30.2 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

MAMBO YA KUZINGATIA UNAPOTAKA KUNUNUA VIATU VYA KUKIMBILIA

 

 

Dk. Fredirick L Mashili, MD, PhD

WATANZANIA wengi siku hizi wamehamasika kufanya mazoezi. Kutokana na hamasa hii, kumekuwa na ongezeko kubwa la klabu za kukimbia maarufu jogging clubs.

Lakini pia hivi karibuni kumekuwa na ongezeko kubwa la ushiriki katika mashindano ya mbio ndefu au marathon. Nadhani utakubaliana nami kwamba mashindano haya pia yanazidi kuongezeka siku hadi siku.

Katika vitu muhimu sana kwenye kukimbia ni viatu. Kwa mkimbiaji  wa kulipwa, zoezi la kununua viatu ni sawa na zoezi la kununua gari kwa mtu anayependa magari au kununua nguo kwa mwanamitindo. Hii inatokana na ukweli kwamba miguu yake itatumia muda mwingi ndani ya viatu hivyo zaidi ya sehemu nyingine yoyote.

Swali ni kwamba endapo wewe ni mkimbiaji kwa sababu zozote zile je, unafahamu kwamba ni muhimu kuchagua viatu vya kukimbilia vinavyokufaa?

Nadhani wengi tutakuwa hatufahamu. Kutumia viatu visivyoendana na miguu yako kunaweza kukusababishia kupata maumivu na hata majeraha. Kwa wale ambao wamewahi kupata fursa ya kununua viatu vya kukimbilia nje ya nchi au katika maduka ya kisasa zaidi, watakubaliana na mimi kwamba kabla ya kuamua kuchukua viatu hivyo, utavivaa na kujaribu kukimbia navyo kwenye ‘treadmill’ au utapimwa kwa kutumia kifaa maalumu kisha utapewa ushauri na muuzaji mwenye uzoefu na ujuzi kidogo wa jinsi mwili unavyofanya kazi.

Kwa kuwa hapa kwetu huenda tukawa hatujafikia huko, leo tutajadili mambo makuu mawili ambayo ni muhimu kuzingatia wakati wa kuchagua viatu vya kukimbilia.

Aina ya mguu wako/soli ya mguu

Kwa kifupi ziko aina tatu. Miguu isiyo na uvungu (flat feet), miguu yenye uvungu wa kawaida (normal arch feet) na miguu yenye uvungu mkubwa (high arch feet).

Ni rahisi kufahamu aina ya miguu uliyonayo, ila kuwa na uhakika zaidi onana na wataalamu. Kama mguu wako una uvungu wa kawaida unaweza usiwe na shida sana katika kuamua aina ya kiatu.

Kama mguu wako hauna uvungu, ni muhimu kuchagua viatu vyenye  soli iliyopanda juu kidogo na kuwa nene zaidi sehemu ya katikati, ili kuuzuia mguu usikunjike sana katikati wakati wa kukimbia. 

Kama mguu wako una uvungu mkubwa  ni vema kuchagua viatu vyenye uvungu pia, ambavyo soli yake ni laini sana mbele kwenye vidole na nyuma kwenye visigino.

Sehemu hizi za mbele na nyuma ya mguu wa mtu mwenye uvungu mkubwa,  huweka shinikizo kubwa katika kiatu, hivyo huitaji kuwa laini. Miguu isiyo na uvungu huwa kwenye hatari zaidi ya kuumia kuliko ile yenye uvungu mkubwa.

Aina ya mbio unazokimbia

Wengi wetu tunakimbia kama mazoezi tu, kwa sababu hii huenda isihusike sana. Lakini wapo wengine ambao hata kama wanafanya mazoezi hukimbia kwa spidi kubwa.

Hii ni sawa na kufanya mazoezi ya kukimbia kushiriki mbio fupi (kukimbia kwa kasi kubwa)  au kwa lugha ya kiingereza sprinting. Mtu anayefanya sprinting anahitaji viatu tofauti na yule anayefanya marathon.

Kwa sehemu kubwa, aina ya viatu tuliyoijadili hapo juu inawahusu zaidi  wale wanaokimbia mbio ndefu au wanaofanya mazoezi kwa kukimbia mchaka mchaka (jogging).

Kwa wale wanaofanya sprinting, vinatakiwa viatu vyepesi zaidi lakini vyenye uwezo wa kuuzuia mguu usipate misukosuko inayotokana na shinikizo kubwa la kukimbia mbio fupi.

Mara nyingi viatu hivi huwa na soli nyembamba na nyepesi na huwa na kusheni nyembamba zaidi ukilinganisha na vile vya kufanya jogging.

Viko viatu vya sprinting (kukimbia kwa kasi kubwa) ambavyo huwa na meno au spikes. Meno haya husaidia kudumisha uwiano (balance) kwa mkimbiaji wakati anapokimbia kwa kasi kubwa.

Kwa kifupi hayo ndiyo mambo makuu mawili ya kuzingatia unapochagua viatu vya kukimbilia. Kutokufanya hivyo huweza kuathiri afya ya miguu yako. Yako mambo mengine chungu nzima ikiwamo kujisikia vizuri unapokuwa umevaa viatu na hata uchaguzi binafsi. Kwa maelezo zaidi na vipimo zingatia kuwasiliana na wataalamu.

Dk. Mashili  ni mtaalamu wa fisiolojia ya mazoezi na homoni. Pia ni mhadhiri katika chuo kikuu cha sayansi na tiba Muhimbili (MUHAS). Kwa maelezo zaidi unaweza wasiliana naye kwa kutumia: namba 0752255949, baruapepe, [email protected]. Unaweza pia kujifunza zaidi kwa kutembelea mojawapo ya tovuti zake: www.jamiihealthtz.com au www.jamiiactive.org

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles