27.9 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Marekani yatia chumvi mgogoro Ukingo wa Magharibi

WASHINGTON, MAREKANI

UMOJA wa Ulaya umejitenga na uamuzi wa Marekani wa kubadili sera yake kuelekea ujenzi wa makazi ya walowezi unaofanywa na Israel Ukingo wa Magharibi.

Kwa upande wake, Palestina imekemea uamuzi huo wa Marekani ambayo imesema haizingatii tena kuwa ujenzi huo unakiuka sheria za kimataifa.

Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya, Federica Mogherini, alisema msimamo wa umoja huo kuhusu sera ya makazi ya Israel, hautobadilika kwa kuwa inakwenda kinyume na sheria za kimataifa.

Mogherini alisema sera hiyo ya Israel inaweka kizingiti uwezekano wa kupatikana suluhisho la mataifa mawili pamoja na amani ya kudumu katika mzozo kati ya taifa hilo na Palestina.

Matamshi yake yamekuja baada ya Marekani juzi kutangaza kuunga mkono haki ya Israel ya kujenga makazi ya Wayahudi katika eneo inalolikalia kwa nguvu la Ukingo wa Magharibi.

Tangazo lililotolewa na Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Marekani, Mike Pompeo, lilisema taifa hilo limefikia hitimisho kwamba sera ya Israel kuhusu makazi ya Walowezi haiendi kinyume na sheria za kimataifa.

Wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari mjini Washington, Pompeo alisema utawala wa Donald Trump unabadili sera ya utawala wa Barack Obama kuelekea suala la makazi ya Walowezi wa Israel.

“Hatushughulikii wala kutoa uamuzi wa mapema kuhusu hatma ya Ukingo wa Magharibi. Hilo ni kwa Waisraeli na Wapelestina kujadiliana.

“Sheria ya kimataifa hailazimishi matokeo wala haiweki kizingiti cha kisheria kwa suluhisho lililofikiwa baada ya majadiliano,” alisema Pompeo.

Kwa mujibu wa Pompeo, matamshi ya Marekani kuhusu suala la makazi ya Walowezi yamekuwa yakitofautiana.

Alisema mwaka 1978 Rais wa zamani Jimmy Carter alihitimisha kuwa ujenzi huo ni kinyume cha sheria ya kimataifa, lakini Rais Ronald Reagan alisema mwaka 1981 kuwa makazi hayo hayakiuki sheria.

Msemaji wa Rais wa Palestina, Mahmoud Abbas, alisema uamuzi wa Marekani unakiuka kabisa sheria za kimataifa.

Alisema Washington hairuhusiwi kukiuka sheria za kimataifa na haina haki ya kubariki hatua ya Israel kuendelea na mpango wake katika Ukingo wa Magharibi.

Naye Waziri wa Mambo ya Nje wa Jordan, Ayman Safadi, alionya kuwa hatua ya Marekani ya kubadili sera yake hiyo ni hatari katika kutatua kushughulikia amani ya Mashariki ya Kati.

Safadi kupitia ukurasa wake wa Twitter alisema makazi ya Israel katika eneo hilo ni kinyume na yanaondoa matumaini ya kumaliza mgogoro uliodumu muda mrefu.

Kwa uamuzi huo, Marekani imeipa kisogo sera yake ya miongo minne iliyobainisha kuwa ujenzi wa makazi katika eneo hilo unakiuka masharti ya sheria ya kimataifa.

Kadhalika tangazo hilo limefikisha idadi ya maamuzi matatu makubwa chini ya utawala wa Rais Trump ambapo Marekani imeegemea na kuipendelea Israel na kupuuza misimamo ya Palestina na mataifa ya Kiarabu.

Uamuzi huo wa Marekani ni ushindi kwa waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, anayehangaika kusalia madarakani baada ya chaguzi mbili zilizoshindwa kumwezesha kuunda Serikali.

Netanyahu aliusifu msimamo huo mpya wa Marekani ambao hata hivyo umewakasirisha Wapalestina wanaozingatia ujenzi wa makazi kwenye ardhi ya Ukingo wa Magharibi ni kinyume na sheria.

Mpatanishi Mkuu wa Palestina kwenye mazungumzo ya amani, Saeb Erekat ameitaja hatua hiyo ya Marekani kuwa inayorudisha nyuma kanuni za kimataifa za kutatua mizozo kwa njia za amani.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles