Na Renatha Kipaka
BAADHI ya mama tilie katika Manispaa ya Bukoba  Kagera wanalia na ukata kutokana na vyakula vyao  kukosa wateja.
Kauli hiyo  ilitolewa kwa nyakati tofauti na kina mama hao  katika soko kuu la Bukoba
Hao ni  Fatima Abduri, Mariam Jabili na Koku Mgisha.
Akizungumzia hali hiyo, Fatima   alisema tangu ameanza kufanya biashara hiyo sasa ni miaka 10 lakini hivi sasa mambo yamekuwa tofauti  kufikia   kupika kilo moja ya mchele wakati alikuwa akipika kilo 10 kwa siku.
“Siku zilizopita nilikuwa napika kilo 10 na wakati mwingine zaidi ya hapo lakini sasa ninapika kilo moja nayo haiishi.
“Hivi sasa wakati mwingine  ninatoka nyumbani nawaacha watoto   hawana uhakika wa kula, yaani inasikitisha,”alisema mama huyo.
Naye Mariam  alisema    ushuru nao ni tatizo kwa sababu mkusanyaji  ushuru hajui siku hiyo wameuza au hawajauza.
Alisema   ushuru huwa wanalipa Sh 13,000 kwa mwezi, inafika wakati fedha hiyo inakosa kutokana na ugumu uliopo.
“Mimi kipindi kilichopita nilikuwa na uwezo wa kupika ndizi mikungu miwili, mchele kilo 15 na vina kwisha.
“Nikifika nyumbani familia yangu inaishi kwa furaha lakini sasa imekuwa tofauti kama ninauza Sh 2,000   wakati nina watoto sita si hatari hiyo,”alisema.
Koku Mgisha alisema baada ya kuona anapika chakula anakimwaga kwa kukosa wateja,  kukigawa au wakati mwingine kukikopesha, aliona ni bora afunge biashara  na kukaa  nyumbani kwake Rwamisenye.
“Wakati mwingine nasema kuwa wakati wa mwezi mtukufu hali huwa inakuwa hivi ingawa wakati huu imekuwa tishio.
“Mimi kwa upande wangu nitumie nafasi hii kuiomba serikali kuwapunguzia mama ntilie ushuru … kipato ni kidogo  na asilimia kubwa   tunategemewa na familia kwa maana ya watoto,” alisema Mgisha.
Alisema miaka iliyopita alikuwa akipata hadi Sh 20,000  kwa siku  kama faida na mtaji pembeni.