28.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

MARIDHIANO MAKINIKIA YAIBUA HOJA MPYA

Na WAANDISHI WETU

SIKU moja baada ya Serikali na Kampuni ya kimataifa ya uchimbaji madini ya Barrick Gold kufanya maridhiano katika maeneo takribani 14 kama njia ya kutatua mgogoro wa udanganyifu uliokuwa ukidaiwa kufanywa kwenye mchanga  wa madini (makinikia), zimeibuka hoja mpya.

Baada ya mazungumzo yaliyodumu kwa takribani miezi mitatu, juzi pande hizo mbili zilizokuwa katika mgogoro zilifikia maridhiano pamoja na mengine kwa kampuni hiyo kutoa asilimia 16 ya hisa zake kwenye kila mgodi wake nchini, asilimia 50 ya faida ya mauzo, na zaidi ikitoa Sh bilioni 700, huku mazungumzo yakiendelea kuhusu ulipaji wa fedha nyingine.

Miongoni mwa hoja zilizozua maswali katika makubaliano ya juzi ni namna ya kufanikisha ugawanaji wa faida asilimia 50 kwa 50 na Serikali ya Tanzania, wakati ziko taarifa zinazodai kuwa, kampuni hiyo imekuwa ikipata hasara baada ya mauzo.

Mbali na hilo, hoja nyingine iliyozua maswali ni namna kiasi cha Sh bilioni 700 ambazo Barrick imekubali kuilipa Tanzania kitakavyolipwa, huku hatima ya zaidi ya Sh trilioni 400 zinazopaswa kulipwa na kampuni hiyo kutokana na madai ya udanganyifu kwenye makinikia ikiwa bado haijulikani.

KABUDI AFAFANUA

Pengine ni kwa hoja kama hizo, jana Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi, alilazimika kueleza namna ambavyo Serikali itanufaika kwa asilimia 70 kupitia makubaliano hayo, hasa katika eneo la kumiliki asilimia 16  na lile la kugawana faida kwa asilimia 50 kwa 50.

Kabudi, ambaye alirekodiwa na video yake kurushwa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, alisema amelazimika kufafanua jambo hilo kwa  kwa sababu baadhi ya watu hawajaufahamu vizuri .

Alisema kabla ya kugawana faida ya asilimia 50 kwa 50, kampuni hiyo italazimika kulipa kwanza kupitia kodi zote za serikali, kama loyalty (mrahaba) asilimia 6, kodi ya mapato asilimia 30, ushuru wa mafuta na barabara, huduma kwa jamii, na ushuru kwa halmashauri za wilaya.

Alifafanua kwamba, zikijumuishwa kodi zote kabla ya mgawo wa 50 kwa 50, Serikali itakuwa haipati asilimia 50 tu, bali ni 70 kwa 30.

“Kwa hiyo ningependa hilo lieleweke wazi kabisa, yale mapato stahili ya Serikali yanabaki pale pale kama yalivyo ndani ya sheria na kinachokuja kugawanywa 50 kwa 50 ni kile kilichobaki baada ya kodi zote na ushuru wote wa serikali kulipwa na ndio nasema mtu mwenye asilimia 16 anakuja kupata asilimia 70 jumla, kwa maana ile ya kodi ya serikali na ile 50 kwa 50.

“Atakayesema hayo si mafanikio basi tumwombee kwa Mwenyezi Mungu ampe akili, macho na masikio ya kuona, kufahamu yaliyofanikiwa na hilo halijawahi kutokea kokote duniani,” alisema Profesa Kabudi.

Alisema mtindo huo ni tofauti kabisa na ule wa 50 kwa 50, ambao Kampuni ya Barrick imetumia nchini Dominica, Saud Arabia na Argentina, ambao unajumuisha pia na kodi ambazo serikali inazikusanya.

Alisema wakati wa majadiliano, Serikali ya Tanzania ilikikataa kipengele hicho na kilikuwa ni moja ya mambo yaliyoleta mvutano mkubwa.

Kuhusu makinikia, Profesa Kabudi alisema watu wengi walidhani shughuli yao ilikuwa ni suala la makinikia tu, jambo ambalo si kweli, kwani walibeba mambo makuu matano ambayo lengo lake ni kufungua mwelekeo mpya katika sekta ya madini.

“Ndiyo maana mmeona katika mazungumzo yetu hatukujikita tu katika makinikia, tungejikita katika makinikia tungeishia na malipo ya fedha tu, lakini sasa tumepata zaidi ya hayo kwa sababu Rais katika mkakati wake lengo lake lilikuwa tunaanza na makinikia, lakini tunafungua mambo mengine zaidi kuhakikisha sheria yetu inatekelezwa,” alisema Profesa Kabudi.

BILIONI 700 ZAZUA UTATA

Kabla Kabudi hajafafanua hilo, jambo jingine lililozua maswali ni namna zitakavyolipwa Sh bilioni 700 ambazo Barrick imekubali kuilipa Tanzania, hasa baada ya jana kampuni tanzu ya Acacia kutoa msimamo tofauti.

Shirika la Habari la Kimataifa la Reuters, jana lilimkariri Mkurugenzi wa Fedha wa Acacia, Andrew Wray, akisema kampuni hiyo haina uwezo wa kulipa fedha hizo.

Kauli hiyo ya Wray imekuja wakati ambako maridhiano hayo bado hayajafikishwa kwenye bodi ya Acacia kwa ajili ya uthibitisho kama ilivyotaka kupitia taarifa yao ya awali iliyotolewa juzi, baada ya hafla ya kuyasaini iliyofanyika Ikulu, Jijini Dar es Salaam mbele ya Rais Dk. John Magufuli.

Taarifa kwa umma iliyotolewa na Kampuni hiyo ya Acacia juzi ilisema bado inaendelea kusaka ufafanuzi wa kutosha kuhusu makubaliano yaliyofikiwa, kwa kuwa haijapatiwa taarifa rasmi kuhusu maridhiano hayo.

Acacia inachimba madini katika migodi mbalimbali hapa nchini ina hisa asilimia 36.1, huku kampuni mama ya Barrick ikiwa na hisa asilimia 63.9.

Kauli hiyo ya sasa ya Wray ni wazi imetoa taswira ya kuwako kwa mgongano kati yake na Barrick kuhusu kulipa fedha hizo, jambo ambalo limeibua maswali na kuacha sintofahamu.

Zitto Kabwe, mwanasiasa na mmoja wa wachambuzi mahiri wa masuala ya uchumi nchini, ameonekana kushtushwa na kauli hiyo mpya ya Acacia iliyoitoa kupitia Shirika la Reuters.

Mwanasiasa huyo, ambaye alikuwa akizungumza na Redio Deutsche Welle ya mjini Bonn, Ujerumani kuhusiana na msimamo huo mpya wa Acacia, alisema nchi ilifanya kosa kutangaza ushindi kwenye mazungumzo kati ya Serikali na Kampuni ya Barrick.

“Ni kawaida ya Barrick kutoa ahadi kama ambazo wamezitoa jana. Mwaka 2006 walitoa ahadi ya namna hiyo kwenye suala la misamaha ya kodi baada ya kuwa wamebanwa bungeni. Na wamefanya kama hivyo Chile, Ecuador na Bolivia, kwa hiyo kwangu mimi nilishangaa sana kuona kwamba tunajazwa upepo,” alisema Zitto.

Akijibu swali la Mtangazaji kuhusu kuwapo kwa taarifa mbili tofauti za makubaliano, Zitto alisema Serikali ilikuwa ikizungumza na mmiliki na si kampuni iliyofanya makosa.

“Kwenye sheria ya makampuni ni vitu viwili tofauti. Kampuni inasimama yenyewe na mmiliki anasimama mwenyewe, kwa hiyo kuanzia mwanzo kabisa niliona kuwa kuna tatizo ama tunachezewa.

“Na ndio hivyo ambavyo imetokea jana (juzi), taarifa ya Makamu wa Rais wa Barrick inaonesha kwamba watatoa kishika uchumba cha dola milioni 300 (Sh bilioni 700), hiyo hiyo jioni Acacia wakasema lazima iende kwenye bodi yao na leo tumesikia Acacia wanasema hawana uwezo wa kulipa fedha hizo. Tunachezewa shere. Haya ni makosa tuliyoyafanya kwa kutokutumia ni maarifa ya namna gani ya makampuni ya nchi za kibeberu,” alisema Zitto.

WASIFIA

Hata hivyo, mtazamo huo wa Zitto unatofautiana kwa kiasi kikubwa na wasomi wengine waliozungumza na MTANZANIA Jumamosi kuhusiana na kile ambacho Serikali imefanikiwa kuibana Kampuni ya Barrick.

Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) Idara ya Uchumi, Profesa Humphrey Moshi, alisema juhudi kubwa zimefanywa na Rais na timu yake katika kufikia mwafaka na kupata fedha hizo ambazo ni Sh bilioni 700.

“Rais alitakiwa apongezwe kwa hatua hiyo. Sifa ya Tanzania itaamsha nchi nyingine ili waone tunavyoibiwa Afrika,” alisema Profesa Moshi.

Alisema amekuwa akisafiri nje ya nchi mara kwa mara na hivi karibuni alikwa nchini China na kupokea pongezi kutoka nchi nyingine kuhusu mazungumzo yaliyokuwa yakiendelea.

“Hii kitu italeta hamasa kubwa dunia nzima, hasa kwa nchi zinazoendelea kuangalia upya sera ya madini, mikataba ya madini na kujua kuwa tulikuwa tukiibiwa. Afrika itaamka,” alisema Profesa Mosha.

Naye Mhadhiri mwingine wa UDSM, Dk. Benson Bana, alisema hatua iliyofikiwa si jambo jepesi na la kubeza, kwani isingefanikiwa bila jitihada za Rais Magufuli.

Alisema mazungumzo hayo yamezaa faida kwa nchi na kwamba fedha zilizopatikana si ndogo, kwa kuwa pia suala la kodi linaendelea kufanyiwa kazi.

Mbali na wasomi hao, Chama cha Wananchi (CUF) kilicho upande wa Mwenyekiti Profesa Ibrahim Lipumba, licha ya kupongeza, kilisema mikataba mibovu ilikuwa ni moja ya mambo waliyopigia kelele kwa miaka mingi.

Kupitia Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Mahusiano na Umma-CUF Taifa, Abdul Kambaya, alisema karibu asilimia 80 ya makubaliano hayo yanatokana na sera ya chama hicho katika chaguzi za mwaka 2000, 2005 na 2010.

ACACIA NA HASARA

Jana Acacia ilitoa taarifa ikionyesha mwenendo wa biashara yake kwa muda wa takribani miezi mitatu hadi Septemba 2017.

Imeonyesha kuwa, kampuni hiyo imezalisha wakia 191,203 za dhahabu kwa miezi mitatu ya mwanzo wa mwaka, ikiuzwa kwa dola za Marekani 939 kwa wakia.

Ikimnukuu Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Acacia, Brad Gordon, taarifa hiyo ilieleza kuwa, pamoja na changamoto zilizopo, biashara yao imeendelea kuwa imara, hasa katika mgodi wa Buzwagi, hali ilikuwa inafurahisha zaidi, ingawa vizuizi na ukosefu wa marejesho ya malipo ya VAT katika mauzo ya makinikia imetoa athari katika vitabu vyao vya hesabu.

Ripoti hiyo inadai mzunguko wa fedha wa kampuni hiyo umeshuka hadi dola za Marekani milioni 95 hadi mwisho wa mwezi Septemba.

Ili kukabiliana na hali hiyo, Gordon alisema wamechukua hatua mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kupunguza kiwango cha uendeshaji katika mgodi wa Bulyanhulu na kwamba mauzo ya dhahabu yote hadi Februari 2018 yanatarajiwa kuwa dola za Marekani 1,300 kwa wakia moja.

Maelezo mengine ni kwamba, mauzo ya dhahabu kwa kipindi chote cha miezi mitatu ni dola 171 milioni, ikiwa ni pungufu ya asilimia 40 ukilinganisha na kipindi kama hicho mwaka jana.

Katika robo mwaka iliyobaki, Acacia inatarajia kuuza kati ya wakia 8,000 na 10,000 za dhahabu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles