25.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 23, 2024

Contact us: [email protected]

MARUFUKU KUWAAMBIA WANAFUNZI WAMEPENDEZA- SALMA KIKWETE

Na KENNETH NGELESI-MBEYA


MAMA Salma Kikwete amewaonya wanaume kuacha tabia ya kuwaambia wanafunzi wa kike wa shule za msingi na sekondari kwamba wamependeza.

Alisema kauli ya kupendeza haina lengo jingine bali kuwarubuni na kuwashawishi kufanya nao mapenzi.

Kauli ya mama Salma ambaye ni mke wa Rais Mstaafu, Jakaya Kikwete  ni ya pili katika kipindi kifupi baada ya ile ya kuwataka watoto wa kike kubana mapaja yao ili kuepuka mimba za utotoni.

Akiwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya siku ya mtoto wa kike Oktoba 11 mwaka huu, chini ya Shirika la Room to Read  Mailimoja mkoani Pwani, mbunge huyo wa kuteuliwa alisema watoto wa kike lazima watambue thamani ya usichana wao kwa kufunga mapaja, kwani kufanya hivyo hakuna mdudu yeyote atakayeingia katikati yake.

“Nimelazimika kutumia lugha hii nyepesi ili watoto wote wanielewe ninachomaanisha, itaweza kusaidia kuliko kutumia lugha ngumu ambayo inaacha maswali”alisema.

Kauli ya sasa ameitoa katika mahafali ya Sekondari ya St Marcus ya mkoani Songwe Oktoba 23 mwaka huu, ambapo aliwambia wahitimu wa kidato cha nne, wazazi wa wanafunzi kwamba tabia ya kuwasifia watoto wa kike kuwa wamependeza inazidi kushamiri lakini lengo kuu ni kuwashawishi kimapenzi.

“Niwaambie wanaume wote wanaowaambia wasichana wa shule kuwa wamependeza kwa lengo la kuwashawishi kufanya nao mapenzi wakome ..waache kuwarubuni kwa maneno hayo machafu ambayo hayafai kwa watoto wa shule” alisema.

Kuhusu wanafunzi, mama Salma alisema si kosa kwa mwanafunzi wa kike kuwa na rafiki wa kiume kwani rafiki wanaweza kusaidiana kimasomo, lakini si urafiki wa kufanya naye mapenzi.

‘Nyie watoto wa kike kuwa na ‘boy friend’ si tatizo kwani ni rafiki wa kiume lakini siyo kwa mapenzi unapaswa uwe na “boy friend” wa kukusaidia kukokotoa fizikia, bioloji na masomo mengine lakini si kufanya mapenzi, narudia tena fungeni mapaja yenu’ alisema Mama Salma.

Akizungumzia umuhimu wa kuwapo kwa shule binafsi nchini, mama Salma aliiomba Serikali kuendelea kuweka mazingira mazuri na rafiki kwa wadau mbalimbali kushiriki katika uboreshaji wa maendeleo ya elimu nchini.

Aidha kabla ya kuhutubia mahafali hayo, Mama Salma alitembelea shule hiyo na kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa bweni na kutoa msaada wa  mifuko 200 ya saruji kwa ajili ya ujenzi.

Pia aliahidi kuwasomesha wanafunzi watano ambao wanatoka Jimbo la Songwe na wana uwezo darasani lakini hawana uwezo wa kumudu gharama za masomo kuanzia kidato cha kwanza na kuendelea.

Mbali na mifuko hiyo alitoa msaada wa kompyuta tano za kisasa kwa shule hiyo ambayo ina wanafunzi wa awali msingi na sekondari.

Mmiliki wa shule hiyo, Philip Mulugo alisema shule hiyo ambayo ilianzishwa mwaka 2014 imendelea kufanya vizuri katika taaluma kwani katika mtihani wa kidato cha nne mwaka jana shule hiyo ilishika nafasi ya pili kimkoa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles