24.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Mapya yafichuka mfanyabiashara aliyeuawa Kenya

NAIROBI, KENYA

WAKATI polisi wakiimarisha msako wa mtu ambaye hajafahamika, aliyeambatana na mshukiwa mkuu wa mauaji Joseph Irungu karibu na eneo ambalo mfanyabiashara Monica Kimani aliuawa, mapya yameibuka kuhusu marehemu huyo.

Ndugu na jamaa wa marehemu wanadai kuwa Kimani alikuwa ameolewa na mwanasiasa na bwana vita wa zamani wa Sudan Kusini, Daniel Awet Akot.

Hata hivyo, baba wa marehemu, Paul Ngarama amepuuza madai hayo, lakini akikiri Akot alikuwa karibu na familia yake.

Ndugu wa karibu na marafiki walidai Kimani aliolewa na Akot, na kupitia uhusiano huu hali ya familia yao ikaimarika kwa kipindi cha miaka mitatu iliyopita.

Kimani aliuawa kwa kukatwa koo katika bafu la makazi yake ya Kilimani jijini hapa usiku wa Septemba 19, mwaka huu mauaji yaliyomweka matatani mtangazaji maarufu wa televisheni ya Citizen, Jacque Maribe.

Maribe anashukiwa kufahamu na hivyo kuficha uhalifu huo, ambao mshukiwa mkuu ni rafiki yake wa kiume Irungu na jirani Brian Kassaine.

Wote watatu wanashikiliwa wakati polisi wakijaribu kupata jawabu juu ya kilichotokea usiku wa mauaji na ukweli wa utetezi uliotolewa na Maribe.

Ngarama ambaye alikuwa mchuuzi wa magazeti mjini Juba mwaka 2013, alisema Akot, ambaye alipanda ngazi kufikia Uluteni Jenerali katika Jeshi la Ukombozi wa Watu wa Sudan (SPLA) na mkongwe wa vita, alimsaidia kuanzisha makanisa huko Rumbek, Juba na sehemu nyingine za Sudan Kusini.

Vyanzo vya habari vimedai kuwa Ngarama alihamia Sudan Kusini mwaka 2007 kuuza magazeti ya Kenya na kuondokea kuwa maarufu miongoni mwa Wakenya waishio huko.

“Alikuwa akigawa magazeti kwa baiskeli na alikuwa mcheshi na rafiki wa kila mtu huku akiishi maisha ya kawaida,” alisema mtu anayeifahamu familia, lakini aliyeomba kuhifadhiwa.

Alisema Ngarama baadaye alihamia Rumbek na akawa karibu na Gavana wa Bahr el Ghazal, Awet Akot, ambaye aliondokea kujenga imani kwake.

Mwaka 2013, ikiwa ni mwaka mmoja tu baada ya Kimani kuhitimu kutoka Chuo cha Polytechnic, vyanzo vya habari vinasema Ngarama alimkaribisha bintiye huyo Rumbek, ambako alipata kazi katika ofisi ya gavana.

“Gavana aliondokea kumpenda na daima waliambatana kila mahali na hivyo akapanda vyeo haraka ofisini mwake.

“Baadaye Ngarama alianzisha Kanisa la Apostolic Faith Mission na kufungua tawi jingine kwa msaada wa gavana,” alisema na kuongeza kuwa kanisa hilo kwa sasa lina matawi kote Afrika Mashariki.

Akot, kwa mujibu wa taarifa za mtandanoni alipata mafunzo ya kijeshi Sudan Kusini na Marekani.

Aliongoza waasi wa SPLA eneo la Renk kaskazini mwa Sudan Kusini.

Kiongozi wa waasi, marehemu John Garang ambaye alikuwa rafiki yake, alimteua kuwa mmoja wa viongozi 11 wa kamandi ya siasa na kijeshi ya SPLA na kumfanya kuwa mmoja wa makamanda wa kijeshi wenye nguvu zaidi.

Wakati Luteni Jenerali (mstaafu) Akot alipokuwa Naibu Spika wa Bunge la Taifa la Sudan Kusini, alihamia Juba na familia yake.

Alihamia na Kimani, ambaye wakati huo hakuwa akifanya kazi katika ofisi yake bali akipanua biashara ya familia mjini Juba.

“Biashara ya familia inahusisha huduma za usafirishaji vifurushi baina ya Kenya na Sudan, lakini Kimani alianza kujihusisha na bidhaa za urembo hasa kutoka Kenya na Uganda.

“Taratib, biashara ilikuwa na kisha akaanzisha ubunifu wake mwenyewe mwaka 2017 na kupata mikataba kutoka ofisi za Serikali na taasisi binafsi shukrani zikienda kwa uhusiano wake na Akot,” alisema rafiki wa familia.

Ndani ya miaka miwili tu Kimani alikuwa amenunua miliki Nairobi, Ruiru na Syokimau. Pia alimnunulia mama yake gari na aliagiza jingine kwa ajili ya baba yake.

“Alikuwa akisafiri kuja Kenya mara mbili kwa mwezi kwa sababu alikuwa na makazi Nairobi, na pia kuangalia miliki za Akot jijini Nairobi zilizopo maeneo ya Kilimani na Kileleshwa,” alisema mwanafamilia mwingine.

Marafiki zake mjini Juba wanaamini Kimani huenda alisafiri Kenya Jumatano ya Septamba 19 akiwa na kiasi kikubwa cha fedha kwa sababu benki za Kenya ziendeshazo shughuli Juba kwa kawaida huchukua muda kuruhusu uhamishaji fedha.

Chanzo kilidai kuwa pamoja na sheria kali zinazodhibiti uvushaji wa fedha kutoka nchi hiyo, Akot alitumia ushawishi wake kumwezesha asafiri na fedha.

Lakini polisi walisema hawajaona fedha zozote katika makazi yake wala katika nyumba ya Maribe.

Kimani aliuawa Jumatano ya Septemba 19 akikatwa koo kitaalamu na kuachwa chumbani katika makazi yake ya Kilimani, Nairobi.

Kaka yake George Thiru, aliukuta mwili wake asubuhi ya siku iliyofuata baada ya kumkosa kwa mawasiliano ya simu na kushindwa kutokea Uwanja wa Ndege wa Jomo Kenyatta, alikokuwa aelekee Dubai kwa mapumziko.

Polisi wanaamini Kassaine na Irungu walikuwa na ugomvi kabla ya Irungu kujipiga risasi kifuani.

Awali akishirikiana na mpenzie Maribe, walidai kupigwa na wahuni waliokuwa katika pikipiki kabla hawajabadili kauli hiyo.

Polisi wanaamini Irungu na Kassaine walikuwa pamoja usiku ambao Kimani aliuawa kutokana na ushahidi wa vitu mbalimbali ikiwamo vilivyokutwa katika gari la Maribe.

Aidha imeelezwa marehemu Kimani na washukiwa wa mauaji yake Irungu na Kassaine walisoma pamoja katika Chuo cha Polytechnic na walikuwa marafiki na walikuwa walikutana na Maribe mara kadhaa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles