24.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

‘Mapanki’ yazua balaa Mwanza

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John MongellaNa BENJAMIN MASESE – MWANZA

MWENYEKITI wa Serikali ya Mtaa wa Kanindo, Ndalawa Masibuka, ameahidi kuwaongoza wananchi kuwaondoa kwa nguvu wafanyabiashara wanaojihusisha na ununuzi, ukaushaji wa masalia ya samaki walioondolewa minofu maarufu kama ‘mapanki’, ifikapo Agosti 30, mwaka huu.

Kwa muda mrefu wananchi wa mitaa ya Kishili na Kanindo wanataka biashara ya ukaushaji ‘mapanki’ kuondolewa kwenye makazi yao baada ya visima vya maji wanayotumia majumbani kuwa na harufu ya samaki.

Mbali na hayo, wananchi hao wanadai kuwa maji hayo pia hubadilika rangi, na kuwa na ladha ya chumvi chumvi, huku miti na mazao mengine yakiendelea kukauka na harufu mbaya ikiendelea kusambaa kwenye makazi yao.

Wakati wananchi wakiweka kusudio hilo, msimamizi mkuu wa wafanyabiashara hao, Rusi Kasubi,   akizungumza na MTANZANIA jana, alimtaka Ndalawa asikurupuke kuwaongoza wananchi kwenda eneo hilo Agosti 30,  kwani anaweza kujikuta anaingia kwenye migogoro asiyoitarajia.

Alisema anatambua umuhimu wa kuondoa biashara hiyo katika eneo hilo kutokana na uwepo wa makazi ya watu, hivyo anaendelea kutafuta eneo jingine.

Aliongeza  kuwa  licha ya kupokea barua kutoka kwa afisa afya wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza kumtaka kuondoa biashara hiyo, ameomba kuvumiliwa.

“Maofisa afya wa kata na jiji walinitembelea Agosti 19 mwaka huu, tena walikuja na Diwani  wa Kata ya Kishili, Sospeter Ndumi na huyo huyo Ndalawa anayetaka kunifanyia vurugu, tulizungumza na kufikia mwafaka wa kunipa siku 10 kuhama, sasa kunahitajika maandalizi.

“Kuna maeneo zaidi ya 6  yakiwamo Kanyama-Kisesa, Ihayabuyaga kule Magu, Mkolani na Buhongwa ambayo nafuatilia ili kupata eneo, unapohamia eneo lazima kuwe na maji na barabara ili malori yafike, sasa nimpe onyo Ndalawa na kumtaka asikurupuke maana anaweza kuingia kwenye migogoro,” alisema Kasubi.

Kwa upande wake, Ndalawa alisema wamemvulimia Kasubi kwa miaka mingi na amekuwa akipewa siku za kuhama, lakini anakaidi kitendo ambacho kimeleta athari kubwa kwa wananchi kutokana na mimea kukauka kutokana maji ya chumvi chumvi yanayotoka eneo hilo.

Pia alisema  maji ya visima vilivyopo eneo hilo yamebadilika rangi, huku harufu kali ikisambaa katika makazi ya watu jambo ambalo limekuwa likisababisha wananchi kuugua, hivyo alisisitiza kuwaongoza wananchi kumhamisha kwa nguvu ikiwa hatakubali kuondoka ndani ya siku alizopewa na jiji.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella,  aliwapowasili mkoani hapa akitokea Kagera, alipewa malalamiko hayo na kuahidi  kuyaondoa, lakini hadi sasa mvutano kati ya wananchi na wafanyabiashara hao bado unaendelea.

Moja ya mikutano ya kutafuta suluhu kati ya wananchi, na wafanyabiashara hao wa ‘mapanki’, Msafiri Ndalama na Ephaem Manoga waliwahi kusema  hawawezi kuhama eneo hilo kwa sababu shughuli zao zinatambulika katika uongozi wa Jiji la Mwanza na wanalipa kodi.

Maeneo mengine kunakofanyikia shughuli ya ukaushaji wa ‘mapanki’ jijini Mwanza ni Kanyama (Magu), Ibanda (Mkolani Relini), Mwaloni (Kirumba) na Kishili (Igoma).

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles