25.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 18, 2024

Contact us: [email protected]

Marekani, Urusi zanyukana kuhusu Venezuela

WASHINGTON, MAREKANI

SERIKALI za Marekani na Urusi  zimeendelea kupambana vikali juzi kuhusiana na jinsi ya kuisaidia Venezuela iliyokumbwa na mzozo wa kisiasa, ambapo Urusi iliamua kutoa njia mpya za kutoa misaada kupitia Rais Nicolas Maduro wa Venezuela, lakini Marekani ikatangaza kuweka vikwazo vipya dhidi ya taifa hilo la Amerika Kusini.

Siku moja baada ya Urusi na  China  kupiga  kura  ya  turufu dhidi ya  azimio la  Marekani  na  Ulaya  katika  baraza  la  Usalama  la Umoja  wa  mataifa ambalo lilitaka  kufikishwa misaada bila vizuizi, Marekani  ilisema  inawalenga  maofisa  sita  wa  jeshi  la Venezuela  kwa kuzuia  msafara  ulioongozwa  na  Marekani mwishoni  mwa  wiki  iliyopita.

Watu wanne waliuawa  katika  vurumai  iliyotokea  wakati  majeshi ya Maduro  yalipozuia  tani 178  za  mchele, maharage na vyakula  vingine kutoka Marekani kuingia  nchini  humo  kupitia  Colombia. Kiongozi huyo wa  Venezuela  amesema msaada huo ni njama za uvamizi zinazoongozwa  na  Marekani.

“Tunaweka vikwazo  dhidi  ya  wanajeshi  wa  jeshi  la  usalama  la Maduro  kujibu  ghasia  za  ukandamizaji, vifo pamoja  na  hatua  ya kuchoma  moto  vyakula  na  madawa  vilivyokuwa vinapelekwa kwa  wagonjwa  na  wale  ambao  hawana  chakula  nchini Venezuela,” amesema Waziri  wa  Fedha, Steven Mnuchin, alipowasilisha taarifa ya Serikali kuhusiana na jambo hilo.

Taarifa zinasema kuwa wanajeshi sita  waliowekewa vikwazo ni  pamoja  na  Meja  Jenerali  Richard Jesus Lopez Vargas, Kamanda  wa  Jeshi  la  Ulinzi  la  Taifa. Vikwazo  hivyo vinazuia  mali  zozote  zilizoko  nchini  Marekani  na  kutoa  adhabu kwa shughuli  zote  za  kifedha  nchini  Marekani  zitakazofanywa na maofisa hao.

Marekani  pia  imeondoa  visa  kwa  maofisa  49  wa  Venezuela pamoja  na  familia  zao, wizara  ya  mambo  ya  kigeni  imesema.

Kiongozi  wa  upinzani   wa Venezuela,  Juan Guaido, ambaye Marekani  inamtambua  kuwa  rais  wa  mpito, alikuwa  na  matarajio ya  kuweza  kuingiza  shehena  ya  misaada  nchini  Venezuela, ambayo  Marekani  imeratibu  pamoja  na  Colombia  na  Brazil.

Guaido  amesema  watu 300,000  huenda  wakafa  njaa  bila  ya kuingizwa  misaada  nchini  Venezuela. Umoja  wa  mataifa  unasema Wavenezuela  milioni  2.7 wameikimbia  nchi  hiyo  tangu  mwaka 2015 wakati  taifa  hilo  lenye  uchumi  wa  kisoshalisti ulipoporomoka, kutokana  na  kupungua  kwa  mahitaji  muhimu kwa watu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles