30.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Malecela atoa kauli nzito kutekwa Mo

Na EVANS MAGEGE – Dar es Salaam


WAKATI giza nene likiwa bado limetanda juu ya tukio la kutekwa nyara na mahali alipo mfanyabiashara maarufu nchini, Afrika na duniani, Mohammed Dewji maarufu pia kwa jina la Mo, Waziri Mkuu mstaafu, John Malecela ametoa kauli nzito juu ya tukio hilo.

Akizungumza na MTANZANIA Jumapili katika mahojiano maalumu yaliyofanyika juzi nyumbani kwake Sea View, Upanga, Dar es Salaam, Malecela alivishangaa vyombo ya dola kwa kushindwa kujipanga sawasawa.

Malecela ambaye katika mahojiano hayo alizungumzia pia kumbukizi ya Mwalimu Julius Nyerere inayoadhimishwa leo na hali ya siasa nchini, alisema anasikitishwa na tukio la Mo kutekwa nyara pamoja na matukio mengine ya aina hiyo yaliyopata kutokea siku za nyuma.

Alishangaa vyombo vya dola kushindwa kujipanga kwa kadiri maendeleo yanavyokua na uhalifu unavyoongezeka.

Malecela ambaye amepata kuhudumu katika nafasi mbalimbali za uongozi kuanzia Serikali ya awamu ya kwanza na zaidi akiwa Waziri Mkuu kwa takribani miaka minne (1990-1994) katika Serikali ya awamu ya pili chini ya Rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi, alisema vyombo vya usalama vilipaswa kusoma alama za nyakati miaka mitano iliyopita.

Alisema vyombo hivyo vilipaswa kutambua miaka mitano iliyopita kwamba ipo siku taifa litafikia katika kiwango hiki cha uhalifu wa watu kupotea, kutekwa nyara au kujeruhiwa na watu wasiojulikana.

Malecela alisema kama taifa haitoshi kila siku kikitokea kitu kipya watu washangae, badala yake uwekwe utaratibu madhubuti wa kufanya tathmini ya kila siku kuangalia mbele zaidi usalama wa raia.

“Hivi kweli kwa vyombo vya usalama, miaka mitano iliyopita havikujua kwamba tutafika hapa? Kwamba Tanzania itakuwa na wahalifu kama Nigeria, ambako wahalifu 20 au 30 wanaweza kuvamia mtaa, wakateka watu nyara au wakachukua vitu na kutoweka chini ya nguvu ya mtutu?” alihoji Malecela.

Alisema mtazamo wake vyombo vya usalama lazima vifanye tathmini juu ya mambo yajayo na kujitayarisha kwa sababu uhalifu unaotokea hapa nchini hauwezi ukatajwa kuwa si wa kawaida, kwamba haujawahi kutokea duniani.

“Hivi matukio ya kuibiana watoto, watu kutekwa nyara haijapata kutokea sehemu nyingine duniani? Na sisi Tanzania kwa sasa kama tusipojiangalia, uhalifu wa Afrika Kusini utahamia kwetu, hivyo kuanzia sasa hatuna budi kujitayarisha,” alisema Malecela.

Alisema kadiri taifa linapokuwa na watu wengi ndipo hali ya uhalifu huongezeka, hivyo ni jukumu la vyombo vya usalama kujitayarisha kwa kuweka mbinu mahususi za kushinda uhalifu.

“Hatuwezi kukaa na kuanza kuomboleza kutekwa watu nyara, tuliona wenzetu Kenya mambo haya yalianza siku nyingi wakina Kariuki (Josiah Mwangi Kariuki, mwanasiasa na mmoja wa viongozi mara baada ya Kenya kupata uhuru) walipotea hivi hivi.

“Kenya wanasiasa wengi walipotea hivi hivi, watu kuuawa,  mfano marehemu Tom Mboya (Waziri wa zamani wa Kenya na mwanasiasa machachari wa Kanu), haya yalikwisha tokea kwa nini yasitokee na Tanzania?

“Kama uhalifu huu upo lazima tujitayarishe na ninatoa pole kwa wenzetu ambao wamepoteza watoto wao na ndugu zao na pia nasikitika sana, lakini ni mambo ambayo yatatokea na yataendelea kutokea.

“Kwa upande wa Jeshi la Polisi wasipopata msaada wa raia watakuwa na wakati mgumu kudhibiti uhalifu, kwa sababu raia hao hao wanaopiga kelele kulaumu polisi ndio unakuta hao hao wamehifadhi wahalifu,” alisema Malecela.

TUKIO LA MO KUTEKWA

Mo alitekwa nyara na watu wasiojulikana Alhamisi alfajiri katika Hoteli ya Colosseum, Oysterbay, Dar es Salaam, mahali ambako amekuwa akienda kufanya mazoezi ya mwili (gym).

Tukio la Mo kutekwa nyara na watu wasiojulikana ni mwendelezo wa matukio mbalimbali ambayo yametokea hapa nchini.

Miongoni mwa matukio hayo ni pamoja na lile la kupotea kusikojulikana kwa Mwandishi wa Gazeti la Mwananchi, Azory Gwanda, kada wa Chadema Ben Saanane na kushambuliwa na watu wasiojulikana kwa risasi Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu na mengine kadhaa yenye kufanana na hayo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles