27.1 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Marekani yaiwekea vikwazo Uturuki kwa kuwashambulia Wakurdi Syria

Washington, Marekani

MAREKANI imeiwekea vikwazo Uturuki na maofisa wa Serikali ikiwa ni kujibu hatua ya nchi hiyo kuingilia kijeshi eneo la Kaskazini mwa Syria.

Makamu wa Rais, Mike Pence alisema Rais Donald Trump pia amempigia simu mwenzake wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan kutaka kufikiwa kwa makubaliano.

Pence alisema atatembelea eneo hilo haraka iwezekanavyo.

Hatua hiyo inakuja baada ya Marekani kuondoa wanajeshi wake kutoka eneo hilo, ambayo baadhi ya watu wanasema iliipatia Uturuki ishara ya kuendelea mbele na mpango wake.

Vikosi vya Marekani vimekuwa vikipambana kwa ushirikiano na wanamgambo wa Kikurdi kaskazini mwa Syria dhidi ya kundi la Islamic State (IS).

Operesheni ya Uturuki ambayo ilianza wiki iliyopita, inalenga kukabili vikosi vya pamoja vya Syria (SDF) kutoka eneo hilo la mpakani.

Uturuki inaamini SDF ni kikosi cha magaidi.

Vikosi vya Uturuki pia vimebuni kile ambacho Serikali yao inataja kuwa eneo salama la kuwapa makazi wakimbizi milioni mbili wa Syria ambao wamepewa hifadhi katika nchi hiyo.

Wengi wao sio Wakurdi na wakosoaji wanaonya kuwa hatua hiyo huenda ikasababisha jamii hiyo katika eneo hilo kulengwa kimakosa.

Wametaja hatua ya Marekani kujiondoa iliyosababisha Uturuki kuingia eneo hilo kuwa ni usaliti.

Kuna hofu kuwa hatua ya kuwahangaisha wenyeji katika eneo hilo huenda ikafufua tena kundi la IS, kwa sababu maelfu ya jamaa wa wapiganaji hao wanazuiliwa kaskazini mwa Syria.

Mamia kati yao wanadaiwa kutoroka katika moja ya kambi waliyokuwa wamehifadhiwa.

Baada ya makabiliano makali, vikosi hivyo vinavyoongozwa na Wakurdi, Jumapili vilitangaza kufikia makubaliano kati yao na Serikali ya Syria kuomba msaada wa kijeshi ili kudhibiti mashambulizi kutoka vikosi vya Uturuki.

VIKWAZO VILIVYOWEKWA

Waziri wa Fedha wa Marekani, Steven Mnuchin, alitangaza vikwazo ambavyo vililenga wizara mbili na maofisa wakuu watatu wa Serikali mjini Washington DC.

Taarifa ya Marekani ilisema hatua ilichukuliwa dhidi ya wizara za Uturuki za ulinzi na kawi, na mawaziri wa ulinzi, kawi na usalama wa ndani.

Hatua hiyo inazuia mali zao nchini Marekani na kupiga marufuku kujiuhusisha kwao na shughuli zozote zinazowahusisha wao na mfumo wa kifedha wa Marekani.

“Hatua ya Uturuki inahatarisha maisha ya raia wasiokuwa na hatia na kusababisha vurugu katika eneo hilo, ikiwa ni pamoja na kuhujumu kampeni ya kuishinda ISIS,” taarifa hiyo iliongeza.

Rais Trump anakabiliwa na shinikizo la kutaka iichukulie hatua mshirika wake katika Nato.

Katika taarifa iliyowekwa katika mtando wa Twitter, Rais Trump alisema ataongezea kodi vyama kutoka Uturuki kwa asilimia 50 na kukomesha mara moja mashauriano yanayohusiana na mkataba wa kibiashara wa dola bilioni 100 na Uturuki.

“Sisi Marekani na washirika wetu tumekomboa kwa asilimia 100 maeneo yaliyokuwa yanakaliwa na na ISIS, Uturiki haistahili kuweka hatarini hatua iliyofikiwa katika mapambano hayo,” ilisema taarifa hiyo.

Mapema Jumatatu, nchi wanachama wa Muungano wa Ulaya (EU) ziliahidi kusitisha mpango wa kuiuzia silaha Uturuki, hali ambayo huenda ikageuka kuwa vikwazo kamili vya kisilaha dhidi ya nchi hiyo.

Ikijibu tamko hilo, Uturuki ilisema itachunguza ushirikiano wake na EU kutokana na tabia yake isiyo halali na ya upendeleo.

KINACHOENDELEA SYRIA

Baada ya kufikia makubaliano na vikosi vinavyoongozwa na wapiganaji wa Kikurdi, Jeshi la Syria lilianza kufanya mashambulizi kuelekea mpakani siku ya Jumatatu.

Vyombo vya habari vya Syria vilitangaza kuwa vikosi vya Serikali vimeingia katika mji wa Manbij, eneo ambalo Uturuki inataka kubuni eneo salama.

Wanajeshi wa Uturuki na wapiganaji wanaopinga Serikali walianza kukusanyika karibu na mji huo.

Mkataba huo ulionekana kuimarisha utawala wa Rais wa Syria, Bashar al-Assad, kwani ulimaanisha vikosi vyake vitarejea katika maeneo ya kaskazini mashariki kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2012, baada ya kujiondoa kwao katika maeneo mengine ili kukabiliana na waasi kutoa nafasi kwa wanamgambo wa Kikurdi kuchukua udhibiti wa eneo hilo.

Licha ya kupinga jaribio lao la kutaka kujitenga na kujitawala, Assad hakupigania kukomboa eneo hilo, hasa baada ya wapiganaji wa Kikurdi kuwa washirika wake katika vikosi vya muungano dhidi ya IS kwa ushirikiano na vikosi vya Marekani.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles