo au utakwenda tena chama kingine cha siasa?

MASHA: Nimekulia katika familia ya kisiasa na kitu nilichofundishwa niipende nchi yangu. Ufanye kile ambacho unaona ni sahihi kwa ajili ya maendeleo ya nchi yangu, leo hii tunavyoongea sioni sababu ya kujiunga na chama chochote cha upinzani.

Rais Magufuli anafanya kazi ambayo wananchi wamekuwa wakiomba ifanywe kwa muda mrefu, sisi wengine katika shughuli tunazozifanya hatufanyi kwa ajili ya tunatafuta kitu au tunataka kitu, tunafanya kwa ajili ya maendeleo ya watoto wetu na Watanzania kwa ujumla.

Leo nikisema Rais John Magufuli hafanyi kazi nitakuwa muongo. Imani yangu ni kwamba Rais Magufuli ana nia njema na nchi na anataka kuibadilisha na kazi anafanya.

Suala la kuniuliza sijui baada ya miaka 50 nitafanya nini nafikiri si sawa, lakini kama nilivyoeleza siku ile nilivyokubaliwa kule, mimi hapa nitakuwa mwaminifu kwa CCM na nitakuwa mwaminifu kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

MTANZANIA JUMAPILI: Umesema Rais anafanya vizuri, lakini miezi miwili iliyopita ulikuwa kwenye mkutano wa Chadema na wanahabari, ukapinga kwa nguvu zote kuwa nchi inaendeshwa kwa kutofuata sheria, je, bado unaamini hivyo?

MASHA: Hapana! Ni vyema mngesikiliza kwa makini nilichokisema siku ile. Nilichokisema ni kwamba, tunaomba pamoja na nia njema sheria ifuatwe, kuna procedure zina process ambazo zinatakiwa kufuatwa.

Bahati mbaya sisi wengine ambao tulipata kushika fursa ya madaraka tunatambua kabisa kwamba huwa kuna uwezekano wakati mwingine pamoja na nia njema uliyonayo, unaweza kuruka kabla hujatakiwa kufika pale unapotakiwa kwenda.

Kikubwa ambacho kinatakiwa kufanyika ni kwamba, kwanza washauri wake wa karibu na yeye mwenyewe atambue kwamba tunayo Katiba na sheria za nchi hii na zinatakiwa kufuatwa.

Ukizifuata inasaidia kwa sababu kesho na keshokutwa hakuna mtu ambaye anaweza kuuliza kwanini hili lilifanyika kwa sababu the law is there (sheria ipo).

MTANZANIA JUMAPILI: Ulipokuwa unakemea pale kwenye mkutano wa wanahabari, ina maana uliona kuna kitu hakifanyiki na sasa hivi kinafanyika?

MASHA: Ninachotaka kusema ni hivi, mimi nilipojiunga na CCM hata juzi hapa nilisema katika maongezi mbalimbali tofauti Magufuli si malaika, ni binadamu, lakini ana nia njema na nchi.

Kukosea au kupoteza step kidogo wakati mwingine si kosa lake, yeye ana watu wanaotakiwa kumshauri ili aweze kufika kule anakotaka kwenda.

Kikubwa tunachotakiwa kuangalia ni dhamira ya mtu ni kipi anachotaka kukifanya kwa ajili ya watu wake na wataalamu wamsaidie kuhakikisha kwamba tunafuata process ambazo zinatakiwa kufuatwa.

MTANZANIA JUMAPILI: Kwenye hilo la Katiba na sheria, unadhani mpaka sasa wataalamu wake wanamshauri vyema?

MASHA: Tatizo ambalo ninaliona hivi sasa unajua nafasi ya Rais ni kubwa sana na naamini kabisa kuwa, kuna watu wengi wanamwogopa na kwa bahati nzuri au mbaya Rais amekuwa serikalini kwa miaka mingi, pia anajua ujinga unaofanyika serikalini na mimi nimekaa serikalini nafahamu vizuri.

Hivyo unatakiwa kuwa na watu ambao kwanza wanakuheshimu, pili ni wataalamu kweli na tatu wanakueleza ukweli. Hicho ndicho kinachotakiwa.

Nimecheka sana hapa juzi, unajua mimi nilipohama kuna watu wakakaa wakasema Masha amehamia njaa. Masha anasubiri uteuzi. Hivi mbona hawakusema nilipohamia Chadema au ni teuzi gani niliokuwa nausubiri nilipoingia Chadema.

Mimi nimelelewa kwamba unatakiwa kujenga nchi yako, kitu ambacho nimekuwa nawaambia watoto wangu siku zote ni kwamba kama Mtanzania kisomo ulichokipata, kazi unayoifanya ushauri unaoutoa unatoa kwa manufaa yako wewe binafsi au unatoa kweli kwa sababu ya taifa lako.

Mwisho wa siku history is the greatest judge, unaweza ukatukanwa na kila mtu Tanzania leo hii, kwa sababu hawatambui wewe unachokisema ni kitu kwa ajili ya manufaa yao.

Lakini baada ya miaka 50 anayeandika historia atakaa akasema kwamba huyu aliwahi kusema ukweli, kuna vitu vingine si sifa yetu, kwanini tudanganyane tuwe wakweli.

Naweza kutambua mtu akiwa na ugomvi na serikali, lakini ukiniambia kuwa serikali ya CCM haijawahi kufanya kitu huyo mtu anatakiwa kuombewa.

Hata mimi kipindi niko kule nilikuwa nikipata mshtuko mtu ambaye amezaliwa Tanzania ambaye anaweza akathubutu kusema serikali ya TANU na CCM haijawahi kufanya kitu chochote, ni mtu ambaye anatakiwa kuombewa.

MTANZANIA JUMAPILI: Ulihama Chadema ukijua serikali ya CCM inafanya kazi vizuri sasa au?

MASHA: Hapana, nilihama kwa sababu zangu, hata siku niliporejea ndani ya chama nikasema sababu zangu wao wanazifahamu, sina sababu ya kuanza kuyatangaza, lakini nilipohama na kurejea CCM kutoka Chadema nilieleza wazi kwenye waraka wangu kwamba kimsingi hawa watu hawako tayari kutawala.

MTANZANIA JUMAPILI: Nini kilikufanya ukahama mwanzoni au uliona wako tayari kupata dola, baada ya miaka miwili sasa unasema hawako tayari?

MASHA: Wakati ule nilichokiona CCM hawakuwa serious (makini) kupata dola; process ndani ya chama hazikufuatwa kama zinavyopaswa kufuatwa.

Ninachosema sasa hivi ni jinsi uongozi wa CCM ulivyo, nikiangalia process zinazofuatwa, nikiangalia chama kinavyoendeshwa napata moyo kuna uwezekano mkubwa kwa haya yanayofanywa.

MTANZANIA JUMAPILI: Unaamini kwamba yanayofanywa na serikali ya CCM hivi sasa yako sawa kwa asilimia 100?

MASHA: Asilimia 100 haiwezekani kwa sababu wanaoongoza ni binadamu, tutakuwa tunadanganyana hapa. Wewe unafikiri kila kitu kinachofanyika mimi nafurahia?

MTANZANIA JUMAPILI: Kipi ambacho hukifurahii?

MASHA: Sasa ni hivi, kwa bahati mbaya hapa si mahali pake, kama nikitaka kumshauri Rais nakaa naye namweleza, mwisho wa siku anaamua yeye katika nchi ya watu milioni 50, Rais ni mmoja na mwisho wa siku ana maamuzi yake.

Kazi yangu ni pale ambapo nina uwezo wa kumshauri nimshauri properly, mwisho wa siku maamuzi ni ya kwake. Niliwahi kuambiwa na mtu mmoja ambaye naye amefanya kazi serikalini sitamtaja, alisema hivi, Rais umfikishie ujumbe, umpatie information (taarifa), lakini mwisho wa siku tambua yeye ndiye rais, si wewe.

MTANZANIA JUMAPILI: Katika kipindi kidogo ulichorudi CCM au ulipokuwa upinzani, ulishawahi kumshauri Rais?

MASHA: Mimi sina nafasi yoyote ndani ya CCM wala sina nafasi yoyote ndani ya serikali, sasa leo hii mimi namshauri kama nani?

MTANZANIA JUMAPILI: Kuna taarifa kwamba ulipokuwa Chadema hukuwa na msaada na muda mwingi ulitumia kulewa, pengine hii ni moja ya sababu iliyokufanya uhame kwa sababu ulilitambua hilo?

MASHA: Hapa nilipo nimewahi kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Tanzania Oxygen Limited, nimekuwa waziri wa mambo ya ndani, nilikuwa Mtanzania wa kwanza kuingia kwenye Jukwaa la Kimataifa la Uchumi (WEF) kama kiongozi kijana kutoka Tanzania.

Kunywa pombe sikatai kama nakunywa, I drink alcohol wala sifichi. Unajua tofauti zetu ni hivi; mimi nakwenda baa nanunua pombe nakunywa hadharani, wengine wanalewa chumbani.

Swali langu nitajie kazi niliyovuruga kutokana na kunywa pombe kipindi chochote kile nilichokuwa kazini. Sikuwahi kuwa na cheo Chadema, nilikuwa mwanachama wa kawaida.

MTANZANIA JUMAPILI: Wakati ulipotangaza kuhamia CCM, Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, aliandika katika mitandao ya kijamii, kuwa maamuzi yako yametokana na tamaa ya pombe, hili unalizungumziaje?

MASHA: Si kazi yangu kumwongelea Lema, wote tuna udhaifu wetu, namheshimu mdogo wangu, lakini mbona nilipohamia Chadema hakuyasema haya?

Wote tumekuwa tukisoma kitabu cha sizitaki mbichi hizi, namheshimu Lema, yuko kwenye chama chake akae pale aendelee kufanya kazi, sitamtukana, sitamsema, mimi nitakachofanya ni kuongelea mustakabali wa maendeleo ya taifa letu.

Na ukweli ni kwamba leo hii tunavyoongelea maendeleo ya Tanzania, mtu ambaye hakubali Magufuli (Rais) anafanya vizuri hata kama kuna matatizo along the way.

Tunachotakiwa kufanya ni kutoa pongezi katika lile zuri na yale ambayo unaona ni mabaya toa ushauri wako wa namna ya kurekebisha.

Sisi sote ni Watanzania, hakuna mtu ambaye atafaidika hapa Tanzania kwa nchi yetu kuwa na sura mbaya kwa mtazamo wa watu nje ya nchi yetu. Unapokaa kazi yako ni kubomoa tu, hivi hata moja la kusifia huna?

Maajabu ni kwamba, baadhi ya vitu ambavyo vinaongelewa sasa hivi, ni yale ambayo yamekuwa yakisemwa na upinzani, mimi nafikiri kikubwa ambacho tunatakiwa kufanya sisi Watanzania, watu waanze kuongelea hoja.

MTANZANIA JUMAPILI: Ulikuwa msaidizi wa Mwenyekiti wa Chadema-Freeman Mbowe kwenye mambo ya nje na umewahi kumsindikiza kwenye baadhi ya balozi, ukiwamo ubalozi wa Canada, je, wakati unaondoka ulimuaga?

MASHA: Ni kweli nilimsindikiza ubalozi wa Canada wala nisiseme uongo. Walikuwa wana nia ya kuniteua, lakini ninavyofahamu sijawahi kuteuliwa kuwa msaidizi wake. Lakini kwa kuwa nilifundishwa kujitolea muda wote, siku yoyote kipindi kile Chadema walipokuwa wakinihitaji nilikuwa napatikana.

Hata kama walitoa vyeo vya mezani kwa sababu nafanya kazi kwa ajili ya taifa langu, hivyo nasimamia kwa ajili ya nchi yangu, hivyo naheshimu kazi anayoifanya Magufuli.  Akija mtu mwingine ambaye hafai, hilo ni jukumu langu kusema pia na yule anayefanya vizuri ni lazima nimheshimu.

MTANZANIA JUMAPILI: Ziko taarifa kwamba una mpango wa kugombea Jimbo la Sengerema, je, taarifa hizi zina ukweli wowote?

MASHA: Ni hivi, mimi natoka Sengerema, kama mwanachama wa CCM, nina haki zote za kugombea, lakini sijatangaza popote pale kwasababu kwanza muda haujafika.

Naomba nilieleze hili kwa mtu yeyote ambaye ananifahamu na kunijua vizuri, mwaka 2010 kwenye kamati ya siasa ya Wilaya ya Nyamagana nilitangaza hadharani kwamba sitagombea Nyamagana na nikamuomba Stanslaus Mabula agombee, mimi sina shida na madaraka.

Watu wengi hawajui kwamba niliamua kutokugombea mwenyewe. Ndani ya Chadema waliniomba nigombee; walinipa sehemu tatu za kugombea nikazikataa zote, lakini ninachosema ni kwamba, nilikataa kipindi kile nilichowaambia na kama ninasema uongo waje wakane.

Niliwaambia kuna watu wamejenga hiki chama, sisi ambao tumehamia huwezi kuingia kwa jina lako ukasema unachukua nafasi, walikuwa tayari kuniteua kati ya majimbo matatu lakini nilikataa, kuna watu wanasema mtu ana uchu wa madaraka, hata uenyekiti wa kanda ya Victoria nilikataa mwenyewe. Wengine tuna maisha yetu hatuhitaji madaraka.

MTANZANIA JUMAPILI: Wakati unachukua uamuzi wa kurudi CCM je, ulimuaga Lowassa?

MASHA: Sikumweleza, hata siku ile wakati najiunga na CCM nilisema nitaendelea kumheshimu kama mzee wangu na atakayesema simheshimu mzee Lowassa atakuwa mwehu.

Nitaendelea kumheshimu baba yangu, sijamuaga na sijaongea naye hadi leo hii, lakini kila mtu ana akili yake kwamba kinachofanyika hivi sasa CCM ni sawa, lakini kinachofanyika Chadema si sawa, lakini atabaki kuwa baba yangu, nitaendelea kumheshimu, sitamtukana, sitamsema popote.

MTANZANIA JUMAPILI: Unayazungumziaje matukio ya kulala selo ukiwa Chadema

MASHA: Nilikiona cha mtema kuni, ni zaidi ya kuonana na Osama Bin Laden. Niliwekwa ndani pale Oystebay Polisi na kama Mwigulu (Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Nchemba) ananisikiliza pabadilishwe, hapafai pale, nimekaa pale for one night (usiku mmoja) lakini nilikipata.

Nikakimbizwa kesho yake kwenda Kisutu nikanyimwa dhamana, nikalala Segerea, kimsingi ninachotaka kusema haya mambo yanatokea katika mapambano yoyote na yamenipata.

Mpanda nilikuwa nina kesi nikawa naenda kila mwezi, namshukuru Mungu kuwa nilishinda kesi zote.

Mwisho wa siku kila mtu anajua ukiongea na kukitaka chakula cha mwenzako utashughulikiwa, hivyo ulitambue hilo, mimi si nilishughulikiwa?

MTANZANIA JUMAPILI: Unadhani bado kuna haja ya kuendelea kuwa na mfumo wa vyama vingi?

MASHA: Vyama vingi lazima viwepo.  Hakuna nchi inayotawala bila kuwa na chama ambacho kinawapa changamoto ya kuleta maendeleo.

Lakini suala la kukaa jukwaani kuanza kutishia watu na kutukana mara unawaita ma-CCM kwani huhitaji kura zao? Wakati mwingine nikikaa na mama zangu wanasema sasa hawa wanaotukana majukwaani tukiwapa madaraka itakuwaje?

MTANZANIA JUMAPILI: Wakati uko Chadema ulipata kusema kuwa tukio la kushambuliwa kwa Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, si fedheha Serikali kuomba uchunguzi kutoka nje, je, bado unaamini hivyo?

MASHA: Naamini jeshi letu linaweza kufanya uchunguzi, lakini pia si fedheha kuomba msaada. Ilitokea Kenya aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje, Dk. Robert Ouko, ambaye alipotea ukafanyika uchunguzi kutoka nje.

Huwezi ukamtakia mabaya mtu aliyepata matatizo kama Lissu, ndiyo maana hata juzi Samia (Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan) alimtembelea hospitalini Nairobi.

Kwa sababu tutakuwa nchi ya wanyama kama Mtanzania mwenzako anapatwa na matatizo halafu unakosa utu wa kusema kwamba huyu nimjali, nimfuate, nimtakie mema.

Unajua nimekaa kwenye siasa kwa muda mrefu, hata kama mnashindana kwenye siasa huwezi kumfanyia mtu vile kama alivyofanyiwa Lissu, tungeleta hawa watu wa upande wa pili wa kuongeza nguvu labda watu wangekuwa na imani.

Hawa wanaosema Jeshi lote la Polisi ni baya huwa siwaelewi, sasa ina maana kesho au keshokutwa ukichukua nchi utaweza kubadili jeshi lote la polisi? Utamtoa wapi IGP kama si hawa waliopo, huwezi kuniambia ndani ya Jeshi la Polisi watu wote ni wabaya.

- Advertisement -

Related Articles

1 COMMENT

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles