MAMBA ANAYEABUDIWA KAMA MUNGU NIGERIA

0
390

JOSEPH HIZA NA MITANDAO


WATU huwa na imani tofauti na huabudu vitu vingi duniani, nchini Nigeria kuna kabila moja ambalo humuabudu mamba kama mungu.

Utamaduni wa kuabudu mamba hata hivyo si mgeni, kwani ulikuwa ukiendeshwa katika Misri ya kale.

Mabaki ya mamba akiwa na mamba wadogo 20 yalichimbuliwa huko Kom Ombo, katika hekalu na eneo la makaburi mwaka 1893, kwa mujibu wa gazeti la Telegraph.

Katika kipindi hicho, mamba mkubwa aliabudiwa kama mungu Sobek, mjusi aliyemwongoza mungu wa Kimisri na alitendewa kwa heshima na makuhani, kwa mujibu wa ripoti, inasemekana alikuwa kiashiria cha madaraka na rutuba.

Tukirudi nchini Nigeria, mamba huyo wanayemwabudu kwa sasa ana umri wa miaka 78, ambapo wakazi wa eneo hilo la Oje viungani mwa mji wa Ibadan kusini magharibi mwa Nigeria humuenzi na wanaamini kwamba anaweza kujibu maombi yao.

Wakazi huwa wanamrushia kuku kama zawadi kumshawishi kutimiza maombi yao, wengine humpa mbuzi.

Mamba huyo humilikiwa na familia ya Delesolu ambayo imekuwa ikimfuga kama mnyama kipenzi. Anadaiwa kuanza kufugwa na familia hiyo kuanzia mwaka 1940 baada ya mamba mwingine aliyekuwa akifugwa kabla yake kuchukuliwa na Wazungu.

Ajabu ni kwamba, familia hiyo yenyewe huwa haiamini kwamba ana nguvu zozote za kipekee kama ambavyo kiongozi wa sasa wa familia hiyo ya Delesolu, Raufu Yesufu anasema:

“Kwa sababu ya imani yetu, sisi ni Waislamu, hatuamini kwamba ana nguvu zozote.”

Lakini hilo huwa haliwazuii watu kuendelea na imani zao.

Anasema waganga wa kienyeji na matabibu wengine huwa wanafika kwa sababu mbalimbali kutafuta msaada.

Baadhi hufika kuomba usaidizi katika kuwaponya wagonjwa au kuwasaidia watu wanaotatizika kushika mimba.

Familia hiyo huwa haiwazuii kufika kumuomba mamba huyo ambapo huwa wanampa kuku.

Watu wamekuwa wakifika kwa mamba huyo kwa muda mrefu, baadhi wakiwa na maombi ya ajabu.

Wapo wanaofika wakitaka kuchukua kinyesi chake na wengine kutaka kuchota maji kutoka kwa kidimbwi anamoishi.

Yesufu anasema kinyesi hicho na maji hayo baadaye hutumiwa na waganga au watu binafsi kama tiba.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here