25.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 23, 2024

Contact us: [email protected]

MAREKANI, TANZANIA KIWAKILISHI CHA ‘DUNIA’ MBILI KATI YA TATU ZINAZOKIDHANA KUHUSU ISRAEL

JOSEPH HIZA, DAR ES SALAAM


MAPEMA wiki iliyopita na wiki hii dunia imeshuhudia historia ikiwekwa kwa husiano za kidiplomasia linapokuja Taifa la Israel baada ya Tanzania na Marekani kwa nyakati hizo mbili tofauti kufungua balozi mpya katika Taifa hilo la Mashariki ya Kati.

Wakati Tanzania ikifungua ubalozi mara ya kwanza nchini humo licha ya kuwahi kushirikiana huko nyuma, Marekani si mgeni kwani ndiye mshirika namba moja wa Israel duniani.

Marekani badala yake ilikuwa ikihamisha ubalozi wake kutoka Tel Aviv, ambako Tanzania imeweka kambi kama ilivyo sehemu kubwa ya dunia kwenda Yerusalem, mji wenye utata.

Ufunguzi wa ubalozi huo wa Marekani katika mji huo juzi Jumatatu, ni utimilizo wa ahadi ya kampeni ya Rais Donald Trump mwaka 2016 ya kuutambua mji huo mtakatifu kuwa mkuu wa Israeli.

Wakati hilo likitokea, mapema siku hiyo kwa upande wa Palestina katika Ukanda wa Gaza mpakani na Israel, vurugu na huzuni zilitawala baada ya Wapalestina zaidi ya 50 kuuawa na majeshi ya Israel katika mfululizo wa maandamano, ambayo Wapalestina wameyaita “Maandamano Makubwa ya Urejeshaji.’

Ni maandamano yanayokumbushia madhila ya Wapalestina kwa miaka 70 tangu lilipoundwa Taifa la Israel kwa gharama ya damu na ardhi yao.

Kitendo cha Marekani kuutambua mji huo unaozozaniwa na pande hizo mbili kuwa mkuu wa Israel kiliwaghadhibisha Wapalestina, waliosema Taifa hilo limepoteza sifa ya kuwa mpatanishi wa kuaminika wa mchakato wowote ule wa amani baina yao na Israel.

Mbali ya kuwakasirisha Wapalestina na mataifa ya Kiarabu uamuzi huo umelaaniwa duniani kote.

Marais wote waliotangulia wa Marekani wakifahamu unyeti wa suala hilo kwa upatikanaji wa amani ya Mashariki ya Kati pamoja na karibu kila nchi waliepuka kufungua balozi Yerusalem.

Walisisitiza hawatakuwa na shida iwapo tu hadhi ya mji huo itatatuliwa kupitia majadiliano baina ya Israeli-Palestina.

Wapalestina wamekuwa wakitaka Yerusalem Mashariki kuwa mji mkuu wa Taifa lao lijalo litakalohusisha Ukingo wa Magharibi na Ukanda wa Gaza.

Lakini Israel inauhesabu mji wote huo ikiwamo eneo hilo la Mashariki ililolitwaa mwaka 1967 wakati wa Vita ya Mashariki ya Kati kama mji wake mkuu wa milele na usiogawanyika.

Tangu kuanzishwa kwa Taifa la Israel mwaka 1948, Marekani na mataifa mengine mengi kupitia Umoja wa Mataifa (UN) hazikutambua umiliki wa Taifa lolote kwa mji huo mtakatifu kwa Wayahudi, Waislamu na Wakristo.

Lakini Israel imejenga mamia ya makazi Mashariki mwa Yerusalem kukiwa na Wayahudi 200,000 wanaoishi, licha ya Baraza la Usalama la UN kulihesabu eneo hilo kuwa sehemu ya Palestina.

Kwa sababu hiyo mataifa mengi kama ilivyokuwa Marekani kabla ya uamuzi tatanishi wa Trump zimeweka balozi zao badala yake mjini Tel Aviv ili kuepuka kusababisha machafuko.

Kwa mujibu wa maafikiano wakati wa mazungumzo ya amani baina ya Wapalestina na Waisraeli mwaka 1993, hatima ya mji huo iliafikiwa itaamuliwa katika hatua za mwisho za mazungumzo ya amani kutokana na unyeti wake.

Ikumbukwe mji huu huwa na umuhimu mkubwa kwa dini tatu kuu; Ukristo, Uislamu na Uyahudi.

Dini zote hizo humuangazia Abraham anayetajwa kwenye Biblia na Koran kama mmoja wa waanzilishi au mababu wa imani.

Hivyo ni mji ambao umedhibitiwa na dini hizo kwa vipindi mbalimbali katika historia.

Kwa Kiebrania, ukifahamika kama Yerushalayim, kwa Kiarabu kama al-Quds na Kiswahili Yerusalemu, ni miongoni mwa miji ya kale zaidi iliyopo bado duniani.

Ni mji ambao umetekwa, ukabomolewa na kuangamizwa na kisha kujengwa tena mara nyingi. Na kila sehemu ya ardhi yake unapoichimba kwenda chini hufichua enzi fulani katika historia yake.

Ingawa umekuwa chanzo cha ubishi na mzozano kati ya dini mbalimbali, dini zote huungana na kukubaliana pamoja kuwa ni eneo takatifu.

Ndani yake kuna Mji Mkongwe, ambao una njia nyembamba, vichochoro na nyumba za kale na maeneo manne makuu, ambapo kila eneo, majengo huwa tofauti; kukiwa na eneo la Wakristo, Waislamu, Wayahudi na Waarmenia.

Eneo hilo huzungukwa na ukuta mkubwa wa mawe, ambapo kunapatikana baadhi ya maeneo yanayoaminika kuwa matakatifu zaidi duniani.

Yote hayo yanaonesha jinsi gani mji huo ulivyo nyeti na unaohitaji busara kubwa kufikia mwafaka, tofauti na uamuzi wa upande mmoja wa Marekani.

Madai kuwa uamuzi wake una maslahi ya pande zote tatu; Marekani, Israel na Palestina, si ya kweli bali.

Ni wazi uamuzi wa Trump umelenga zaidi kuwafurahisha wafuasi wake na Israel kwa gharama ya Wapalestina, ambao wameendesha mlolongo wa maandamano yaliyogharimu damu ya wapendwa wao wengi.

Kwanini Trump kachukua uamuzi huo? Kumekuwapo shinikizo la muda mrefu kutoka kwa wanasiasa wanaoiunga mkono Israel mjini Washington, wakitaka ihamishe ubalozi mjini Yerusalem na hivyo Trump alilidaka hilo kuwa moja ya ahadi zake zitakazompatia kura wakati wa kampeni ya urais 2016.

Uamuzi huo unapendwa zaidi na wahafidhina wengi pamoja na Wakristo wa kiinjili waliompigia kura, ambao wengi wanaounga mkono utambuzi huo wa Yerusalem kwa kile kinachoonekana sababu za kihistoria na kidini.

Trump alichukua uamuzi huo chini ya Sheria ya mwaka 1995, inayoitaka Marekani kuhamishia ubalozi Yerusalem, lakini ambayo marais wengine wote waliomtangulia wakiwamo Bill Clinton, George W. Bush na Barack Obama waliikwepa wakifahamu athari zake.

Hivyo  ujio wa Trump kama Rais wa Marekani umekuwa zawadi kwa wafuasi wake na Israel, wakitetea kuwa kuutambua rasmi Yerusalem kama mji mkuu wa Israeli ni njia ya kuelekea makubaliano ya amani.

Akiachana na sera ya kigeni ya Marekani ya miongo saba, Desemba mwaka jana, Trump alisema: “Tunataka makubaliano, ambayo yana manufaa kwa Waisrael na Wapalestina. Marekani itaunga mkono suluhu ya mataifa mawili iwapo itakubaliwa kwa pande zote.”

Naye Waziri Mkuu wa Israeli Benjamin Netanyahu alizitaka nchi nyingine zifuate mfano huo wa Marekani akidai ni kitu sahihi”.

Akihutubia wageni katika Wizara ya Mambo ya Nje siku moja kabla ya ufunguzi wa ubalozi huo, Netanyahu alisema: “Hamisheni balozi zenu Yerusalem kwa kuwa ni kichocheo cha amani na kwa vile hamuwezi kuifikia amani kwa msingi wa kujidanganya ukweli huu.

Lakini sehemu kubwa ya dunia ikiwamo mshirika wake Umoja wa Ulaya (EU), haikubaliani naye kwa msingi kwamba haiwezi kuwa kichocheo cha amani bali machafuko.

Hata hivyo, yapo mataifa yaliyoungana na Marekani kuunda kundi linaloiunga mkono Israel kwa kila kitu yakiwamo manne wanachama wa EU; Austria, Jamhuri ya Czech, Romania na Hungary ambazo zilihudhuria sherehe hizo.

Kati ya nchi 86 zenye ubalozi nchini Israel zilizokaribishwa ni 33 tu zilizothibitisha kuhudhuria tukio hilo.

Tanzania iliyofungua ubalozi mjini Tel Aviz wiki iliyopita iko kundi linalopinga kuhamia Yerusalem.

Itakumbukwa mwishoni mwa mwaka jana, Tanzania ilikuwa miongoni mwa mataifa zaidi ya 120 lakini pekee Afrika Mashariki yaliyopiga kura UN kupinga uamuzi huo wa Trump licha ya vitisho alivyotoa.

Na kupitia Serikali juzi, ilisisitiza haitabadilisha uamuzi wa kufungua ubalozi katika Mji wa Yerusalem badala ya Tel Aviv.

Akizungumza Dar es Salaam juzi, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk. Augustine Mahiga alisema kuhamisha ubalozi Yerusalem ni kwenda kinyume na makubaliano ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lililosema kuwa mji huo bado una migogoro.

“Nchi zote za Afrika na duniani balozi zake zipo katika Mji wa Tel Aviv isipokuwa Marekani. Hivyo na sisi hatuwezi kubadilisha ubalozi wetu kwa sababu tutakuwa tunakiuka makubaliano ya UN,” alisema Dk. Mahiga.

Hata hivyo, Mahiga alisifu kuwapo ushirikiano mzuri na Israel, akisema ujio wa wataalamu kutoka Israel katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), umeokoa Sh. bilioni 70 ambazo zingetumika kuwapeleka wagonjwa wenye matatizo ya moyo nchini India.

Kwa mujibu wa Dk. Mahiga wataalamu hao walifika nchini kwa vipindi tofauti na kwenda kufanya kazi katika taasisi hiyo.

Alisema katika kipindi cha miaka miwili iliyopita zaidi ya wagonjwa 2,440 wamefanyiwa opareshini ya magonjwa ya moyo hapa nchini na wataalamu hao wakishirikiana na wa hapa nchini.

Aidha alisema Serikali ya Israel imeahidi kutoa nafasi za kuwasomesha Watanzania katika masuala ya udaktari na kuiboresha JKCI ili iwe hospitali bora na kubwa katika nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara.

Katika hatua nyingine, alisema Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, anatarajia kuja nchini mwakani akiambatana na ujumbe wa wawekezaji walioahidi kuwekeza katika sekta zote zilizopo.

Msimamo huo wa Tanzania kuhusu Israel unafanana na mataifa mengine mengi yanayoshirikiana na Israel katika nyanja mbalimbali lakini yakitofautiana nayo linapokuja suala la uhusiano wake na Palestina.

Hata hivyo, awali Tanzania haikuwa katika kundi hilo linaloshirikiana na Israel na kutofautiana nayo kuhusu Palestina. Ilikuwa katika kundi la tatu la mataifa yasiyositisha uhusiano na Israel ambayo mengi yamebakia kuwa ya Kiarabu.

Katika miaka ya 1960, uhusiano baina ya Afrika ikiwamo Tanzania na Israeli ulikuwa mzuri na Israel ilikuwa na balozi 32 katika mataifa mbalimbali ya Afrika.

Hata hivyo, haraka haraka mambo yakageuka kuwa chungu kufuatia Vita ya Siku Sita mwaka 1967 na ile ya Yom Kippur mwaka 1973 baina ya Israel na ushirika wa Mataifa ya Kiarabu.

Katika kipindi hicho, uliokuwa Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU) ukichagizwa zaidi na Misri iliyokuwa sehemu ya ushirika huo, uliziagiza nchi wanachama kuvunja uhusiano wa kidiplomasia na Taifa hilo.

Mataifa yote kasoro Malawi, Lesotho na Swaziland yalitii agizo hilo, ingawa baadhi yalivunja uhusiano kwa shingo upande ukiachia mataifa kama Tanzania yaliyofanya kwa dhati.

Chini ya Mwalimu Julius Nyerere, Tanzania ilikuwa miongoni mwa mataifa yaliyokuwa na msimamo mkali dhidi ya Israel kipindi, ambacho ilikuwa kitovu cha harakati za mstari wa mbele ukombozi wa Kusini mwa Afrika.

Mbali ya uhusiano huo mchungu kuchochewa na matendo yake kwa Palestina, Israel iliendekeza uhusiano na utawala wa makaburu wa Afrika Kusini, ambao walikuwa walengwa wakuu wa harakati za mstari wa mbele zilizokuwa zikiendekezwa na Tanzania.

Msimamo huo dhidi ya Israel ulibakia hivyo hadi katika miaka ya 1990 wakati mataifa mengi ya Afrika yalipoanza kurejesha uhusiano.

Nguvu msukumo iliyo nyuma ya mataifa ya Afrika ikiwamo Tanzania kulegeza misimamo yao kwa Israel kwa kiasi kikubwa imelenga maslahi ya kibiashara, afya na kijeshi.

Lakini bado kuna mataifa ikiwamo ya Afrika yaliyobakia katika msimamo wa kundi la tatu, ambayo hayachangamani bado na Israel kwa namna inavyoishi na Wapalestina.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles