24.4 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Marcio Maximo atua kwa kishindo Dar

Maximo
Kocha mpya wa klabu ya Yanga ya Dar es Salaam, Marcio Maximo

NA KAMBI MBWANA, DAR ES SALAAM

HATIMAYE Kocha wa zamani wa timu ya Taifa (Taifa Stars), Marcio Maximo ametua nchini jana kwa mbwembwe na kulakiwa na wanachama kadhaa wa Yanga waliofika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere, kushuhudia kocha huyo akiwasili nchini.

Maximo aliyeonekana mwenye furaha, hakuweza kuzungumza lolote alipowasili na kuahidi kuzungumza leo suala lililomleta.

“Nashukuru sana kupokewa kwa shangwe na Watanzania, ila kilichonileta naomba nikiseme kesho rasmi.

“Najua kuna mengi watu wanataka kujua hasa hatima yangu Yanga, ila wasiwe na haraka kwasababu ndio kwanza nimeingia muda huu nikitokea Brazil,” alisema.

Wakati Maximo anazungumza ndani ya uzio wa geti la kutokea la VIP, watu walikuwa wakiimba kwa shangwe na kulitaja jina lake kiasi cha kumfanya apate faraja kubwa.

Ujio wa kocha huyo ulisubiriwa kwa hamu na wapenzi wa Yanga, kwa ajili ya kuingia makubaliano na uongozi wa klabu ya Yanga kuifundisha timu hiyo, huu ni ujio wa pili baada ya awali kuja kama kocha wa timu ya Taifa ‘Taifa Stars’ na kuipatia mafanikio makubwa.

Maximo alipokanyaga kwa mara ya kwanza ardhi ya Tanzania mwaka 2006, alisema kuwa Watanzania wasitegemee miujiza kutoka kwake kwani yeye ni binadamu kama wengine.

“Msitegemee miujiza kutoka kwangu, ila juhudi za pamoja kati yangu na Watanzania ndio zitatufikisha mbali,” alisema.

Kauli hiyo ya Maximo ilithibitika baada ya kuinua soka la Tanzania, pia kuifanya timu ya Taifa iheshimike na mataifa makubwa katika soka, kwani aliweza kuitikisa vilivyo miamba hiyo.

Kocha huyo kipenzi cha Watanzania, aliwasili saa tisa alasiri akiambatana na kocha msaidizi wake, Leonardo Neiva, huku mchezaji Countinho akielezwa kuja baadaye.

Kabla ya kuwasili kocha huyo uwanja wa ndege haukuonyesha tofauti yoyote kwamba siku hiyo kungeingia kocha mkubwa anayeheshimika kwa kiasi kikubwa Tanzania.

Hata hivyo kadri muda ulivyozidi kusonga mbele, mabadiliko yalianza kuonekana hasa kwa kuanza kuonekana baadhi ya wanachama na wafuasi wa Yanga.

Nusu saa baadaye, Katibu Mkuu wa Yanga, Beno Njovu na Baraka Kizuguto waliwasili uwanjani hapo kwa ajili ya kumpokea kocha huyo, huku kwa ushirikiano na walinzi wa Uwanja wa Ndege walikuwa wakipanga mbinu na namna ya kumtoa uwanjani hapo.

Baada ya kutoka nje, Maximo alipanda kwenye gari lenye namba za usajili T AUZ 390 na kuanza msafara wa kuelekea Makao Makuu ya klabu ya Yanga, Jangwani, jijini Dar es Salaam.

Baada ya kufika klabuni, Njovu alianza kumtembeza kocha huyo katika ofisi za jengo hilo sambamba na kumuonyesha hali ya uwanja wa klabu hiyo.

Kocha huyo anayekumbukwa kwa kuliwekea mazingira mazuri soka la Tanzania, alipanda juu ya jengo hilo na kuanza kuangalia mazingira ya Makao Makuu ya Yanga.

Hata hivyo watani wao wa jadi Simba, walionekana kuwa kimya baada ya picha za kuwasili kocha huyo kuanza kuonekana katika mitandao ya kijamii, mashabiki hao walionekana kuwa kimya tofauti na walivyokuwa wakiubeza ujio huo.

Ujio wa kocha huyo ulianza kushika kasi baada ya mwenyekiti wao, Yusuf Manji, kutangaza katika mkutano wa wanachama kuwa anakuja kuifundisha Yanga.

Hata hivyo taratibu zote za ajira ya Maximo akiwa na msaidizi wake zitajulikana rasmi leo baada ya kukutana na waandishi wa habari wa michezo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles