30.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

MAMBO YA KUZINGATIA UNAPOMPELEKA MTOTO KITUO CHA MALEZI

SONY DSC

Na CHRISTIAN BWAYA,

WATAFITI wa malezi ya watoto wamejaribu kuangalia namna gani huduma za malezi ya kituoni – day care yanavyoweza kuboreshwa. Moja wapo ya watafiti maarufu katika eneo hili ni Taasisi ya Marekani ya Mtandao wa Afya ya Mtoto na Maendeleo ya Utafiti wa Malezi ya Watoto (NICHD).

Maswali ya msingi yanayojaribu kujibiwa na tafiti hizi ni ikiwa kuna uhusiano wa ubora wa huduma zinazotolewa na vituo hivi na makuzi ya mtoto katika nyanja za kiakili, kihisia, kimwili na kistadi; aina ya mazingira yanayoweza kuhusianishwa na ukuaji mzuri wa kihisia na kiakili kwa mtoto na kiasi cha saa kinachopendekezwa kwa mtoto kulelewa katika kituo kwa siku/juma.

Jambo lililodhahiri ni kwamba huduma hizi zinapoboreshwa hupunguza uwezekano wa changamoto zinazotokana na huduma zisizokidhi viwango. Makala haya yanaangazia vigezo vilivyothibitika kusaidia kuondoa kwa kiasi kikubwa madhara hayo kwa makuzi ya mtoto.

Uwiano wa idadi ya walezi na watoto

Idadi ya watoto wanaoangaliwa na mlezi (mwalimu) mmoja ni muhimu. Ingawa zinaweza kuwapo tofauti za kiutamaduni baina ya nchi na nchi, kwa ujumla tunaweza kusema ni vyema watoto wadogo wakaangaliwa kwa ukaribu zaidi pindi wanapokuwa kituoni.

Kwa mujibu wa NICHD, watoto wenye miezi 6 hadi mwaka 1½, kwa mfano, uwiano wapaswa kuwa angalau watoto watatu wanaoangaliwa na mlezi mmoja. Kwa mwaka 1½ mpaka 2 uwiano unaopendekezwa ni watoto watano kwa mlezi mmoja na kwa miaka 2 mpaka 3, uwiano unaopendekezwa ni watoto saba hadi kumi kwa mlezi mmoja.

Watafiti wengine wanashauri kwa umri usiofikia miezi sita, ni vizuri kila mtoto awe na mlezi wake. Lengo la uwiano huu ni kuwasaidia watoto kupata uangalizi wa karibu unaozingatia mahitaji binafsi ya kila mmoja.

Ukubwa wa makundi ya watoto

Ukubwa wa kituo cha malezi nao ni kigezo kimoja wapo cha ubora wa huduma. Inapendekezwa kuwa watoto wawekwe kwenye makundi madogo yanayoangaliwa na walezi zaidi ya mmoja ili kuwawezesha kufahamiana kwa karibu.

Kufahamiana kunawasaidia kuwapa utulivu wa kisaikolojia na kuwapa fursa walezi kushirikiana kwa karibu katika kuwasaidia watoto.

Kwa mtoto mwenye miezi sita hadi mwaka 1½ inapendekezwa watoto sita wawe kwenye kundi moja, wakiangaliwa na walezi wawili. Mwaka 1½ mpaka 2, watoto nane kwa kundi, wakiangaliwa na walezi wawili.

Tafsiri ya mapendekezo haya katika mazingira yetu, ni kuwa kituo kinahitaji kuwa na walezi wa kutosha kuwaangalia watoto kwa karibu. Hili linawezekana ikiwa kituo unachofikiri kumpeleka mwanao kitakuwa kimesajiliwa na mamlaka zinazohusika.

Mafunzo kwa walezi

Ubora wa kituo pia unategemea ubora wa mafunzo waliyonayo walezi. Inashauriwa walezi wawe wamejifunza angalau mambo ya msingi kuhusu makuzi. Mafunzo hayo yatawasaidia kujua namna ya kufanya kazi na watoto kwa kuzingatia mahitaji yao maalumu.

Katika nchi yetu, tunavyo vyuo vinavyotoa mafunzo ya elimu ya awali kwa ngazi ya Astashahada, Stashahada na hata Shahada. Ni muhimu kuwatumia walimu hawa kufanya kazi ya kuwalea watoto katika vituo hivi.

Walezi wanapokuwa na uelewa wa mahitaji ya watoto, watakuwa kwenye nafasi ya kujua aina ya vifaa vinavyowasaidia watoto kujifunza kulingana na mahitaji yao; aina ya michezo inayowafaa watoto na mambo kama hayo.

Itaendelea…

Mwandishi ni Mhadhiri wa Saikolojia Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge. Blogu: http://bwaya.blogspot.com, 0754870815.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles