29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

MALIASILI, TAMISEMI KUAMUA MGOGORO MSITU

Na HAMZA TEMBA -TABORA

NAIBU Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga, amesema Wizara yake itakutana na Wizara ya Tamisemi na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, kwa ajili ya kutoa uamuzi wa kumaliza mgogoro wa mpaka baina ya Hifadhi ya Msitu wa North Ugala na vijiji jirani vya Kangeme, Utenge na Mtakuja, wilayani Urambo.

Hayo aliyasema jana mkoani Tabora, wakati wa ziara yake ya kikazi ya siku mbili mkoani humo, kwa lengo la kutafuta suluhu ya mgogoro huo pamoja na kuzungumza na watumishi wa vituo vya taasisi zilizopo chini ya wizara yake.

Akiwa mkoani humo alitembelea eneo lenye mgogoro, akafanya mkutano wa hadhara na wananchi na viongozi mbalimbali wa Serikali kwa ajili ya kupata majibu ya utatuzi wake.

Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kijiji cha Kangeme, mkazi wa kijiji hicho, Ramadhan Rashid, alisema wananchi wa vijiji hivyo wanailalamika Serikali kupitia Wakala wa Huduma za Misitu kwa kusogeza mpaka wa hifadhi hiyo hadi ndani ya ardhi ya vijiji wakati wa zoezi la uwekaji wa vigingi vipya vya mpaka wa hifadhi na vijiji hivyo. Alisema eneo hilo ni la vijiji hivyo tangu mwaka 1988.

Naye Meneja wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania Kanda ya Magharibi, Peter Maiga, alisema hifadhi hiyo ilianzishwa mwaka 1956, ikiwa na hekta 165,282, huku mipaka yake halisi ikiwa haijabadilishwa. Alisema zoezi la uwekaji wa vigingi vipya vya mpaka lilizingatia mipaka halisi kwa kutumia mfumo wa GPS.

Kwa upande wake, Mbunge wa Urambo, Magreth Sitta (CCM), alisema idadi ya wananchi inaongezeka, huku maeneo yakiwa hayaongezeki, hivyo akaiomba Serikali ione uwezekano wa kuwaongezea wananchi maeneo ya kulima na kuendeshea maisha yao.

Akijibu malalamiko na maombi ya wananchi hao wa Urambo, Naibu Waziri Hasunga alisema Serikali ya awamu ya tano imedhamiria kutatua kero za wananchi sambamba na kuwaletea maendeleo.

“Baada ya kukagua eneo hili na kusikiliza pande zote, tunakwenda kukaa pamoja na Wizara ya Tamisemi na Wizara ya Ardhi tuangalie ramani zote zilizopo, Matangazo ya Serikali (GN) na taarifa mbalimbali ili tujiridhishe ni ipi mipaka halali tufikie ufumbuzi wa mwisho, migogoro ya namna hii haiwezi kwisha bila kushirikisha wizara hizi.

“Nawaagiza watendaji wangu kwenye taasisi mshirikiane na wananchi muwaelimishe na mzuie wasiendelee na uharibifu hadi hapo tutakapopata suluhu ya mgogoro huu,” alisema Hasunga.

Katika hatua nyingine, Naibu Waziri Hasunga aliwataka wananchi wa vijiji hivyo kujiepusha na vitendo vya kuingiza mifugo kwenye maeneo ya hifadhi. “Mkiingiza mifugo tukaikuta tutaitaifisha kwa mujibu wa sheria,” alisema Mhe. Hasunga.

“Asali ina soko zuri duniani kwa sasa, bei yake ni nzuri, kila mtu afuge tuchangie uchumi wa taifa letu,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles