24.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

MAPYA YAFICHUKA AJALI ILIYOUA WANAFUNZI 33 ARUSHA

ELIYA MBONEA na JANETH MUSHI

-ARUSHA

SIRI mpya ya ajali iliyotokea wiki iliyopita na kusababisha vifo vya wanafunzi 33 wa darasa la saba katika Shule ya Msingi ya Lucky Vincent, walimu wao wawili na dereva mmoja wa basi, imefichuka baada ya mmiliki wake, Innocent Mushi, kufikishwa mahakamani.

Mushi alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha jana na kutuhumiwa kutenda makosa manne ya usalama barabarani, yanayodaiwa kusababisha ajali hiyo iliyotokea Mei 6, mwaka huu, baada ya basi walilopanda wanafunzi na walimu wao kutumbukia kwenye korongo lililopo Marera, eneo la Rotia, Wilaya ya Karatu, mkoani Arusha.

Mushi na mtuhumiwa mwenzake, ambaye ni Mwalimu Mkuu Msaidizi wa shule hiyo, Longino Nkana, walifunguliwa kesi na 78 ya mwaka huu na wanatuhumiwa kwa makosa hayo, likiwamo la kusafirisha watoto bila kuwa na vibali muhimu.

Akiwasomea mashitaka yao mjini hapa mbele ya Hakimu Mkazi Desdery Kamugisha, Wakili wa Serikali, Rose Sule, alidai Mushi, ambaye ni mtuhumiwa wa kwanza, anakabiliwa na makosa manne, wakati Nkana akituhumiwa kwa kosa moja.

Sule alidai kwamba, Mushi akiwa mkurugenzi wa shule hiyo anatuhumiwa kumiliki gari la abiria bila kuwa na leseni ya usafirishaji.

Alidai kuwa Mei 6, mwaka huu, katika eneo la Kwamrombo, wilayani Arusha, mtuhumiwa huyo alifanya shughuli ya usafirishaji wa abiria akiwa anamiliki gari aina ya Mitsubishi Rossa, lenye namba za usajili T871 BYS.

Aliendelea kudai mahakamani hapo kuwa kosa la pili linalomkabili ni la kuruhusu kuendeshwa kwa gari bila kuwa na bima (road license) ambapo Mei 6, mwaka huu, aliruhusu gari hilo kuendeshwa huku akijua halina bima.

“Kosa la tatu ni kushindwa kuingia mkataba na mwajiri wake, ambapo Mei 6, mwaka huu, ukiwa mmiliki wa gari hilo ulishindwa kuingia mkataba wa ajira na dereva wako, Dismas Gasper, ambaye kwa sasa ni marehemu,” alidai Sule, alipokuwa akisoma mashitaka na kuongeza:

“Mtuhumiwa unakabiliwa na kosa la nne ambalo ni la kubeba abiria waliozidi zaidi ya 13 ambapo Mei 6, mwaka huu ukiwa mkurugenzi, ofisa msafirishaji na mmiliki wa Lucky Vincent, ulibeba na kusafirisha abiria zaidi ya 13, kinyume cha sheria.”

Akisoma mashitaka kwa mtuhumiwa wa pili, Sule alidai mahakamani hapo kuwa, Nkana anadaiwa kuandaa safari iliyozidi abiria 13, huku akijua ni kinyume cha sheria.

Alidai kuwa Mei 6, mwaka huu, mtuhumiwa huyo akiwa na nafasi ya mwalimu mkuu msaidizi wa shule hiyo na mwandaaji wa safari aliruhusu kupakia abiria zaidi ya 13 katika gari lililosababisha vifo vya watu.

Kwa upande wake, Wakili Method Kimomogolo, anayewawakilisha watuhumiwa mahakamani hapo, aliiomba mahakama hiyo kuwapa dhamana wateja wake na Sule hakuwa na pingamizi dhidi ya ombi hilo.

Akitoa masharti baada ya kuzisikiliza pande zote mbili, Hakimu Kamugisha alisema washtakiwa hao watatakiwa kuwa na wadhamini wawili kila mmoja watakaotakiwa kutimiza masharti.

“Mnatakiwa kuwa na wadhamini wawili kila mmoja watakaosaini dhamana ya shilingi milioni 15. Watuhumiwa mtatakiwa kuwasilisha hati zenu za kusafiria, lakini pia hamtakiwi kuondoka nchini na ndani ya mkoa bila ruhusa ya mahakama,” alisema Kamugisha.

Watuhumiwa wote wawili walifanikiwa kutimiza masharti yaliyotolewa na mahakama hiyo na kesi hiyo sasa itatajwa Juni 8, mwaka huu.

RAMBIRAMBI

Katika hatua nyingine, zaidi ya Sh milioni 200 zimepatikana kutoka kwa wadau mbalimbali wanaoendelea kuchangia  rambirambi kwa familia za wanafunzi hao wa

Shule ya Lucky Vincent waliopoteza maisha kwenye ajali ya basi iliyotokea wiki iliyopita.

Akitoa taarifa hiyo kwa waandishi wa habari ofisini kwake jana, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo, alisema hadi sasa wamepokea kiasi cha Sh milioni 215 kutoka kwa wadau mbalimbali, ikiwamo Bunge la Tanzania.

Gambo aliwataja wadau wengine kuwa ni Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Wizara ya Elimu Zanzibar, mifuko mbalimbali ya hifadhi ya jamii pamoja na wadau wengine.

Alisema hadi sasa zaidi ya Sh milioni 190 zimetumika, ikiwamo Sh 3,850,000 kwa familia 32 zilizopoteza watoto wao katika ajali hiyo, gharama za mazishi, ikiwamo magari na usafiri kwa ajili ya maziko yaliyofanyika katika mikoa ya Arusha, Iringa, Tanga, Mbeya na Kilimanjaro.

“Tumeendelea kupokea michango kutoka kwa wadau mbalimbali na tunatarajia kuendelea kutoa mchanganuo wa fedha hizo na kukabidhi barua na vyeti vya shukrani kwa wale wote waliochangia na kiasi cha fedha walizochangia zitaandikwa katika barua na vyeti hivyo,” alisema Gambo.

NYALANDU

Akizungumzia kukamilika kwa baadhi ya hatua ya safari ya wanafunzi watatu ambao ni majeruhi watatu wa ajali hiyo, Mbunge wa Singida Kaskazini (CCM), Lazaro Nyalandu, alisema mchakato wa viza ukishakamilika, watoto hao wanatarajiwa kusafiri kesho (Jumapili).

Shirika la Mfuko wa Msamaria la Marekani linaloendeshwa na Frankline Graham, mtoto wa mhibiri maarufu duniani, Bill Graham, limetoa ndege kubwa kwa ajili ya kubeba wanafunzi hao ambapo ndege hiyo aina ya DC 8 iliruka usiku wa juzi katika Uwanja wa Ndege wa Charlotte, uliopo Jimbo la North Carolina, Marekani na kutarajiwa kutua Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA).

Kwa mujibu wa Nyalandu, ndege hiyo inatarajiwa kuwasili KIA leo jioni na mchakato wa viza utakapokamilika Gambo ndiye anatarajiwa kuongoza viongozi wa dini na wengine wa Serikali mkoani hapa kuwasindikiza majeruhi hao na wazazi wao hadi KIA kwa ajili ya safari hiyo ya kesho.

Pia alisema Kampuni ya Utalii ya Thomson imegharamia gharama za ndege kwa wazazi watatu wa watoto hao, huku Hoteli ya Serena ya Dar es Salaam ikijitolea malazi kwa wazazi hao wanaofuatilia viza jijini humo.

Watoto hao wanatarajiwa kupatiwa matibabu katika Hospital ya Mecry, iliyopo Marekani, ikiwa ni moja kati ya hospitali 30 bora nchini humo.

Naye Mwakilishi wa Shirika la Samaritan, Ed Morrow, alisema ajali hiyo imegusa mioyo ya watu wengi duniani kote, ndiyo maana walipoombwa kusaidia kusafirisha watoto hao walikubali ombi hilo.

Alisema shirika lao linasaidia jamii yote bila kubagua dini wala rangi na kuwa watoto hao watapatiwa huduma hiyo ya matibabu kwa ubora na uangalizi wa hali ya juu.

“Tunasaidia jamii bila kuangalia dini wala rangi na ndiyo maana tumeamua kuwasaidia watoto hawa kwa sababu hakuna anayejua, labda mmoja wao anaweza kuja kuwa rais au daktari na akaweza kuokoa maisha ya watu wengine,” alisema Morrow.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles