27.9 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Marufuku kusafirisha masanduku ya kura

Damian Lubuva_NEC2*Tume yasema matokeo yatatangazwa vituoni

*Fomu ya matokeo ya urais kuskaniwa jimboni

NA JONAS MUSHI, DAR ES SALAAM

MWENYEKITI wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji Mstaafu Damian Lubuva, amesema kura zote za urais, ubunge na udiwani, zitahesabiwa katika vituo vya kupigia kura na matokeo yote kutangazwa hapo hapo na ni marufuku kusafirisha masanduku ya kura kama ilivyokuwa zamani.

Jaji Lubuva aiyasema hayo Dar es Salaam jana katika mkutano na wawakilishi wa walemavu   kujadili namna bora ya wao kushiriki katika Uchaguzi Mkuu Oktoba 25 mwaka huu.

Alisema katika uchaguzi wa  mwaka huu ni marufuku kuhamisha masanduku ya kura kwa sababu vituo vya kupigia kura vitabadilika kuwa vituo vya kuhesabia kura baada ya upigaji kura kumalizika.

“Kura zote za urais, ubunge na udiwani zitahesabiwa katika kila kituo na matokeo yatabandikwa vituoni hapo hivyo sijui wanaosema kura zitaibiwa zitaibiwaje,” alisema JajiLubuva na kuongeza:

“Baada ya matokeo kubandikwa katika kila kituo yatapelekwa katika kata husika   kujumlishwa na hapo pia yatabandikwa.

“Mshindi wa udiwani atatangazwa hapo na yale ya ubunge na urais yatapelekwa jimboni ambako yatajumlishwa na mshindi wa ubunge atatangazwa na kukabidhiwa cheti huku ya urais yakipelekwa makao makuu ya Tume.

“Matokeo ya urais yatabandikwa katika kila jimbo na fomu ile ya matokeo itaskaniwa na kutumwa moja kwa moja makao makuu ya tume kwa kupitia mkongo wa mawasiliano wa taifa badala ya simu za mkononi kama ilivyokuwa awali,” alisema Lubuva.

Alisema njia hiyo ya itasaidia matokeo kufika kwa haraka kama inavyotakiwa na baada ya tume kupokea matokeo hayo itakuwa ikiyatangaza moja kwa moja kupitia luninga na redio.

Jaji Lubuva alisema  njia nyingine iliyoandaliwa ya kutuma matokeo ni kwa nukushi (fax) ambako  halmashauri zote nchini zimepatiwa vifaa vitakavyoziwezesha kuyatuma matokeo haraka.

Alisema hatua ya tume kutangaza matokeo hayo kupitia luninga na redio itasaidia wananchi kulinganisha matokeo watakayokuwa nayo na yatakayokuwa yanatangazwa na tume.

Kutokana na hali hiyo alivishauri vyama vya siasa viache kauli za kuwataka wafuasi wao wasiondoke vituoni baada ya kupiga kura kwa vile  hakuna kura zitakazoibiwa.

“Sioni haja ya vyama kusema vinalinda kura kwa sababu kura zote zinabaki vituoni na zitahesabiwa palepale tofauti na zamani ambako zilikuwa zikipelekwa kata na jimboni kuhesabiwa,” alisema.

Jaji Lubuva pia alivitaka vyama vya siasa kuacha kuingilia majukumu ya Tume hiyo ikiwamo kuhoji mabadiliko ya watendaji yanayofanywa ndani ya taasisi hiyo.

“Navishauri vyama vya siasa viache kuingilia majukumu ya Tume, haviwezi kutuchagulia na kutuambia pale weka karani fulani hapa fanya hivi… waache kuingia jikoni wasubiri chakula kipikwe watakula kwa haki wala wasiogope,” alisema.

Ametoa kauli hiyo  siku chache baada ya vyombo vya habari kumnukuu Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), akisema Mkurugenzi wa Tehama wa Tume hiyo, Sisti Cariah ameondolewa katika nafasi hiyo huku akihusisha mabadiliko hayo na maandalizi ya  kuiba kura.

Hata hivyo NEC ilikanusha taarifa hizo   ikisema hakuna mtu yeyote aliyehamishwa katika idara zake zote isipokuwa wakuu hao wa idara walichelewa kuwasilisha picha zao ndiyo sababu  hawajaingizwa katika orodha iliyomo katika tovuti ya Tume.

Jaji Lubuva alisema daftari la mwisho la wapiga kura litakamilika baada ya wiki mbili hadi tatu na wapiga kura watapata fursa ya kulihakiki kwa siku nane kabla ya uchaguzi.

Lugha chafu

Mwenyekiti huyo wa NEC alionya na kuahidi kukichukulia hatua chama chochote cha siasa kitachokiuka maadili ya uchaguzi kwa siku zilizobaki za kampeni.

“Kuanzia leo tunatangaza kuchukua hatua mara moja kwa chama kitakachokiuka kanuni za maadili ya uchaguzi ikiwamo kuongeza muda wa kampeni, kutumia maneno yasiyo na staha na kauli za kupotosha,” alisema Lubuva.

Hatua hizo ni pamoja na kukisimamisha chama kupiga kampeni, kulipa faini na adhabu nyingine kama inavyoelekezwa kwenye kanuni.

Alisema  amekuwa akishangazwa na kitendo cha baadhi ya wagombea na wanasiasa wanaopanda majukwaani kuwasema vibaya wagombea wenzao kwa kuwakashifu badala ya kutumia nafasi hiyo kutangaza sera ya vyama vyao na wagombea wao.

Hadi sasa kuna   wapiga kura milioni 23.7 ambao wanasifa za kupiga kura na   idadi hiyo inaweza kuongezeka kutokana na taarifa za wapiga kura kuendelea kuchakatwa, alisema.

Naye Kaimu Mkurugenzi wa NEC, Emmanuel Kawishe, alisema kuna vituo 72,000 vya kupigia kura ambavyo vitawekwa katika mazingira yatakayozingatia mahitaji ya watu wenye ulemavu.

Alisema mwaka huu watu wasioona wataweza kupiga kura peke yao kwa vile zipo karatasi za maandishi ya nuktanundu.

“Walemavu wataweza kupiga kura peke yao tofauti na zamani lakini pia watakuwa na nafasi ya kwenda na ndugu kama watahitaji,” alisema.

Mkurugenzi huyo alisisitiza umuhimu wa wasimamizi wa uchaguzi kuhakikisha walemavu wanapewa kipaumbele wakiwamo pia wazee na wanawake wajawazito ili wasipange foleni.

Kuhusu mawakala wa vyama vya siasa, alisema vituo vitakuwa na wakala hao wakati wote wa   upigaji kura na kituo kisipokuwa na wakala msimamizi wa kituo hazuiwi kuendelea na hatua ya  kupiga kura.

Wagombea waliofariki dunia

Akizungumzia uchaguzi wa madiwani na wabunge ulioahirishwa kutokana na kufariki dunia wagombea, alisema uchaguzi huo utafanyika Novemba 22 mwaka huu.

Uchaguzi huo utahusisha majimbo ya Lushoto na Ulanga Mashariki   na kata tano za Bomang’ombe-Hai, Bukene-Shinyanga, Msingi- Mkamala Singida, Muleba- Kagera na Uyole-Mbeya.

“Mchakato wa uchaguzi huo utakuwa kama ifuatavyo: uteuzi utafanyiaka Oktoba 12, kampeni Oktoba 13 hadi Novemba 18 isipokuwa siku ya uchaguzi Oktoba 25 na 26 na siku ya kupiga kura itakuwa Novemba 22 mwaka huu,” alisema Kawishe.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles