22.8 C
Dar es Salaam
Thursday, April 18, 2024

Contact us: [email protected]

Makosa ya kimalezi wanayofanya wazazi waliofanikiwa

Na CHRISTIAN BWAYA

MAJUZI nilizungumza na rafiki yangu mmoja aliyestaafu utumishi wa umma miaka kadhaa iliyopita. Mzee huyu ana vijana wawili ambao kwa sasa ni watu wazima. Wote wawili ni wasomi wenye elimu ya kiwango cha chuo kikuu na wana umri wa zaidi ya miaka 30.

Katika mazungumzo yetu, mzee hakufurahia maisha waliyokuwa wanaishi vijana wake hao.

“Wote wawili naishi nao hapa nyumbani. Hawataki kuajiriwa na hakuna mwenye dalili ya kuwa na familia inayoeleweka,” anasema kwa masikitiko na kuendelea:

 “Huyu wa kwanza mwenye miaka 39 sasa amezaa na mwanamke mmoja hata sijui alimtoa wapi. Walijaribu kuishi hapo Survey kwa miezi sita maisha yakawashinda. Imebidi waje kuishi hapa nyumbani,”

“Huwa nikifikiria nasikitika. Hawa vijana wakiwa wadogo niliwapa kila walichokihitaji. Unajua nilipitia maisha magumu enzi za ujana wangu. Tulitoka kwenye familia duni. Sikupenda na wanangu nao wapate shida. Nilijitahidi kuhakikisha hawapitii shida nilizopitia mimi,” anakumbuka kwa masikitiko.

Nilimtazama rafiki yangu vile anavyojisikia fedheha kuelezea mambo ya namna hii. Najua katika umri wake angependa kuwa na simulizi la mafanikio ajisikie kama mtu mwenye mafanikio. 

Huku akinitazama kama mtu anayejisikia hatia, alijisemea: “Sijui nilikosea wapi. Huwa najiuliza hili swali mara kwa mara. Vijana wakubwa namna hii hakuna kitu wanafanya. Uwezo wa kufikiri maisha ni kama hawana pamoja na kuwa na hizo ‘degree’ walizonazo.

“Wakati mwingine najuta. Naona nimechelewa. You get my point? (Sijui unanielewa?) Mtu huwezi kuwa na amani kuwa na mijitu mikubwa hivi haijui kazi. Miaka mitatu imepita nilimkabidhi [mmoja wao] biashara aiendeshe. He was so rough (hakuwa anafanya mambo yake kwa utaratibu) ilibaki kidogo biashara ifilisike. To cut the story short (kufisha habari) ilibidi nimwondoe,” anatikisa kichwa kwa uchungu.

Kwa ujumla vijana wa mzazi huyu hawakuwa wanafahamu maisha. Walitegemea kupata mahitaji yao mengi kwa baba yao ambaye kimsingi tungesema ilikuwa zamu yake sasa kutunzwa na watoto wake. Je, nini kimefanya watoto wawe na uzembe wa kiwango hiki?

Kuna ukweli kwamba watoto wanaokulia kwenye mazingira yenye kila kitu wanakuwa kwenye hatari ya kunyimwa changamoto. Wanakulia kwenye mazingira ambayo karibu kila wanachokipata kinapatikana. Mtoto akiomba fedha za matumizi hakosi. Mzazi anaamini kwa kumpa kila anachokihitaji basi mtoto atakuwa na utulivu wa kujifunza maisha.

Hata hivyo, watoto hawa mara nyingi wanakuwa tofauti na wenzao wanaokulia kwenye maisha ya uhitaji. Shida ya kukosa mahitaji ya kila siku, shida zinazomfanya ajione mtu duni akilinganisha na wenzake wenye nafuu zinaweza kuwa motisha kubwa ya kumsukuma kijana kupanua ufahamu wake. Shida zinakuwa mwalimu wa maisha ya mtoto. 

Tunawafahamu watu wengi waliokulia kwenye familia duni lakini waliweza kufika mbali. Watu hawa walikosa ada ya shule, walibangaiza fedha za matumizi lakini kupitia changamoto hizi wakajifunza namna ya kupangilia matumizi, namna ya kuishi na watu ili kupata msaada na hata kujifunza uvumilivu mambo yanapokuwa magumu.

Ipo sababu ya mzazi mwenye mafanikio kumsaidia mtoto kutafuta maisha yake. Badala ya kumpa kila senti anayohitaji, mathalani, ni vizuri kumtengenezea mtoto upungufu kidogo utakaomsaidia kujenga nidhamu ya kile alichonacho. Kwa kufanya hivi, mtoto atajifunza namna ya kukabiliana na upungufu hali itakayomfunza upande wa pili wa maisha.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles