24.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Marais EAC kuamua hatima ya Nkurunziza

Burundi's President Pierre NkurunzizaNa Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
WAKUU wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) wanatarajia kukutana Dar es Saalam Mei 13 mwaka huu, katika mkutano wa dharura utakaoamua hatima ya Rais Pierre Nkurunziza wa Burundi.
Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa jana, ilieleza kuwa hatua hiyo imechukuliwa wiki chache baada ya amani kuchafuka nchini Burundi kutokana na chama tawala cha CNDD-FDD kumteua Rais Nkurunziza kuwania nafasi hiyo kwa muhula wa tatu kinyume cha Katiba ya nchi hiyo.
“Lengo kuu la mkutano huo utakaofanyika Dar es Salaam ni kujadili hali ya amani wakati wa kuelekea kipindi cha uchaguzi nchini Burundi,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo. hiyo
Taarifa hiyo pia ilizungumzia ziara iliyofanywa na mawaziri wa mambo ya nje wa EAC nchini Burundi wakiongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, kujadili hali ya maendeleo ya siasa nchini humo.
“Wakiwa nchini humo, mawaziri hao walikutana na kuwa na mazungumzo na Rais Pierre Nkurunziza, viongozi na wawakilishi wa vyama 45 vya siasa vya upinzani nchini humo mazungumzo yaliyodumu kwa takriban saa moja na nusu.
“Mawaziri hao walifikisha mwaliko kutoka kwa Rais Kikwete kumwalika Nkurunziza kuhudhuria mkutano huo wa dharura wa wakuu wa nchi,” ilisema taarifa hiyo.
Taarifa hiyo ilieleza kuwa Membe akiwa kwenye mazungumzo hayo alimuomba Rais Nkurunziza na viongozi wa vyama vya siasa nchini humo kutoa maelezo na maoni yao kwa jopo hilo kwa uwazi na kupendekeza jinsi viongozi wa EAC watakavyoweza kuisaidia Burundi.
“Pande zote mbili zilizoshiriki kwenye mazungumzo hayo na jopo la mawaziri kwa nyakati tofauti walieleza kufurahishwa kwao na hatua ya Rais Kikwete kuitisha kikao hicho cha dharura kujadili suala la Burundi kwa wakati muafaka.
“Wakati mazungumzo hayo yakiendelea wakimbizi wapatao 28,000 wameikimbia nchi hiyo kuingia Rwanda na Tanzania ambako wengi wao wameingia Rwanda.
“Hili ni janga la binadamu ambalo ni lazima jumuiya yetu chini ya uenyekiti wa Rais Kikwete kulipatia ufumbuzi kwa haraka,” ilisema taarifa hiyo.
Waandamanaji wauawa
Wakati huohuo, mtu mmoja ameuawa na wengine tisa kujeruhiwa mjini Bujumbura jana wakati wa vurugu zilizozuka upya kati ya waandamanaji na polisi.
Shirika la Msalaba Mwekundu limesema watu wote waliouawa na kujeruhiwa ni raia.
Watu walioshuhudia waliliambia Shirika la Habari la Ufaransa (AFP) kuwa kundi dogo la waandamanaji lilikabiliana na wafuasi wa rais wanaoshukiwa kuwa wanamgambo wa CNDD-FDD katika Wilaya ya Kinama mjini Bujumbura.
Juzi, Rais Nkurunziza alisema katika hotuba yake kuwa muhula wake ujao utakuwa wa mwisho ikiwa atachaguliwa.
Aliyasema hayo baada ya Mahakama ya Katiba kutoa uamuzi kuwa anaweza kuwania tena muhula mwingine kwa vile muhula wake wa kwanza alipochaguliwa na Bunge badala ya wananchi, hauhesabiki kwa mujibu wa katiba.
Alitoa wito wa kusimamishwa maandamano hayo ambayo hadi sasa yamesababisha vifo vya watu 14 na wengine maelfu kuikimbia nchi hiyo, ili maandalizi ya uchaguzi wa Juni 26 yafanyike katika mazingira ya utulivu.
Habari nyingine zinasema Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AU), Nkosazana Dlamini Zuma amesema Burundi inapaswa ifikirie kuahirisha uchaguzi uliopangwa kufanyika Mei na Juni mwaka huu hadi makubaliano yatakayohakikisha utulivu wa siasa yatakapofikiwa.
Zuma alikiambia Kituo cha Televisheni cha CCTV mjini Addis Ababa, Ethiopia kwamba hali ya Burundi haiwezi kuruhusu kufanyika uchaguzi muafaka na katika utulivu.
“Aina gani ya uchaguzi inatarajia kufanyika katika hali hii? Kama AU tumepanga kutuma waangalizi kwa kipindi kirefu lakini hatuwezi kwa sasa. Hatuwezi, kwa sababu mazingira hayafai kuendesha uchaguzi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles