27.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 18, 2024

Contact us: [email protected]

MALINZI, MWESIGWA WARUDISHWA RUMANDE

Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi, akielekea kupanda gari la Magereza kurudishwa rumande baada ya kesi inayomkabili ya utakatishaji wa fedha kuahirishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam jana. Picha na Imani Nathaniel.

Na ADAM MKWEPU-DAR ES SALAAM

RAIS wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi, Katibu wake Celestine Mwesigwa na Mhasibu, Nsiande Isawafo Mwanga wamerudishwa tena rumande hadi Julai 17, mwaka huu kesi hiyo itakapotajwa tena.

Viongozi hao ambao walipandishwa kizimbani jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, walirudishwa rumande kufuatia upelelezi wa shauri hilo kutokamilika.

Wakili Mwandamizi wa Serikali, Nassoro Katuga, alidai mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Wilbroad Mashauri, kuwa upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika.

Wakili huyo pia aliiomba mahakama kuuonya upande wa utetezi, kuacha kuingilia kesi hiyo kwa kuzungumza nje ya mahakama.

“Ni kinyume cha utaratibu kuishawishi mahakama nje, hoja zote ziletwe mahakamani na kujadiliwa na vyombo vya habari viripoti bila kuharibu mwenendo wa kesi, kwa sababu upande wa Jamhuri hauwezi kuhamisha mahakama na kuipeleka katika chombo cha habari kama walivyofanya wenzetu,” alidai Katuga.

Hakimu Mashauri aliwataka upande wa utetezi kufuata sheria na kama hawajaridhika wakate rufaa Mahakama Kuu na si kwenye vyombo vya habari.

“Nilitarajia wakili (wakili wa utetezi) anajua taratibu, kama hamjui sheria msije mahakamani. Kuwa wakili si kwamba unaweza kusema lolote, ama kusema ovyo ovyo tu, sivyo tulivyoapishwa.

“Hatuwazuii kusema lakini fuateni sheria, kama hamkuridhika kateni rufaa Mahakama Kuu na si kwenye vyombo vya habari.

“Si sahihi kupotosha umma hata kama ukiwa wakili wa Mahakama Kuu, suala hili hata upande wa utetezi wenyewe wanatambua kuwa mashtaka ya utakatishaji fedha hayana dhamana,” alisema Hakimu Mashauri.

Hakimu Mashauri aliahirisha kesi hiyo hadi Julai 17, mwaka huu itakapotajwa tena na watuhumiwa walirudishwa rumande, huku akitaka upelelezi ukamilike ndani ya siku 90.

Watuhumiwa hao wanakabiliwa na mashtaka 28 ya kughushi na kutakatisha fedha kupitia akaunti ya TFF iliyopo katika Benki ya Stanbic, Dar es Salaam.

Malinzi, Mwesigwa na Nsiande wanatuhumiwa kutenda kosa la utakatishaji wa fedha Dola za Marekani 375, 418 (zaidi ya Sh milioni 840) wakati wakijua fedha hizo ni matokeo ya mapato ya kughushi.

Shtaka jingine ambalo liliwahusisha Malinzi na Mwesigwa ni kutoa fedha hizo kwa njia ya kughushi katika Tawi la Benki ya Stanbic iliyopo Kinondoni, ikiwa ni kinyume cha sheria wakati Nsiande, alikutwa na kosa la kushirikiana na viongozi hao kujipatia kiasi cha fedha hizo, huku wakitambua ni mapato ya kughushi.

Wakati Malinzi na wenzake wakiendelea kusota rumande, Kamati ya Utendaji ya TFF imepanga kukutana leo kwa dharura, ambapo pamoja na ajenda nyingine itatathmini mwenendo wa kazi za Kamati ya Uchaguzi ya shirikisho.

Kaimu Katibu Mkuu wa TFF, Salum Madadi, alisema kwamba kamati hiyo ya utendaji inakutana kwa dharura kwa mujibu wa Ibara ya 35 (1) ya Katiba ya TFF inayosomwa pamoja na Ibara ya 35 (6).

Kamati hiyo inakutana baada ya barua ya Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi, Wakili Revocatus Kuuli, kudai kwamba kuna mitazamo tofauti ya kiuamuzi inayosababisha kutokamilisha majukumu yao kwa asilimia 100 kutoka hatua moja hadi nyingine wakati huu wa mchakato wa uchaguzi.

Dosari hiyo ilisababisha Wakili Kuuli kusitisha mchakato wa uchaguzi huo kwa muda hadi utakapotangazwa tena.

Inadaiwa kuwa baadhi ya wajumbe wa kamati hiyo, wanataka Malinzi apitishwe kutetea kiti chake bila kufanyiwa usaili, jambo lililopingwa na Kuuli.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles